Featured Post

HATARI: AINA 100 ZA WANYAMA WA KUFUGA ZATOWEKA DUNIANI, NYINGINE 1458 HATARINI!





Imeandaliwa na MaendeleoVijijini Blog
JANUARI 2016, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) lilitoa ripoti inayoeleza kwamba wafugaji na watunga sera ulimwenguni walikuwa wakihangaika katika kutunza baioanuai ya wanyama ili kuongeza uzalishaji na akiba ya chakula katika sayari yenye joto kali na msongamano wa watu.
Lakini shirika hilo likaonya kwamba, kutokana tafiti mbalimbali zinazofanywa katika kutafuta aina ya wanyama chotara au wa kutengeneza watakaomudu matarajio ya uzalishaji bora, kuna hatari ya jamii muhimu za asili za wanyama kutoweka na kutaka ziwepo juhudi za makusudi za utafiti endelevu wa wanyama chotara (genetic breeds).

Kwa mujibu wa Ripoti ya Pili isemayo The State of the World'sAnimal Genetic Resources for Food and Agriculture, ambayo MaendeleoVijijini inayo nakala yake, asilimia 17 (jamii 1,458) za wanyama wa kufuga duniani ziko hatarini kutoweka kabisa, wakati hali ya kutoweka kwa wanyama wengine (asilimia 58) haijulikani kutokana na kutokuwepo kwa takwimu kuhusu wingi na uwepo wa wanyama hao.
Inaelezwa kwamba, karibu jamii 100 za wanyama wa kufugwa zimetoweka duniani katika kipindi cha mwaka 2000 na 2014.
Rekodi za nchi mbalimbali zinaonyesha kwamba, uzalishaji wa wanyama kwa kutumia jamii tofauti tofauti (cross-breeding) ndio unaosababisha kutoweka kwa jamii za asili za wanyama hao.
Changamoto nyingine inayosababisha kutoweka kwa wanyama ni matumizi ya wanyama wasio wa asili ya nchi husika (non-native breeds), sera dhaifu na taasisi zinazosimamia sekta ya mifugo, kutoweka kwa mfumo wa asili wa uzalishaji wanyama, na kupuuza kwa jamii za wanyama ambazo zinaelezwa kwamba hazina ubora katika upande wa uzalishaji wa kibiashara.
Ulaya na eneo la Caucasus, na Marekani ni maeneo mawili duniani ambayo yako katika hatari zaidi ya kutoweka kwa wanyama wa asili na kwa maana nyingine, idadi kubwa ya jamii ya wanyama wa kufuga walio hatarini kutoweka iko Ulaya na eneo la Caucasus.
Maeneo yote hayo yanaelezwa kwamba yana viwanda vinavyotumia baadhi tu ya wanyama katika kuzalisha bidhaa zao na wanatumia jamii wachache sana za wanyama hao.

Kwanini baioanuai ni muhimu
MaendeleoVijijini inaamini kwamba, jenetiki zinatoa fursa kwa wakulima na wafugaji kuboresha jamii zao za mifugo na kuendana na idadi ya wanyama katika mabadiliko ya kimatingira na mabadiliko ya mahitaji.
"Kwa maelfu ya miaka, wanyama wa kufuga kama kondoo, kuku na ngamia, wametoa mchango wa moja kwa moja kwa maisha na usalama wa chakula kwa mamilioni ya watu," alisema Mkurugenzi Mkuu wa FAO José Graziano da Silva, "Hiyo inahusisha asilimia 70 ya watu maskini duniani ambao kwa sasa wanaishi vijijini."
"Baioanuai ya wanyama ni muhimu kuiangalia katika changamoto zijazo," kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu, ambaye aliongeza wakati huo kwamba ripoti hiyo "kusisitiza jitihada bora za kuhakikisha aina za wanyama zinatumika na kuendelezwa ili kuongeza uhakika wa chakula duniani, na waendelee kuwepo kwa vizazi vijavyo."
Miongoni mwa changamoto zilizopo na zijazo ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, kuibuka kwa magonjwa mbalimbali, uhaba wa ardhi na maji, mahitaji ya soko lisilotengemaa, ambazo zinaonyesha umuhimu kuliko hata awali wa kuhakikisha akiba (genetic resources) ya aina bora za asili za wanyama zinatunza na kutumiwa kwa matumizi endelevu.
Kwa sasa, spishi 38 na jamii tofauti 8,774 za ndege wa kufuga na wanyama zinatumiwa kwenye kilimo na uzalishaji wa chakula.

Kuanzisha akiba ya mbegu asilia
Jumla ya nchi 129 zilishiriki katika uhakiki mpya wa dunia, ambao ulikuja takriban mlongo mmoja baada ya kufanyika uhakiki wa kwanza wa akiba ya mbegu za wanyama (animal genetic resources) mwaka 2007.
"Takwimu tulizokusanya zinaonyesha kwamba kuna jitihada zilizofanyika kupunguza idadi ya wanyama walio hatarini kutoweka tangu uhakiki wa kwanza ulipofanyika," alisema Beate Scherf, Ofisa Mifugo wa FAO na mwandishi mwenza wa ripoti hiyo. "Na serikali kwa ujumla zimechukua hatua za kunusuru kutoweka kwa aina hizo za wanyama na wanatunza vyema aina zao za asili."
Ripoti hiyo inaonyesha kwamba serikali zimeendelea kutambua umuhimu wa matumizi na maendeleo endelevu ya aina asilia za wanyama.
Wakati FAO ilipochapisha uhakiki wa kwanza mwaka 2007, kulikuwa na nchi zisizofikia hata 10 ambazo ziliripoti kuanzisha akiba ya mbegu asilia. Idadi hiyo kwa sasa imeongezeka hadi kufikia nchi 64, na nyingine 41 zina mipango ya kuanzisha akiba za mbegu hizo (gene bank), kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa mapema Januari 2016.
Na jitihada hizi zinazaa matunda, mtaalamu huyo anasema: "Katika kipindi cha mlongo uliopita, nchi kadhaa barani Ulaya zimewekeza sana katika kujenga mifumo ya kubadilishana taarifa na uanzishaji wa akiba za mbegu kama tahadhari ya kiusalama," kwa mujibu wa Scherf.
Ushirikiano wa kikanda kama taasisi mpya ya European Gene Bank Network (Eugena) ni muhimu katika kudhibiti na kuboresha jamii za wanyama kwa siku zijazo, na zinapaswa kuungwa mkono na wahifadhi wa wanyama hai katika mazingira yao ya asili.
Uhifadhi wa wanyama hai pia unatambua utamaduni na thamani ya mazingira ya kuwepo kwa idadi ya kutosha ya wanyama hai wa jamii tofauti.
Nchi 177 tayari zimekwishaanzisha Waratibu wa Kitaifa na nchi 78 zimeanzisha makundi ya ushauri yanayohusisha wataalamu kutoka sekta mbalimbali na kusimamia jitihada za kitaifa katika kutunza jamii asilia za wanyama.

Kuongezeka kwa biashara ya mbegu
MaendeleoVijijini inaamini kwamba, hali hiyo imekuja katika kipindi cha kupanua soko la dunia la ufugaji wanyama na mbegu za mifugo (livestock semen), mara nyingi kwa malengo ya kupandisha wanyama wa jamii tofauti, huku nchi nyingi zinazoendelea zikiwa waagizaji wakuu ingawa baadhi zinasafirisha nje mbegu hizo.
Wakulima na watunga sera katika nchi zinazoendelea wamebariki uagizaji wa mbegu chotara kama njia ya kuongeza uzalishaji wa mifugo yao – kuongeza wingi wa maziwa, kwa mfano, au kupunguza umri wa asili wa ukuaji wa mnyama.
Lakini kama mipango haiku sawa, upandishaji wa aina tofauti za wanyama unaweza kushindwa kupunguza uzalishaji na kusababisha kupotea kwa tabia kama vile uwezo wa kukabiliana na mazingira ya joto kali, uhaba wa maji, malisho duni, mazingira yasiyoridhisha, uwanda wa juu na changamoto nyinginezo za mazingira ya uzalishaji.

(Makala haya imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com, simu: 0656-331974, kwa hisani ya UN News).

Comments