- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Kikosi cha Tukuyu Stars kilichotwaa ubingwa mwaka 1986
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
UKIANGALIA orodha ya klabu bingwa za soka Tanzania
Bara katu huwezi kukosa kuliona jina la Tukuyu Stars ya Mbeya, ambayo kwa
hakika iliushangaza ulimwengu mwaka 1986 wakati ilipounyakua ubingwa huo kutoka
kusikojulikana na kuziacha timu kongwe za Simba, Yanga, Pamba na Coastal Union
zikiwa hazina la kufanya. Timu nyingine zilizoshiriki ligi msimu huo zilikuwa
RTC Kagera (sasa Kagera Sugar), Mwadui ya Shinyanga, Majimaji ya Songea, RTC
Mwanza na Nyota Nyekundu ya Dar.
MaendeleoVijijini inajua kwamba, siyo tu kunyakua ubingwa ndiko kulikowashangaza
wengi, lakini pia Tukuyu Stars mwaka huo ilitoa vipigo vikali kwa timu hizo na
kuthibitisha kwamba, kumbe ukubwa wa pua siyo wingi wa kamasi! Yaani ukongwe wa
timu siyo silaha ya kushinda, bali mchezo wa soka ni dakika tisini uwanjani.
Timu hii, mbali ya kuweka historia ya pekee kwa
kupanda daraja la tatu, kisha la pili hadi kuwa bingwa, pia katika uhai wake
imeweza kutoa wanasoka wengi, ama wengine waliibukia hapo au wengine walitokea
sehemu nyingine na kufanya maajabu.
Kumbukumbu za usajili, ambazo MaendeleoVijijini inazo, zinaonyesha kwamba, baadhi ya wachezaji waliopata kuichezea timu hiyo
tangu ilipopanda daraja mwaka 1986 ni Mbwana Makata, Chachala Muya, Sekilojoa
Chambua, Robert Damian, Muhesa Kihwelu, Ikupilika Nkoba, Gamshard Gamdast,
Betwell Africa, Jebby Mohammed, Asanga Aswile, Vincent Buriani, Yussuf Kamba,
Costa Magoloso, Jimmy Mored, Salum Kussi, Stephen Mussa, Lumumba Richard
‘Burruchaga’, Kelvin Haule, Godwin Aswile, Peter Mwakipa, Selemani Mathew
Luwongo, Caraby Mrisho, Abdallah Shaibu, Peter Mwakibibi, Taisi Mwalyoba,
Augustine Mumbe, John Alex, Daniel Chundu, na wengineo wengi.
Tukuyu Stars, ambayo ilimaliza Ligi Daraja la
Kwanza Tanzania Bara msimu huo iliyokuwa na timu 10 ikiwa na jumla ya pointi
23, ikifuatiwa na Majimaji pointi 22, Simba pointi 21, na Pamba pointi 20,
iliweka rekodi kubwa kabisa kwenye ligi ambayo ilikuja kufikiwa miaka 13
baadaye, kwa kuwa klabu ya kwanza ya vijijini kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.
Kumbukumbu za MaendeleoVijijini zinaonyesha kuwa, katika historia ya ubingwa wa soka nchini Tanzania, hakuna timu ya wilayani, inayotoka nje ya Makao Makuu ya Mkoa, iliyowahi kuvishwa taji la ufalme wa soka kabla ya Tukuyu, hadi Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro ilipokuja kuifikia rekodi hiyo mnwaka 1999 na kuweka rekodi nyingine kwa kuutwaa kwa mara ya pili mfululizo mwaka 2000.
Kumbukumbu za MaendeleoVijijini zinaonyesha kuwa, katika historia ya ubingwa wa soka nchini Tanzania, hakuna timu ya wilayani, inayotoka nje ya Makao Makuu ya Mkoa, iliyowahi kuvishwa taji la ufalme wa soka kabla ya Tukuyu, hadi Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro ilipokuja kuifikia rekodi hiyo mnwaka 1999 na kuweka rekodi nyingine kwa kuutwaa kwa mara ya pili mfululizo mwaka 2000.
Wachezaji waliosaidia kupeleka ubingwa wilayani
Rungwe walikuwa nahodha Ikupilika Nkoba, kipa Mbwana Makata, Justine Mtekere,
Salum Kabunda ‘Ninja’, Lumumba Richard ‘Burruchaga’, Suleiman Mathew Luwongo,
Caraby Mrisho, Abdallah Shaibu, Danford Ngessy, Yussuf Kamba, Aston Pardon,
Ghamshard Gamdast, Betwell Africa, Jebby Mohammed, Asanga Aswile, Vincent
Buriani, Costa Magoloso, Jimmy Mored, Salum Kussi, Stephen Mussa, Kelvin Haule,
Godwin Aswile, Peter Mwakipa, Hussein Zitto, Haji Shomari, Taisi Mwalyoba, Augustine
Mumbe, John Alex, na Daniel Chundu.
Mtindo wa Ligi ya Muungano ambao Bara na Visiwani
kwanza walikuwa wanatafuta mabingwa wao kabla ya kutafuta klabu bingwa ya
Tanzania, mpaka kufikia mwaka 1986 ulikuwa umefikisha miaka mitano na chini ya
mtindo huo, Tukuyu Stars pia ikawa timu ya kwanza kuwa bingwa wa Tanzania Bara
kutoka nje ya Dar es Salaam.
Kabla ya mwaka 1982, ingawa Tanzania Visiwani
ilikuwa na mabingwa wake kila msimu, lakini Tanzania Bara haikuwa inapata
bingwa tofauti, isipokuwa yule yule bingwa wa Tanzania aliyekuwa anapatikana
hatua ya mwisho ya ligi iliyozishirikisha timu za Zanzibar, ndiye aliyekuwa
anavaa kofia ya Taifa na Bara, hasa katika kugombea Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati.
Mwaka 1982 mtindo huo ulipokuwa umeanza, Pan African
ilitwaa ubingwa, mwaka 1983 Yanga, mwaka 1984 Simba na mwaka 1985 Yanga tena.
Kwa hali hiyo, ubingwa wa Tanzania Bara ulikuwa ni wa Dar es Salaam kabla
Tukuyu Stars haijauvunja utawala wa timu za Dar es Salaam.
Tukuyu Stars pia iliweka rekodi ya kuwa timu ya
kwanza nchini kupanda daraja na kutwaa ubingwa msimu huo huo. Timu hii pia
ilikuwa na bahati kubwa, kwani haikustahili kushiriki michuano ya hatua ya
mwisho ya Ligi Daraja la Pili mwaka 1985 ambayo ndiyo iliyopandia daraja na
kwenda la Kwanza.
Katika makundi ya fainali ya Ligi Daraja la Pili
mwaka 1985, Tukuyu Stars ilikuwa kundi la Tabora na makundi mengine yalikuwa
Moshi na Songea. Matokeo ya kundi la Moshi yalifutwa na FAT baada ya timu
kupanga matokeo kwa kufungana mabao 6-6, hivyo timu zilizokuwa za tatu katika
makundi mengine zilipewa nafasi ya kushiriki katika ligi ya timu sita.
Pamoja na hivyo, katika kundi la Tabora, Kiltex ya
Arusha ndiyo ilikuwa ya tatu na Tukuyu Stars ilikuwa ya nne na ya mwisho.
Lakini timu hiyo ilikuwa imewahi kuomba FAT pamoja na RTC Mwanza, ambayo
ilikuwa imeshika nafasi ya tatu katika kituo cha Songea, kwamba zipewe nafasi
kabla nyingine hazijaomba.
Malalamiko ya viongozi wa FAT Mkoa wa Arusha
kwenye Mkutano Mkuu wa FAT Taifa mjini Tabora mnamo Desemba 1985, hayakuweza
kutengua kuingia kwa Tukuyu Stars kwenye Ligi Daraja la Kwanza. Tukuyu Stars
ikawa imejitahidi kupanda kwa kutumia mwanya huo wa uzembe wa FAT.
Tukuyu Stars inatoka wilaya ya Rungwe (Tukuyu) na
ina nyumba yake ya makao makuu mjini Tukuyu, kandokando ya barabara iendayo
Kyela kutoka Mbeya. Timu hiyo mwaka huo ilikuwa inafundishwa na Athumani JUma,
beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, ambaye pia wakati huo alikuwa
akiifundisha timu ya mkoa wa MBeya, Mapinduzi Stars, kwa ajili ya michuano ya
Kombe la Taifa.
Klabu hii, ambayo ilipata bahati kama ile ya klabu
ya Levintis United ya Nigeria (ambayo ilitokea daraja la tatu hadi kuwa bingwa
wa taifa), ilikuwa chini ya usimamizi wa mfanyabiashra mmoja wa Kihindi mjini
Tukuyu, Ramnik Patel ‘Kaka’.
MaendeleoVijijini inazo kumbukumbu halisi kuhusu timu hiyo, ambayo ilianzishwa mapema katika miaka ya 1980
ikiwa inajulikana kwa jina la Limbe, kwa kuiga jina la Limbe Leaf Wanderers ya
Malawi. Wakati huo Ramnik Patel alikuwa akifanya biashara zake huko Kyela
kwenye mpaka wa Kasumulu, unaozitenganisha Tanzania na Malawi.
Ilipobadili jina na kuitwa Tukuyu Stars timu hiyo
ikapanda daraja la tatu mwaka 1981, na ilipotwaa ubingwa wa Mkoa wa Mbeya na
kuingia Ligi Daraja la Pili ngazi ya taifa, ndipo ilipookota dhahabu mpaka
ilipokuwa imefikia mwaka 1986.
Lakini tangu timu hii ishuke daraja mwaka 2002,
hakuna dalili zozote zilizoonyeshwa kwamba kulikuwa na mikakati ya makusudi ya
kuinyanyua timu hii ili ipande daraja tena.
Comments
Post a Comment