- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega,
MaendeleoVijijini Blog
JUMAMOSI Agosti 10, 1974 ni siku ambayo ina kumbukumbu ya
pekee katika soka la Tanzania, kwani ndiyo siku soka la uhakika na la ushindani
baina ya Simba na Yanga lilionekana kwa mara ya mwisho.
Ni mechi hiyo ambayo binafsi huwa ninaiita ‘Thriller’ ambayo
ilichezwa pale Nyamagana, Mwanza.
Lakini MaendeleoVijijini inatambua kwamba, hiyo ndiyo siku ambayo beki mashuhuri namba nne wa Yanga,
Mzizima United (timu ya Mkoa wa Dar es Salaam) na Taifa Stars, Hassan Gobbos maarufu
kama ‘King Hassan wa Morocco’, aliamua kutundika daruga baada ya filimbi ya
mwisho na kumkabidhi majukumu hayo beki msomi, Engineer Leodegar Chilla Tenga
kwenye timu zote hizo.
Nilipata kufanya naye mazungumzo mwaka 2002 wakati akiwa
mtumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) – sijui kama bado yuko pale – na aliniambia
sababu za kuamua kutundika daruga zilikuwa kujikita zaidi kwenye kazi kwani
umri nao ulikuwa unayoyoma!
Lakini anakumbuka vyema mchezo ule wa fainali baina ya Yanga
na Simba pale Nyamagana jinsi ulivyokuwa na ushindani mkubwa.
“Tangu wakati ule sijaona mchezo wa Simba na Yanga wenye
ushindani, zaidi utasikia majigambo tu kwenye vyombo vya habari na ukienda
uwanjani unakuta hali iko tofauti kabisa,” alisema Gobbos ambaye siku hiyo kama
kawaida yake alicheza namba 4 na akampisha Boi Idd.
Kikosi cha siku hiyo cha Yanga kilikuwa na Elias Michael
ambaye aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na Muhidin Fadhil, Ally Yussuf,
Selemani Saidi Sanga, Hassan Gobbos/Boi Iddi 'Wickens', Omari Kapera,
Abdulrahman Juma (nahodha), Bona Max Mwangi, Sunday Manara, Kitwana Manara,
Gibson Sembuli na Maulid Dilunga, kikiwa kinanolewa na Tambwe Leya kutoka Zaire.
Simba wao waliwakilishwa na Athumani Mambosasa, Shaaban
Baraza, Mohammed Kajole, Athumani Juma, Omari Chogo, Omari Gumbo, Willy
Mwaijibe aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na Kessy Manangu, Haidari Abeid
'Muchacho' (nahodha), Saad Ally aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na Adamu
Sabu, Abdallah Kibadeni, na Abbas Dilunga ‘Sungura’. Walikuwa wananolewa na Paul
West Gwivaha.
Gobbos anakumbuka kwamba, hadi kufikia fainali Agosti 10,
1974, kulikuwa na ushindani mkubwa kwenye ligi hiyo iliyofanyika Mwanza kuanzia
Julai 18 mpaka Agosti 10, 1974 katika Uwanja wa Nyamagana.
“Kwa matayarisho ya michuano ya mwaka huo Yanga tulikwenda
kuzuru Brazil na Simba walikwenda Poland, na ndizo timu ambazo zilikuwa na
vikosi imara zaidi msimu huo,” anakumbuka.
Msimu huo timu zilikuwa Yanga, Kazi Mara, Comworks Singida,
Ntomoko Dodoma, Miembeni Zanzibar, Ujenzi Rukwa, Simba, Kaye ya Iringa, Ufundi Kigoma,
Nyota Mtwara, Coast Stars ya Bagamoyo, Mwadui ya Shinyanga, Magunia Kilimanjaro,
Madaraka Rubuma, Polisi Bukoba, na Jeshi Zanzibar.
Nyingine zilikuwa Jeshi Tabora, Rungwe Sekondari, Nyota Tanga,
Jeshi Lindi, Jumuiya Arusha, na Mwatex.
Katika nusu fainali, Yanga iliifunga Miembeni ya Zanzibar
mabao 2-1 huku mabao yote ya Yanga yakifungwa na mshambuliaji mwenye mashuti
makali ambaye hajapata kutokea tena, Gibson Sembuli, wakati Salhina aliifungia
Miembeni bao la kufutia machozi.
Simba yenyewe iliitoa Jeshi Tabora kwa mabao 3-0 ambapo
Hilary wa Jeshi alijifunga katika jitihada za kuokoa na mabao mengine yalifungwa
na Saad Ally na Adam Sabu.
“Ndiposa tukakutana na Simba kwenye fainali na kwa hakika kila
timu ilikuwa imara mno,” alisema Gobbos wakati huo akikumbuka mechi hiyo ya
aina yake.
Inakumbukwa kwamba, siku hiyo Uwanja wa Nyamagana ulifurika
watu isivyo kawaida. Mashabiki walitoka sehemu mbalimbali za nchi - Arusha,
Moshi, Tanga, Dodoma, Dar es Salaam, Tabora, Shinyanga, Kigoma, Morogoro, Mara
na Kagera. Hao ni licha ya wale waliotoka kwenye vitongoji vya Mwanza.
Ilipofika saa 10.30 jioni hapakuwa na nafasi ya kukaa mtu hapo uwanjani, ingawa
wengine walikuwa wanaendelea kumiminika.
Mchezo ulianza kwa nguvu ingawa Yanga walianza pole pole
kidogo wakijaribu kuusoma mchezo wa Simba. Baada ya dakika tano tu matokeo ya
nguvu hizo yalionekana. Saad Ally wa Simba aliumia baada ya kugongana na Gibson
Sembuli wa Yanga na akatolewa nje. Adamu Sabu aliyeingia badala yake,
aliwafurahisha wapenzi wa Simba, kwani aliifungia goli timu yake katika dakika
ya 16.
Katika pambano hilo, golikipa wa Yanga, Elias Michael
aligongana na Willy Mwaijibe wa Simba katika dakika ya 70 na wote wawili
wakakimbizwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando. Nafasi zao zilichukuliwa na
Muhidin Fadhil kwa upande wa Yanga na Kessy Manangu kwa upande wa Simba.
Yanga walijaribu sana kukomboa goli hilo lakini walipata taabu
kwani ukuta wa Simba ulikuwa imara sana. Kadiri mchezo ulivyoendelea watu walidhani
Yanga isingepata hata goli moja na kwamba, siku hiyo ingefungwa tena, kwani
hadi mapumziko matokeo yalikuwa ni yale yale ya goli moja kwa Simba na Yanga
wakiwa na gurudumu.
Katika dakika ya 87 ya mchezo, yaani dakika tatu kabla ya
mchezo kumalizika, mambo yalibadilika. Ilikuwa ni golikiki, ambapo mlinzi wa
Yanga, Ally Yussuf, alipiga mpira kuelekea golini kwa Simba. Mpira huo ulipita
juu ya vichwa vya wachezaji kadhaa wakiwemo Abdallah Kibadeni wa Simba na
Gibson Sembuli na Sunday Manara.
Mpira huo uliambaa ambaa kuelekea goli la Simba ambako Kitwana
Manara, aliyekuwa amebanwa mno na beki wa Simba ambaye hakutaka mchezo, Omari
Chogo 'Chemba', licha ya kuwa ameupa mgongo mpira huo aliruka na kupiga kichwa
kushoto kwake.
Moja kwa moja mpira huo uliingia kwenye 'anga' za nambari tisa
wa Yanga, Gibson Sembuli, aliyeujaza wavuni kwa shuti kali la ugoko,
lililoingilia kwenye kona ya kushoto na kumuacha kipa Athumani Mambosasa,
aliyekuwa ametoka kumkabili mchezaji huyo, akiwa hana la kufanya zaidi ya
kuutumbulia macho mpira huo ukitinga wavuni kuandika goli la kusawazisha kwa
Yanga. Hivyo, hadi mwisho wa dakika 90 za kawaida za mchezo matokeo yalikuwa
1-1.
Goli hilo likabadilisha kabisa sura ya mchezo. Watazamaji
ambao walianza kuondoka uwanjani wakidhani Yanga wameshindwa walirudi tena
uwanjani kuangalia mchezo. Dakika 90 zilipokwisha ubao wa matokeo ukasomeka
Yanga 1 Simba 1 na ndipo dakika 30 zilipoongezwa ili kupata mshindi.
Katika dakika ya saba ya muda wa nyongeza, mlinzi Ally Yussuf
wa Yanga aliipangua ngome ya Simba na kutoa pasi ya juu kwa mchezaji wa kiungo
wa Yanga, Sunday Ramadhan Manara, aliyefunga goli la pili kwa kichwa. Goli hilo
likawa la ushindi kwa Yanga baada ya Simba kushindwa kusawazisha kwa dakika 23
zilizokuwa zimesalia.
“Ilikuwa mechi ngumu mno, haijapata kutokea,” alisema Gobbos,
ambaye mwaka huo pia alikuwemo kwenye kikosi cha Tanzania Bara kilichotwaa
Kombe la Chalenji.
Harakati zake
MaendeleoVijijini inatambua kwamba, harakati za Hassan Gobbos katika kutandaza ndinga zilianza
alipokuwa darasa la tano, Mundemu Middle School, maili 12 kutoka Dodoma mjini.
Akiwa shuleni hapo aliiwakilisha wilaya ya Dodoma katika mashindano ya kikombe
cha Magwaya yaliyotumika wakati huo kupata wachezaji waliounda timu ya mkoa wa
Dodoma (Central Province) kwa ajili ya michuano ya Sunlight Cup (sasa Taifa
Cup). Wilaya nyingine zilizoshiriki zilikuwa Kondoa na Mpwapwa.
Mwaka 1963, Gobbos alichaguliwa kuendelea na masomo ya
sekondari, Dodoma Sekondari, na mwaka huo huo, kutokana na kile alichokielezea
mwenyewe kuwa ni kujiendeleza kimpira, Gobbos alijiunga na timu ya Young
Africans ya mjini Dodoma. Ikumbukwe kwamba zamani Simba (wakati huo Sunderland)
na Yanga zilikuwa na matawi yake katika mikoa mbalimbali ambayo nayo yalichukua
majina hayo hayo.
Uzoefu alioupata wakati wa Magwaya Cup ulimuwezesha kupata
namba ya kudumu (nambari tano) kwenye timu ya mkoa wa Dodoma ambao aliuwakilisha
katika mashindano ya Sunlight Cup lililoshindaniwa kwa mara ya mwisho mwaka
1963, kabla ya kubadilishwa na kuwa Taifa Cup, ambapo pia aliuwakilisha mkoa
huo hadi mwaka 1966.
Akicheza kwa utulivu na kuutumia vizuri urefu wake Hassan
Gobbos aliweza kufagia hatari nyingi kabla hazijasababisha madhara langoni
wakati wa enzi zake. Alikuwa kiboko cha washambuliaji.
Mwaka 1964 alipokuwa kidato cha pili, Hassan Gobbos
aliiwakilisha timu ya Taifa ya Vijana iliyokwenda Malawi kuadhimisha Uhuru wa
nchi hiyo, Julai 6. Huo ulikuwa mchezo wa kwanza wa kimataifa kwa mwanasoka
huyo. Pia aliuwakilisha mkoa wa Dodoma katika riadha, hasa mbio za mita 400
kupokezana vijiti (relay) na kuruka juu.
Januari 1967, Hassan Gobbos alijiunga na Young Africans ya Dar
es Salaam baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari mwaka 1966 mjini Dodoma,
wakati huo huo akiwa mwajiriwa bandarini. Haukupita muda viongozi wa soka
mkoani Dar es Salaam wakawa wamemmulika mchezaji huyo, ambapo alikuwemo katika
orodha ya wachezaji wa mkoa wa Dar es Salaam waliochaguliwa kuuwakilisha mkoa
katika michuano ya Taifa Cup mwaka 1967.
Baada ya mwaka 1964, Hassan Gobbos alipata fursa tena ya kuvaa
jezi ya taifa mwaka 1968 alipochaguliwa kuchezea timu ya wakubwa, Taifa Stars.
Tangu mwaka huo hakuivua jezi hiyo nambari nne kwenye timu ya taifa hadi mwaka
1974 alipoamua kutoweka kabisa uwanjani.
Hassan Gobbos bado anayakumbuka sana mashindano ya kuwania
Kombe la Chalenji ya mwaka 1970 yaliyofanyika mjini Nairobi, Kenya, hususan
mchezo wa mwisho dhidi ya timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars. Baada ya
kuzishinda Uganda na Zanzibar, Kenya na Tanzania Bara zilitoka sare ya bao 1-1.
Hata hivyo, Kenya walichukua kombe kwa wingi wa mabao.
"Wenzetu Kenya walikuwa ndiyo kwanza wamerejea kutoka
Ujerumani Magharibi kujiandaa kwa mashindano hayo. Walicheza mchezo tofauti na
sisi na walikuwa na stamina ya hali ya juu sana," alieleza Gobbos.
Maoni ya mchezaji huyo wa zamani kuhusu hali ya kandanda
nchini ni kwamba, imeshuka. Sababu kadhaa alizozitaja kuhusiana na kuporomoka
kwa kiwango cha soka nchini ni pamoja na kukosekana mara kwa mara kwa vifaa vya
michezo, kukosa michezo ya kutosha ya kimataifa ya majaribio wakati timu zetu
zinapojiandaa na michuano ya kimataifa na pia kukosekana kwa miundombinu pamoja
na programu za maendeleo ya mchezo huo.
"Kwa mfano enzi zetu, Yanga ilikwenda Brazil na Simba
ilikwenda Poland kwa ajili ya kujiandaa na Ligi ya taifa mwaka 1974, achilia
mbali michezo ya kimataifa," alisema.
Pia alitoa wito kwa klabu kubwa hapa nchini kuacha mtindo wa
kuwarubuni wachezaji kutoka timu nyingine, hasa za mikoani, ambapo inaonyesha
dhahiri kwamba wengi wa wachezaji hao wamekuwa wakiishia kukaa benchi na hivyo
vipaji vyao kufa haraka, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linarudisha nyuma
maendeleo ya soka.
"Mchezaji yeyote yule wa kurubuniwa kwa fedha huwa hana
ari anayopaswa kuwa nayo mchezaji uwanjani na anaweza pia akarubuniwa na klabu
nyingine pinzani kuihujumu klabu anayoichezea. Badala ya kunyang'anyana
wachezaji, ni vyema klabu zote zirejeshe mpango wa zamani wa kuwaandaa vijana
chipukizi kuwa wachezaji wa baadaye," aliongeza.
Wachezaji waliomfurahisha enzi zake walikuwa Kitwana Ramadhan
Manara 'Popat' au 'Mtafutaji magoli', Leonard Chitete na Omari Kapera, ambaye
kwa utani alimwita 'Jeuri'.
Kwa wachezaji wa nje alivutiwa sana na Johan Cruyff
mshambuliaji nambari 10 wa Uholanzi na beki nambari mbili Ben Kusi wa Asante
Kotoko na timu ya Taifa ya Ghana, Black Stars.
“Huyu Kusi tulicheza naye katika Klabu Bingwa Afrika mwaka
1969 na 1970,” alisema.
Makala haya yameandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com, simu 0656-331974. Kama utayatumia kwa namna yoyote ile ni lazima utoe credit kwa mwandishi Daniel Mbega au MaendeleoVijijini Blog.
Makala haya yameandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com, simu 0656-331974. Kama utayatumia kwa namna yoyote ile ni lazima utoe credit kwa mwandishi Daniel Mbega au MaendeleoVijijini Blog.
Comments
Post a Comment