Featured Post

MWANAMUZIKI MAYAULA MAYONI: NYOTA WA YANGA ALIYEITANDIKA SIMBA MABAO 2-1



 Mayaula Mayoni (wa tatu kutoka kushoto) akiwa na kikosi cha Vita Club

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog

Kuzaliwa: Novemba 6, 1946
Mahali: Leopoldville (Kinshasa), Congo
Kufariki: Mei 26, 2010
Mahali: Brussels, Ubelgiji
Klabu alizochezea: AS Vita Club (Congo DR), Young Africans (Tanzania), Racing Club de Charleroi (Ubelgiji), Racing Club de Jette (Ubelgiji), FC Fribourg (Uswisi), Timu ya Taifa ya Zaire.
Bendi alizopigia: Kundi la Abeti Masikini, T.P. O.K. Jazz na Soukous Stars.
Nyimbo alizotunga: Cherie Bondowe I & II, Nabali Mizele, Ousmane Bakayoko, Moni, Ndaya (uliimbwa na M’pongo Love), Nasi Nabali (uliimbwa na Tshala Muana), L’Amour au kilo, Mbongo ebima.


Freddie Mayaula Mayoni (alizaliwa Novemba 6, 1946 jijini Léopoldville - ambalo sasa linaitwa Kinshasa, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) alikuwa mchezaji wa soka na mwanamuziki ambaye tungo zake nyingi bado zingali moto hata sasa zinapopigwa.

Maisha yake ya awali
Mayaula Mayoni alimaliza shule za awali bila matatizo na kuhitimu aliza elimu ya sekondari mwaka 1962 katika Chuo cha Kisantu. Tangu akiwa mdogo alipenda sana kandanda. Kati ya mwaka 1968 na 1970 alicheza nafasi ya winga wa kushoto katika timu ya AS Vita Club ya Kinshasa na aliweza kuchaguliwa hata timu ya Taifa ya Congo ‘Les Leopards’.
Baba yake alipopata nafasi ya kufanya kazi katika Ubalozi wa Zaire nchini Tanzania, Mayaula alimfuata huku na kujiunga na timu ya Young Africans mwaka huo huo ambapo alikuwa kwenye kikosi kilichotwaa ubingwa kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Wachezaji wengine waliokuwa katika kikosi hicho kilichokuwa kinanolewa na Dk. Victor Sanculescu kutoka Romania walikuwa Elias Michael, Kitenge Baraka Said, Boi Idd ‘Wickens’, Hassan Gobbos ‘Wa Morocco’, ‘Mwamba’ Omari Kapera, Gilbert Mahinya, Kitwana Manara, Maulid Dilunga, Juma Bomba, Badi Salehe, Leonard Chitete, Abdulrahiman Juma (nahodha), Freddie Mayaula Mayoni (Zaire) na wengineo.
Itakumbukwa kwamba, Jumamosi Juni 30, 1970 katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Karume (kombe hilo lilitolewa na Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karume), dhidi ya mahasimu wa Yanga, Sunderland (kabla haijaanza kuitwa Simba SC), kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) jijini Dar es Salaam, Mayaula Mayoni alifunga mabao mawili yaliyoipata Yanga ushindi wa 2-1.
Mchezo huo ulishuhudiwa na Rais Karume mwenyewe ambapo Mayaula alifunga mabao yote mawili ndani ya dakika 45 za kwanza, huku lile la Sunderland lilifungwa na Omar Gumbo katika dakika ya 19. Sunderland sasa ilikuwa inasubiri kulipa kisasi kwenye Ligi ya Mkoa wa Pwani.
Yanga ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Mayaula mayoni katika dakika ya 32 baada ya kumegewa krosi safi na Maulid Dilunga kabla ya kufumua shuti kali ambalo kipa wa Sunderland, Hassan Mlapakolo, alishindwa kulidaka. Dakika nne baadaye Mayaula tena akaifungia Yanga bao la pili na la ushindi baada ya kutokea piga-nikupige langoni mwa Sunderland.
Siku hiyo timu zilipangwa hivi: Yanga: Elias Michael, Athumani Kilambo, Boi Idd ‘Wickens’, Hassan Gobbos, Omari Kapera, Badi Salehe, Leonard Chitete, Abdulrahiman Juma (nahodha), Kitwana Manara, Maulid Dilunga, Freddie Mayaula Mayoni.
Sunderland: Hassan Mlapakolo, Shaaban Baraza, Mohammed Kajole, Yussuf Salum, Rashid Seif, Omari Gumbo, Ally Kajo, John Kadu (kocha mchezaji), Emmanuel Mbele, Mustafa Choteka, Kimimbi Yusuf Omari.
Mwaka 1971 Mayaula aliondoka Dar es Salaam na kwenda jijini Charleroi, Ubelgiji ili kujiendeleza kimasomo katika kozi ya Data Processing. Huko akajiunga na klabu ya Racing Club de Charleroi kabla ya kujiunga na Racing Club de Jette ya Brussels. Kwa muda mfupi alichezea klabu ya FC Fribourg ya Uswisi, na ni katika kipindi hicho alipoanza kujifunza kupiga gitaa. Muda si mrefu akajiunga na bendi ya wanafunzi Wacongo waliokuwa wanasoma Uswisi iliyoitwa Orchestra Africana akiwa anapiga gitaa la rhythm.
Aliporudi Kinshasa mwaka 1973, Mayaula akabadili kazi kutoka kwenye mpira na kuwa mwanamuziki mtunzi, hakuchukua muda mrefu akagunduliwa na Franco Luambo makiadi aliyemtaka ajiunge na TP OK Jazz, na ndio wakati huo Mayaula Mayoni akatoa kibao cha Cherie Bondowe. Wimbo huo ulipokelewa vizuri sana na wapenzi wa muziki lakini National Censorship Commission ya Zaire wakati huo, iliupiga marufuku kwa kuwa ulikuwa ni wimbo ambao hadithi yake ilikuwa ni ya kahaba mmoja aliyekuwa akielezea shughuli zake zilivyo, Commission iliona wimbo unatetea ukahaba, hivyo kuupiga marufuku. TP OK Jazz ililazimika kuusambaza wimbo huo kutokea Ubelgiji na hatimaye ukaenea Congo na sehemu nyingine za Afrika.
Inasemekana kuwa licha ya Franco kumkaribisha OK Jazz, lakini Mayaula Mayoni hakuwahi kuwa mwanachama halisi wa kundi hilo kwani alipendelea kuwa huru kutunga nyimbo zake na kumpa msanii aliyemtaka. Tungo zake kadhaa zilifanyiwa kazi na TP OK Jazz kama vile Nabali Mizele na Moni.
Mwaka 1977 wimbo wake wa Ndaya ulichukuliwa na kuimbwa na mwanamuziki M’pongo Love. Wimbo huo maarufu ulikuwa unaongea kuhusu mwanamke aliye na furaha kutokana na kuwa na mume bora na kuweza kumdhibiti asitangetange kwa wanawake wengine.
Mwaka 1981 Mayaula Mayoni aliondoka Zaire akiwa na wanamuziki kutoka bendi ya Abeti Masikini walikuhamia Afrika Magharibi ambako kati ya mwaka huo na 1984 alirekodi album kadhaa chini ya label ya Disc-Oriënt ya Lome, Togo. Mwaka 1984 alirudi Zaire na mwaka 1986 alitoa album iliyoitwa Fiona Fiona, na mwaka huohuo Tshala Muana alipata umaarufu kutokana na wimbo Nasi Nabali, uliotungwa na Mayaula Mayoni. Baada ya hapo akarekodi album yake ya Mizele akiwa na TP OK Jazz wakisindikizwa na waimbaji Carlito Lassa na Malage de Lugendo.
Mwaka 1993 alitoa album ya L’amour au kilo (yaani Mapenzi maziko kama kilogramu) akiwa na kundi la Soukous Stars lililowahusisha wanamuziki nyota kama Lokassa ya Mbongo, Ngouma Lokito, Balou Canta, Lucien Bokilo na wengineo. Albam hiyo iliyokuwa na nyimbo nyingi kali kama Mbongo Ebima, ilifanya vizuri sokoni n ahata alipofanya ziara nchini Tanzania mwaka 1994 alipata mashabiki wengi licha ya kwanza wadhamini waliomleta walifanya ufisadi kiasi cha kushindwa kumlipa fedha zake, hivyo bendi hiyo kukwama jijini Dar es Salaam. Wanamuziki wa bendi hiyo waliondoka mafungu mafungu na Mayaula Mayoni, akiwa amempata mwanamke Mtanzania aliyekuwa akifanya kazi kwenye kampuni moja ya wakala wa utalii, akaamua kubaki kwa muda jijini humo.
Miaka saba baadaye akatoa album nyingine ya Bikini. Baada ya album hiyo Mayaula alihamia Dar es Salaam na kuanza kufanya kazi Ubalozi wa Congo. Hata hivyo, muda si mrefu akaanza kuugua na kuamua kurudi Matadi, kwao alikozaliwa. Hali yake ilizidi kuwa mbaya mwaka 2005 akapelekwa Ubelgiji kwa matibabu na hatimaye kufariki dunia jijini Brussels Mei 26, 2010 akiwa na umri wa miaka 64. Alizikwa jijini Kinshasa.

Mafanikio
Katika maisha yake alichaguliwa mtunzi bora wa Zaire mwaka 1978 kwa wimbo wa Bondowe 2, mwaka 1979 kwa wimbo Nabali Mizele na mwaka 1993 wimbo wa Ousmane Bakayoko.

Comments