- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Kikosi cha Mseto FC kilichotwaa ubingwa mwaka 1975. Charles Mkwasa ni wa tano kutoka kulia waliosimama.
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
MWAKA 1974 Yanga
iliifunga Simba mabao 2-1 katika mchezo wa fainali kwenye Uwanja wa Nyamagana,
Mwanza, ukiwa ndio mchezo wao wa pili katika historia yao kufanyika nje ya Dar
es Salaam baada ya ule wa kirafiki uliofanyika mwaka 1959 mjini Dodoma na Simba
(wakati huo ikiitwa Sunderland) ikafungwa mabao 3-1 mbele ya Malimu Julius
Kambarage Nyerere, Mwenyekiti wa Chama cha TANU kilichokuwa kikipigania uhuru
wa Tanganyika wakati huo.
Michuano ya Ligi
ya Taifa mwaka 1975 ilishuhudia Simba wakishindwa kuingia hatua ya fainali, kwa
sababu wakati huo ilibidi timu zote zianzie ngazi za chini kabisa, yaani Ligi
ya Wilaya na Mkoa.
Simba, chini
ya kocha wake Nabi Camara kutoka Guinea, ilikuwa na wachezaji wengi wa mwaka
uliopita akina John Semainda, Daudi Salum 'Bruce Lee', Omari Mahadhi, Mohmmed
Kajole, Filbert Rubibira, Mohammed Bakari 'Tall', Jumanne Hassan ‘Masimenti’ (kutoka
Yanga), Abbas Said Kuka, George Kulagwa, Nico Njohole, Adamu Sabu, Aballah
Mwinyimkuu, Abdallah Hussein ‘Kibadeni’, Abbas Dilunga, Martin Kikwa, Hussein
Tindwa, Thuwein Ally ‘Watakiona’, Isihaka Kibene, Yusuf Kaungu, Kihwelu Musa,
Mohammed Kajole ‘Machela’, Willy Mwaijibe, Aloo Mwitu, Shaaban Baraza, Omari
Gumbo, Lucas Nkondola, Khalid Abeid, Omari Chogo 'Chemba', Haidari Abeid
'Muchacho', Juma Abeid Mzee ‘360 Degree’, na Emmanuel Albert Mbele ‘Dubwi’.
Yanga nayo,
ikiwa inaendelea kunolewa na Tambwe Leya kutoka Zaire, ilikuwa imewasajili tena
Elias Michael ‘Spring’, Muhidin Fadhil, Patrick Nyaga, Leodegar Tenga, Omari
Kapera ‘Mwamba’, Boi Iddi 'Wickens', Juma Shaban, Jella Mtagwa, Juma Matokeo,
Sunday Manara ‘Computer’, Kitwana Manara ‘Popat’, Gibson Sembuli, Muhaji Mukhi,
Ally Yusuf, Ali Selemani, Leonard Chitete, Kaburu, Bona Max Mwangu, Ahmed
Omari, Hassan Gobbos ‘Wa Morocco’, Athumani Kilambo, Adam Juma, Gilbert
Mahinya, Abdulrahman Juma (nahodha), Mohammed Rishard ‘Adolf’, Moshi Hussein
'Dayan', Selemani Said Sanga ‘Totmund Wanzuka’, Adam Juma, na Maulid Dilunga ‘Mzee
wa Mexico’.
Timu ya
Nyota kutoka Mtwara mwaka huo ilikuwa imara sana na ilikuwa na wachezaji kama
Zimbo, Dogoa, Okello, Mohammed Mkandinga, Chohan, Bomba, Kibonge, Namajojo,
Joseph, Bhulji, Kwasa, Mchuru, na wengineo, wakati Mseto ya Morogoro iliyokuwa
inafundishwa na mchezaji wa zamani wa Yanga, Mohemmed Hussein Hassan 'Msomali'
ilikuwa na wachezaji kama Said Ramadhan, Ahmad Rajab, Ahmad Maggid, Miraji
Salum, Ramadhan Matola, Athumani Matola, Vincent Mkude, Jaafar Mohammed
'Spencer', Hassan Shilingi, Hussein Ngulungu, Mohammed Manyanga, Omar Hussein,
Aluu Ali, Shiwa Lyambiko, na Charles Boniface Mkwasa.
Timu
nyingine zilizoshiriki michuano ya mwaka huo zilikuwa ni Miembeni ya Zanzibar,
Nyuki ya Kigoma, Pamba ya Mwanza, Kisarawe ya Pwani, Jumuiya ya Arusha, Mwadui
ya Shinyanga, TPC ya Kilimanjaro, Maji Dodoma, Balimi ya Bukoba, Usalama Dar es
Salaam, Jeshi Zanzibar, Vita Tabora, Kilimali ya Singida, Mazao Iringa, Nchi
Yetu Lindi, Elimu Ruvuma, Kilimo Mara, Coastal Stars ya Pwani, Comworks
(Ujenzi) Rukwa, na Comworks (Ufundi) Mbeya ambayo ndiyo Tanzania Prisons ya
sasa.
Kwa
ukiangalia utaona kwamba karibu nyingi kati ya timu hizi zilikuwa za kazini.
Mashindano
ya mwaka 1975 yalikuwa ya mtoano na yalifanyika mjini Dar es Salaam. Mashabiki
wa soka walikuwa na wasiwasi kwamba ligi ya mwaka huo isingekuwa na msisimko
kwa kuwa Yanga na Simba zisingeweza kukutana. Hata hivyo, wasiwasi wao ulitoka
baada ya kuibuka timu kutoka mikoani ambazo zilikuwa zinacheza soka la uhakika.
Hizi zilikuwa Mseto ya Morogoro na Nyota ya Mtwara ambazo ndizo zilizofuzu kwa
fainali.
Timu nyingi,
hata zile ngeni, mwaka huo zilionyesha upinzani wa nguvu sana hadi kulazimisha
mshindi apatikane kwa njia ya penati baada ya dakika 90 za mchezo kushindwa
kutoa mshindi. Kama ingekuwa ligi, ambapo mshindi alipata pointi mbili na
pointi moja kwa kila timu zilizotoka sare, ingekuwa afadhali, lakini kwa kuwa
ilikuwa ni mtoano, penati hazikuwa na budi kutumika. Mtindo wa ligi kamili
ulikuja baadaye kabisa.
Msisimko
mwingine ulikuja baada ya michezo kadhaa kurudiwa baada ya malalamiko.
Kwa ujumla
timu za nje ya Dar es Salaam zilileta ushindani wa kutosha. Ingawa mkoa wa Dar
es Salaam ulikuwa na timu mbili - mabingwa watetezi Yanga na Usalama (Polisi
waliokuwa mabingwa wa Mkoa) timu hizo zilifungwa na hazikuweza kufika fainali.
Yanga
ilifungwa na Mwadui ya Shinyanga kwa penati 3-2 baada ya kutoka suluhu wakati
Usalama ilifungwa mabao 5-3 na Mseto ya Morogoro, timu ambayo ilionyesha
maajabu makubwa mwaka huo.
Hadi kufika
fainali, kwanza Mseto ililaza Jumuiya Arusha kwa mabao 3-2 katika mchezo
uliofanyika Julai 18, 1975 na kuchezeshwa na Gration Matovu ambapo wafungaji wa
Mseto walikuwa Omar Hussein (penati dakika ya 10) na Aluu Ali dakika za 35 na
48, wakati mabao ya Jumuiya yalifungwa na Marandu Mkubwa dakika ya 47 na Makula
dakika ya 75.
Vikosi vyao
siku hiyo vilikuwa: Mseto: Said
Hashim, Hamdani, Vincent Mkude, Miraji, Matola, Charles Boniface Mkwasa, Shiwa
Lyambiko/Mohammed Manyanga, Shilingi, Omar, Aluu Ali, Jaafar Mohammed ‘Spencer’.
Jumuiya: Tito, Darabu, Makula, Kiluwa/Mkamba, Nyanda,
Okwirini, Bukuku, Marand Mkubwa, Mhina/Owino, Focus, na Martin/Joseph.
Katika mechi
yao ya pili Julai 23, 1975, Mseto waliitandika Kilimo Mara mabao 2-1 huku mabao
ya washindi yakifungwa na Aluu Ali dakika ya 58 na Shiwa Lyambiko dakika ya 70
wakati Mwambeni aliifungia Kilimo bao la kuongoza dakika ya 5.
Kwenye mchezo
wa nusu fainali Julai 26, 1975, Mseto iliitoa Usalama Dar kwa penati 5-3.
Kwa upande
mwingine, Nyota Mtwara ilianza kwa kuichakaza Mazao Iringa kwa mabao 6-1 katika
mechi iliyofanyika Julai 21, 1975. Mabao ya Nyota yalifungwa na Said Dogoa
(penati dakika ya 15), Joseph alifunga matatu dakika za 25, 40, na 62, Namajojo
akafunga dakika ya 35, na Mahmoud wa Mazao alijifunga dakika ya 75 katika
jitihada za kuokoa. Bao pekee la Mazao lilifungwa mapema katika dakika ya 6 na
Kessy Kibuda.
Mchezo wao
wa pili uliwakutanisha na jirani zao, Nchi Yetu Lindi (zamani ikijulikana Young
Africans Lindi), ambapo Nyota walishinda kwa mabao 5-0 hapo Julai 26, 1975.
Katika nusu
fainali walikumbana na Balimi ya Bukoba ambapo waliishindilia mabao 4-0 hapo
Julai 29, 1975.
Baada ya
michezo ya nusu fainali, Nyota Mtwara na Mseto ndizo zilizofuzu kwa fainali,
ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya ligi hiyo kwa mchezo wa fainali
kuzikutanisha timu kutoka nje ya Dar es Salaam.
Pambano hilo
lilichezwa Jumamosi Agosti 2, 1975 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Umati
wa maelfu ya watazamaji waliohudhuria pambano hilo walishuhudia timu hizo ngeni
katika fainali zilivyoonyesha kandanda la kusisimua na kuondoa dhana kwamba
ligi hiyo ni ya Yanga na Simba tu.
Vijana wa
Morogoro, ambako ndiko liliko chimbuko la vijana wengi wacheza soka kwa miaka
mingi, walionyesha wazi kwamba wanaweza kulisukuma gozi baada ya kupata ushindi
mnono wa mabao 3-1.
Bao la
kwanza lilipatikana katika dakika ya saba ya mchezo mfungaji akiwa Hassan Shilingi
baada ya kuunganisha krosi ya Shiwa Lyambiko. Nyota Afrika hawakukata tamaa na
juhudi zao zilizaa matunda baada ya kusawazisha kwa njia ya penati katika
dakika ya 18. Omari Hussein, ambaye baadaye alikuja kpachikwa jina la utani la
'Keegan', aliwainua wapenzi wa Mseto baada ya kupachika bao la pili katika
dakika ya 30 na hadi timu hizo zinakwenda kupumzika matokeo yalikuwa 2-1.
Mseto
walikianza kipindi cha pili kwa kasi ya kulinda lango lao na kutafuta mabao
mengine na katika dakika za majeruhi walifanikiwa kupachika bao la tatu
lililofungwa na Shiwa Lyambiko kwa mkwaju wa mbali, kama mita thelathini hivi.
Shiwa alikuwa anasifika sana kwa kuwa na mashuti makali. Hadi kipenga cha
mwisho kinapulizwa Mseto walikuwa 3 na Nyota Mtwara 1.
Wachezaji
walioziwakilisha timu hizo katika mchezo huo wa fainali walikuwa: Mseto: Said Ramadhan, Hamdan, Charles
Boniface Mkwasa, Vincent Mkude, Ramadhan Matola, Alluu Ali, Shiwa Lyambiko,
Hassan Shilingi, Omari Hussein, Mohammed Manyanga, Jaafar Mohammed 'Spencer',
na Jumanne Hassan Masimenti.
Nyota Mtwara: Zimbo, Said Dogoa, Okello, Mohammed
Mkandinga, Chohan, Bomba, Kibonge, Namajojo, Joseph, Bhulji, na Kwasa/Mchuru.
Taarifa hizi
zimenyofolewa katika mswada wa kitabu cha UBINGWA WA SOKA TANZANIA cha
mwandishi mkongwe wa michezo nchini Tanzania, Daniel Mbega. Kitabu hicho kipo
katika hatua za mwishoni kuingia mitamboni.
Comments
Jumanne Masimenti hakutoka Yanga huyu alitoka Cosmopolitan kwenda Simba
ReplyDeleteJumanne Masementi alitokea Cosmopolitan kwenda Simba hakutokea Yanga
ReplyDelete