Featured Post

YANGA-UKUTA, YANGA-KATIBA HAZIKUIZUIA YANGA KUTWAA UBINGWA 1987




Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
Msimu wa 1987 ulianza kwa migogoro katika klabu ya Yanga ambapo kulikuwa na pande mbili zilizokuwa zinapingana. Upande wa uongozi ulikuwa unajiita Yanga-Ukuta naupande wa wanachama waliokuwa wakiupinga uongozi walijiita Yanga-Katiba. Mgogoro huo ulisababisha Yanga ipeleke orodha mbili za usajili FAT.
Mwenyekiti wa Yanga wakati huo, William 'Billy' Bandawe alikuwa analalamikiwa kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na ufujaji wa fedha. Hali hiyo ilisababisha wafadhili wanne wa Yanga wakati huo, Salehe Sultan Hamad, Ali Mohamed, Felician Ferdnand na Juma Said kumsusa Bandawe na kutangaza kwamba wasingetoa misaada tena kama angeendelea kuwepo madarakani.

Kwa upande mwingine wanachama wa Yanga waliokuwa wanapinga uongozi walimlalamikia mwenyekiti wa FAT wakati huo, Said Hamad El-Maamry kwamba alikuwa anausaidia upande wa uongozi ili aendelee kubaki madarakani.
Mgogoro huo ulipelekwa Mahakama Kuu na baadaye pande zote mbili zilizokuwa zinapingana kukutana na Rais wa Awamu ya Pili wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Ally Hassan Mwinyi, pamoja na mawaziri wote Ikulu kuangalia uwezekano wa kusuluhisha mgogoro huo.
Wanachama waliokuwa wanapinga uongozi waliunda kamati ya watu 13 ambayo ilikuwa na Abdallah Mwamba (Mwenyekiti), Cleophas Kanwa (Katibu), na wajumbe walikuwa S. Sarumanya, S. Omary, Salum Mohamed, Valisanga Mkonjera, D. Othuman, B. Ntila, J. Kayombo, R. Gwao, S. Makule, H. Onyango na Salehe Sultan.
Katika mkutano wao na Rais iliamuliwa zipigwe kura za kuukubali ama kuukataa uongozi, zoezi ambalo lilifanyika Februari Mosi na kuhudhuriwa na Mawaziri pamoja na Wabunge.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Vijana na Michezo, Fatma Said Ally, Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Damian Lubuva, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Nyamka, Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-salaam, Wabunge na Wakuu wa Wilaya za mkoa wote wa Dar-es-Salaam, pamoja na viongozi wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) wote walihudhiria.
Baada ya hapo ilikubaliwa kwamba uchaguzi ufanyike baada ya mwenyekiti wa klabu hiyo Billy Bandawe, kushindwa kwa kura 635-94. Uchaguzi huo ulifanyika Jumapili ya Februari 8 kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, ambapo nafasi ya uenyekiti iliwaniwa na watu watatu; William Bocco, Ally Bakari na Mzee Kheri..
Waliowania nafasi ya makamu mwenyekiti ni Robert Mzeru na wenzake wawili, nafasi ya ukatibu mkuu iliwaniwa na Nicholaus Mathias na Joseph Mbele. Ukatibu mkuu msaidizi uliwaniwa na Salum Mohamed na Charles Mgombelo.
Nafasi ya mweka hazina iliwaniwa na Mohamed Rupembecho peke yake, wakati Juma Kambi na Mwilenza E. Mwilenza walikuwa wanagombea nafasi ya mweka hazina msaidizi. Peter Hassan na Charles Newa walikuwa wanawania nafasi ya katibu mipango wakati Salehe Omary na Ramadhani Karababa walikuwa wanachuana katika nafasi ya katibu mwenezi.
Hata hivyo, waliofanikiwa kuchukua nafasi ya uongozi wa klabu hio ni William Bocco (Mwenyekiti), Robert Mzeru (Makamu Mwenyekiti), Nicholus Mathias (Katibu Mkuu), Salum Mohammed (Katibu Mkuu Msaidizi), Mohammed Rupembecho (Mweka Hazina), Salehe Omari (Mweka Hazina Msaidizi) na Peter Hassan (Katibu Mipango).
Hata hivyo, licha ya mgogoro huyo, Yanga ilifanikiwa kunyakua ubingwa wa soka Tanzania Bara ambao ulikuwa umetwaliwa na Tukuyu Stars mwaka 1986. Yanga pia ikafanikiwa kutwaa na ubingwa wa Muungano mwaka huo.
Yanga ilitwaa ubingwa wa Bara kwa tofauti tu ya mabao dhidi ya Pamba ya Mwanza kwani timu zote baada ya mechi 18 zilikuwa na pointi 23 kila moja. Yanga ilikuwa na mabao 20 ya kufunga na kufungwa 20 wakati Pamba ilikuwa imefunga mabao 18 na kufungwa 9.
Msimu huo Simba ilishika nafasi ya nne kutoka mkiani ikiwa na pointi 17 katika mechi 18, wakati Reli na Nyota Nyekundu zilishuka daraja. Ikumbukwe kwamba, Reli Morogoro ilipanda daraja msimu huo na kushuka tena!
Tuliangalia zoezi la usajili kwa klabu za Daraja la Kwanza Tanzania Bara msimu huo lilikuwa limeanza tangu mwishoni mwa mwaka 1986 baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi. Klabu ya Yanga iliyokuwa imekumbwa na migogoro kama nilivyoeleza hapo awali ilipeleka orodha mbili za usajili FAT, moja ikiwa imepelekwa na uongozi na nyingine ilipelekwa na wanachama waliokuwa wakiupinga uongozi. Hata hivyo, FAT iliupitisha usajili uliofanywa na wanachama.
Timu mbili zilizokuwa zimepanda daraja msimu huo ni Reli Morogoro na RTC Kigoma ambazo zilichukua nafasi za RTC Kagera na Mwadui zilizoteremak daraja. Hebu tutazame jinsi baadhi ya timu hizo zilizofanya usajili wake.
Simba: Kikosi cha Simba mwaka huu kilikuwa kinafundishwa na Omar Mahadhi. Wachezaji waliokuwa wakiunda kikosi hicho ni John Bosco (Magereza Stars ya Moshi), Pazi Ally, Ayoub Mzee na Mohamed Nyauba (wote kutoka Nyota Nyekundu), Daniel Manembe, Saulo Jaji, Jamhuri Kihwelu na Kassim Matitu. Wachezaji wa zamani walikuwa Moses Mkandawire, Lilla Shomari, Twaha Hamidu, Ramadhani Lenny (naodha), Thobias Nkoma, Malota Soma, Mtemi Ramadhani, Omari Salehe, Amri Ibrahim, Willy Kiango, Sunday Juma, Mohammed 'Bob' Chopa, Zamoyoni Mogella, Ezekiel Greyson 'Juju Man', John Douglas, Twalibu Hilal, Adolf Kondo, Raphael Paul, Eric Sagala, Edward Chumila, Francis Mwikalo.
Yanga: Kikosi cha Yanga kilikuwa chini ya mchezaji wa zamani wa klabu hiyo Mwinda Ramadhani 'Maajabu' na kiliundwa wachezaji wafuatao; Juma Pondamali (Pan Africans), Athumani Juma 'Chama' na Celestine 'Sikinde' Mbunga (wote kutoka Maji Maji), Abubakar Salumu (Sigara), Athumani Abdallah China (Tumaini), Issa Athumani Mgaya (RTC Kagera), Said Mwaibambe 'Zimbwe' (Safari Contractors), Yusuph Ismail Bana (nahodha), Freddy Felix Minziro, Isihaka Hassan 'Chukwu', Rashid Idd Chama, Said Mrisho, Edgar Fongo, Hamisi Kinye, Joseph Fungo, Lawrence Mwalusako, Allan Shomari, Dotto Lutta Mokili, Mohammed Yahaya 'Tostao', Gregory Luanda, Charles Boniface Mkwasa, Muhidini Mohammed 'Cheupe', Hussein Idd, Juma Rashid Kampala, Lucius Mwanga, Ali Mchumila, Abeid Mziba 'Tekero', Makumbi Juma 'Homa ya Jiji', 'Field Marshal' Juma Mkambi.
Pamba: Baadhi ya wachezaji waliokuwepo katika kikosi hicho kilichokuwa chini ya kocha  Edmund Thomas msimu huu badala ya Abdulrahman Juma Ako ni Madata Lubigisa, Yusuph Abeid, Abdallah Burhani, Juma Mhina, Rashid Abdallah, Shabani Hamisi, Rajabu Risasi, Beya Simba, Issa Athumani, Mwaka Selemani, Mohamed  'Adolf' Rishard, Kitwana Selemani, John Makelele 'Zig Zag', Ali Bushiri, Yusuph Selemani, Khafan Ngassa, Ibrahim Magongo, Khalid Bitebo 'Zembwela', Venance Kazungu, Joram Mwakatika, Rwemaho Makama, Hamza Mponda, Athumani Juma Abdallah (Mutex-Musoma), David Mwakalebela (Mwadui) na wengineo.
Maji Maji: Ilikuwa na Isihaka Majaliwa, Stephen Nemes, Madaraka Kibode Selemani, John Kabisama, Hussen Kaitaba, Hamisi Fande, Ali Mdeve, Peter Tino, Octavian Mrope, Mohamed Mkandinga, Ahmed Kampira, Abdalah Chuma, Rajabu Mhoza, Athumani Maulid 'Big Man', Peter Mhina, Abdul Ntila, Samli Ayoub, Mdachi Kombo, Mhando Mdeve, Ahmed Abbas,  Venance Motto na wengineo.
Coastal Union: Ilikuwa na akina Idrissa Ngulungu, Hemed Morocco, Mohammed Kampira, Mchunga Bakari, Razak Yusuph 'Careca', Kassim Mwajeki, Abubakar Hassan, Yasin Abuu Napili, Abdallah Shamuni, Douglas Muhani, Salim Waziri, Selemani Jampani, Noordin Gogola, Elisha John, Abdallah Bori, Edward Hiza, Said George, Hussein Mwakuruzo, na wengineo.
RTC Kigoma: Ilikuwa imepanda daraja msimu huu na ilikuwa na akina Issa Hassan, Mavumbi Omar (RTC Kagera), Sanifu Lazaro 'Tingisha' (Balimi), Shabani Msafiri, Ramadhani Bilal, Cheche Kagire (Balimi), Hamza Mohammed Maneno, Wastara Baribari, Leopold Magesa na wengineo.
Nyota Nyekundu: Wachezaji waliokuwepo katika kikosi hiho walikuwa ni Roster David Ndunguru, Stephen Chibichi, John Manyama, Muhesa Kihwelu, Omar Mwimbage, Adam Rashid, Mbaraka Mohammed, Yasin Salehe, Said Seifu, Faustine Kibingwa, Hemed Kilindo, Hamisi Dilunga, Feruzi Udi, Raphael  'Roma' Mapunda na wengineo.
Tukuyu Stars: Ilikuwa inafundishwa na Athumani Juma na ilikuwa na akina Mbwana Makatta, Lumumba Richard 'Burruchaga', Kelvin Haule, Godwin Aswile, Peter Mwakibibi, Frank Mwasimanga, Justine Mtekere, Augustine Sanga, Michael Kidilu (RTC Mbeya), Selemani Mathew, Karabi Mrisho, Yusuph Kamba, Abdallah Shahibu, Hussein Zitto, Aston Pardon, Haji Shomari, Taisi Mwalyoba, Augustine Mumbe, John Alex, Daniel Chundu, Mohammed Salehe, na wengineo.                       
RTC Mwanza: Ilikuwa inaundwa na Kichochi Lemba (RTC Kagera), Philemon 'fumo' Ferdinand Felician (Toto Africans), Ali Majeshi, Nobby Eliuta, Manferd George, Ramadhani Mrisho, Vedastus Limbu, Hassan Ramadhani, Donald Haggai, Daniel Muhoja, Ally Mikidadi Kasanda, Augustine Haule, Benard Mlagala, Emanuel Chitete, Juma Jani, Idd lmas, Dioniz John na wengineo.
Reli Morogoro: Nayo ilikuwa ngeni katika ligi hii msimu huu baadhi ya wachezaji waliounda kikosi hicho ni Sahau Said Kambi, Denis Saigulan, Madundo Mtambo (SUA), Abdul Bakari, Sospeter Malekele, Adam Selemani, Boniface Njohole, Julius Semkiwa, Thabiti Mgalula, Magnus Mzumi, Livingstone Sanke, Venance Mwakalukwa, Bakari Tutu na wengineo.

Comments