Featured Post

STARTIMES KUWAPAMBANISHA 18 FAINALI ZA SHINDANO LA VIPAJI VYA SAUTI KESHO JIJINI DAR ES SALAAM


Mtengenezaji wa Sauti katika chaneli ya StarTimes Kiswahili, Tracy Luo (katikatio) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutangaza kufanyika kwa fainali za shindano la vipaji vya sauti litakalofanyika kesho katika ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kushoto ni mshiriki wa shindano hilo kutoka Zanzibar,  Safiya Ahmed na kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Masoko wa kampuni hiyo, Damien Li. Washiriki 18 kati ya 547 wameingia hatua ya fainali ambapo washindi 10 watajipatia fursa ya kwenda kufanya kazi makao makuu ya StarTimes yaliyopo Beijing, China.

 Mshiriki Safiya Ahmed kutoka Zanzibar (kushoto), akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Mtengenezaji wa Sauti katika chaneli ya StarTimes Kiswahili, Tracy Luo.
Mshiriki Hilda Malecela kutoka Dar es Salaam (kulia), akizungumza na wanahabari katika mkutano huo.
Mshiriki kutoka mkoani Arusha, Mathew Mgeni (kushoto), akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni mshiriki Hilda Malecela kutoka Dar es Salaam.
Taswira meza kuu kwenye mkutano huo.
Washiriki wa shindano hilo. Kutoka kulia ni Safiya  Ahmed kutoka Zanzibar, Mathew Mgeni kutoka Arusha na Hilda Malecela kutoka Dar es Salaam
Washiriki wa shindano hilo wakiwa kwenye mkutano huo.

Na Dotto Mwaibale

WASHIRIKI 18 waliotinga fainali ya shindano la kusaka vipaji vya sauti linaloendeshwa na kampuni ya StarTimes watapanda jukwaani kesho katika ukumbi wa Nkrumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupigania nafasi kumi za kwenda kufanya kazi jijini Beijing, China.

Washiriki hao ambao walipatikana kwenye usaili uliofanyika katika mikoa ya Arusha (washiriki watano), Zanzibar (washiriki watano) na Dar es Salaam (washiriki nane) watakuwa na kibarua kigumu cha kuwavutia majaji wabobezi katika tasnia ya sanaa za maonyesho ili waweze kuchaguliwa na kula mkataba mnono wa kufanya kazi katika makao makuu ya kampuni hiyo ya matangazo ya dijitali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi Mtengenezaji wa Sauti katika chaneli ya StarTimes Kiswahili,  Tracy Luo amesema mchakato wa kuwapata washiriki hao waliotinga hatua ya fainali lilikuwa ni gumu sana kwani watanzania takribani 547 walijitokeza na wengi wameonyesha vipaji vya hali ya juu.

“Shindano la kusaka vipaji vya sauti ni la kwanza na aina yake kuwahi kutokea nchini ambalo limewapa fursa watanzania wenye vipaji kujitokeza na kuzitumia katika kuwaingizia kipato. Lakini mwaka 2014 ndiyo yalianza rasmi ambapo matunda yake ni watazamaji waliweza kufurahia vipindi vizuri zaidi. Katika miaka mitatu iliyopita imeonyesha kuwa filamu na tamthiliya zilizoingizwa kwa lugha mbalimbali za kiafrika zilipendwa zaidi. Na hali hiyo imeifanya kampuni ya StarTimes kusaka vipaji vya watu kuingiza sauti ili ziweze kutumika zaidi.” Alisema Luo

“StarTimes kwa kushirikiana na ubalozi wa China hususani idara ya kukuza utamaduni imeamua kuja na mashindano haya baada ya kuona kuna ombwe katika nafasi ya watu wa kuingiza sauti kwenye filamu na tamthiliya za Kichina kwenda lugha ya Kiswahili. 

Tumegundua kuwa watanzania ni wapenzi wakubwa wa tamthiliya na filamu za Kichina zilizoingiziwa sauti za Kiswahili na kupitia washindi watakaopatikana kesho tunaamini kazi nyingi zaidi zitafsiriwa na kuweza kueleweka miongoni mwa watazamaji wengi. Wateja wetu wamekuwa wakifurahia kazi hizo kupitia chaneli za TBC1 pamoja na chaneli mahususi kwa vipindi na madhui ya kwa lugha ya Kiswahili ya StarTimes Kiswahili kama vile Ma Zu, Kutafuta Mapenzi, Ndoa za Familia ya Mi na kadhalika.” alisema Luo 

Mtengenezaji huyo wa sauti wa chaneli ya StarTimes Kiswahili alihitimisha kwa kusema kuwa, “Watanzania inabidi waamke na kuchangamkia fursa zilizokuja pamoja na kuingia kwa matangazo ya dijitali hususani katika kukuza kazi za sanaa. Kwa mfano hivi sasa kuna uhitaji mkubwa wa maudhui ili kuweza kurushwa kwenye chaneli na vipindi vyetu, endapo watu watautumia ubunifu walionao hii itakuwa ni ajira kubwa kwao. 

Ninaamini kuwa kupitia teknolojia hii mpya wasanii wanaweza kujulikana zaidi sehemu kubwa ndani ya nchi kwa muda mfupi, kwa mfano StarTimes inapatikana katika nchi takribani 16 barani Afrika na zaidi ya mikoa 17 nchini huku baadhi ya chaneli zetu zikionekana zaidi ya nchi moja kama vile chaneli ya StarTimes Kiswahili inayoonekana nchini Tanzania na Kenya.”

Kwa upande wake mshiriki katika fainali za masindano hayo kutoka Arusha Mahew Mgeni amesema kuwa, “Najisikia mwenye furaha kuwa mmojawapo wa washiriki waliofikia hatua ya fainali kwani hapo awali nilikuwa ni shabiki na mtazamaji wa filamu na tamthiliya za Kichina lakini leo hii ninaweza kuwa naingiza sauti kwenye kazi zijazo siku za usoni. Naipongeza sana kampuni ya StarTimes Tanzania kwa kuja na shindano hili la aina yake ambalo halijawahi kutokea na kusisitiza makampuni mengine kwenye tasnia ya matangazo ya dijitali kufanya hivyo.”

Mshiriki mwingine kutoka visiwani Zanzibar, Safiya Ahmed yeye alielezea matarajio yake endapo atakuwa mmojawapo wa washindi.

“Kwanza, nimefurahi sana kuwepo kwa mashindano haya nchini ambapo wasanii kama sisi wenye vipaji vya kuingiza sauti tunaweza kuonekana na kutambulika. Mimi ninaamini kama mashindano haya yakiendelea basi watu wengi zaidi wataendelea kujitokeza na hivyo kupelekea kazi nyingi zaidi kutengenezwa. Natumaini nitatenda haki kwa hadhira inayotarajia kazi nzui kutoka kwangu endapo nitachaguliwa na kuwa mshindi.” alisema Ahmed

Akizungumzia umuhimu wa mashindano hayo katika kupanua fursa zingine za sanaa nchini Tanzania, mshiriki kutoka Dar es Salaam, Halima Malecela amesema kuwa, “Sanaa ina wigo mpana sana kwani kuna wale ambao wanaopenda kuonekana mbele ya kamera kama vile waigizaji wa filamu na tamthiliya mbalimbali, lakini kuna wengine kama sisi ambao tunapenda kuwa nyuma ya kamera na badala yake tukawasilisha sanaa yetu kupitia sauti. Ni vema sasa wasanii wakaliona hili na kuijitanua zaidi kwa upande wa kazi za sanaa.”

Washiriki waliopatikana na kufanikiwa kuingia hatua ya fainali kwa mkoa wa Arusha ni Mathew Philip Mgeni, Dorcas Francis, Halima Hussein, Janeth N Molely na Hilda Kinabo; Zanzibar ni Safiya Ahmed Said, SaiqKuiuiwa Abdalahh, Rukia Hamdan, Imaiu Obeid Fabian na Mohamed Said Mohamed; na Dar es Salaam ni Hilda Malecela, Abraham Richard, Happines Sianslaus ‘Nyamayao’, Richard Rusasa, Emanuel Landey, Coletha Raymond, Jamila na Maisala Abdul;

Comments