Featured Post

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI KUWA MGENI RASMI MKUTANO WA JUMUIYA YA WAISLAMU WA AHMADIYYA

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Dar es Salaam
WAZIRI wa Mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 47 wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya utakaofanyika kuanzia Septemba 30 hadi   Octoba 2 mwaka huu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jumuiya hiyo Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry, Katibu Mkuu Msaidizi Abdurahman Ame alisema kuwa mkutano huo utafanyika eneo la kitonga, kata ya Msongola Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Alisema Jumuiya imeandaa mkutano huo kwa lengo la kuhamasisha amani katika jamii na kuwakumbusha waumini hasa wa kiislamu juu ya misingi sahihi ya dini ya kiislamu pamoja na kumjua na kutimiza haki ya Mwenyezi Mungu.

“Wajibu wa kiongozi wa dini ni kuandaa na kuhamasisha masuala ya dini, hivyo lengo la mkutano huo ni kuhamasisha amani katika jamii na pia kuwakumbusha waumini wa kiislamu juu ya kumjua, kuishi na kutimiza haki ya Mwenyezi Mungu hali itakayosaidia kuondokana na vitendo viovu,” alifafanua Katibu huyo.

Mbali na hayo, mkutano huo utabebwa na kaulimbiu isemayo “kuitambua amani ya jirani yako, huvunjilia mbali kuta zinazowatenganisha” ikiwa na ujumbe ya kwamba kuna haja ya kuelimisha jamii uzuri wa mafundisho ya dini kwa kutumia vitabu vitakatifu kupitia vyombo mbalimbali vya masasiliano.

Vile vile, Washiriki mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi zikiwemo Kenya, Uganda, Burundi, Malawi, Msumbiji na Uingereza wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za kidini na za kijamii watashiriki katika mkutano huo. 

Ahmadiyya ni jumuiya ya waislamu ya kimataifa iliyoenea katika nchi 209 duniani kwa lengo la kuleta uhuisho wa dini ya kiislamu kwa kutangaza kwa amani ujumbe sahihi wa Islam duniani kote.

Comments