Featured Post

WAKAZI WA UKEREWE MKOANI MWANZA WATAKIWA KUITUMIA MELI MPYA NA YA KISASA, MV NYEHUNGE II KUJIINUA KIUCHUMI

Mwonekano wa Mv Nyehunge kwa ndani, sehemu ya abiria kukaa.

Na George Binagi-GB Pazzo @BMG
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, mwishoni mwa wiki amefanya uzinduzi wa Meli Mpya ya Mv Nyehunge ya pili (II) inayofanya safari zake kati ya Mwanza na Ukerewe na kuwataka wakazi wa Ukerewe kuitumia fursa hiyo kujiinua kiuchumi.

Mongella alisema Meli hiyo itasaidia kuondokana na adha ya usafiri kwa wakazi wa Visiwa vya Ukerewe kwa kuwa imeongeza idadi ya Meli zinazofanya safari kati ya Jiji la Mwanza na visiwa hivyo.

Aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo kusafirisha bidhaa zao kati ya Ukerewe na Jiji la Mwanza ili kujiinua kiuchumi huku akisisitiza Kampuni ya Nyehunge inayomiliki Meli hiyo kuzingatia vigezo vya usalama katika uendeshaji wa safari zake.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Nyehunge, Said Mohame, alisema Meli hiyo inaongeza safari kati ya Visiwa vya Ukerewe na Jiji la Mwanza na kufikia safari tatu kwa siku huku suala la nauli nafuu likizingatiwa ili kuondoa changamoto ya usafiri waliyokuwa nayo wakazi wa Ukerewe. Nauli za Ukerewe katika Meli hiyo ni Shilingi 6,000 kwa 7,000.

Baadhi ya wasafiri wa Ukerewe walipongeza ujio wa Meli ya Mv Nyehunge ambapo wamebainisha kwamba itawasaidia kusafirisha kwa wakati bidhaa na mazao ya chakula kati ya Ukerewe na Jiji la Mwanza.

Meli hiyo ya Mv Nyehunge II ina uwezo wa kubeba abiria 500, magari madogo 40 na tani 284 za mizigo ambapo imejengwa na kampuni ya wazawa ya Songoro Marine Transport ya Jijini Mwanza kwa zaidi ya shilingi Milioni 800.
Tazama HAPA Uzinduzi Ulivyokuwa

Comments