- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
BARAKA KITENGE 'ASKARI' WA YANGA ALIYEWAHANGAISHA WASHAMBULIAJI, NDIYE BABA WA MTANGAZAJI MAULID KITENGE
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Baraka Kitenge 'Askari au Zagallo'
Na Daniel Mbega,
MaendeleoVijijini Blog
Kuzaliwa: 1942
Mahali: Tabora
Jina
la utani: Askari au Zagallo
Nafasi
uwanjani: Beki 2
Alianza
kucheza soka: miaka 8
Timu: Young Boys (Tabora) 1961
- 1965; Yanga (Dar) 1966 - 1971; Timu ya Mkoa wa Tabora (Western Province) 1963
- 1965; Timu ya Mkoa wa Pwani (Mzizima United) 1966 - 1971.
Mafanikio: Robo fainali ya Klabu
Bingwa Afrika (Yanga) 1969 na 1970; Ubingwa wa Taifa (Yanga) 1968, 169, 1970,
1971.
WAPENZI
wa kandanda walimwita 'Askari au Zagallo' wakimfananisha na beki nambari mbili
wa Brazil enzi hizo, Mario Jose Lobo Zagallo, kwa uwezo wake wa kumchunga adui
barabara uwanjani. Lakini jina lake halisi ni Kitenge Baraka Said, beki nambari
mbili wa zamani wa Young Africans aliyeichezea timu hiyo kwa miaka mitano.
Mzaliwa
wa Tabora, mwaka 1942, Kitenge Baraka alivua jezi mapema mwaka 1971 baada ya
miaka 20 ya uchezaji. Alianza kulisukuma gozi akiwa na miaka nane na aliendelea
na ari ya kuupenda mchezo huo wa kandanda alipoanza masomo ya msingi shule Town
School hadi sekondari Kazima Sekondari zote za mjini Tabora.
Alishamiri
zaidi kimpira wakati bado akiwa mwanafunzi wa sekondari huko Kazima. Kwa
kipindi cha miaka minne ya sekondari (kuanzia 1961 hadi 1965), pamoja na
kuchezea timu ya hapo shuleni, Kitenge Baraka alikuwa mpenzi na mchezaji wa
Young Boys ya Tabora aliyoiwakilisha katika michezo ya ligi. Wakati huo alikuwa
akichezea nafasi ya mshambuliaji nambari 9. Nafasi nyingine alizowahi kuchezea
ni wingi ya kulia (nambari 7), sentahafu (mkoba - 5) na beki nambari mbili,
nafasi aliyoichezea hadi alipostaafu.
Mwishoni
mwa 1965 baada ya kumaliza kidato cha nne alikuja mjini Dar es Salaam na
kuajiriwa na Shirika la Upakiaji na Upakuaji Mizigo Bandarini (East African
Cargo Handling Services, sasa Tanzania Harbours Authority). Mara tu alipowasili
Dar es Salaam viongozi wa klabu za soka mjini humo walianza kumshawishi ajiunge
na timu zao, kwani hakuwa mgeni kwao. Walikwisha muona akishiriki mashindano ya
Sunlight Cup (sasa Taifa Cup) akiwa na timu ya mkoa wa Tabora (Western
Province). Lakini chaguo lake likawa Yanga, aliyojiunga nayo mwaka 1966.
Mwaka
huo huo alichaguliwa kuunda timu mchanganyiko ya mkoa wa Dar es Salaam (Mzizima
United) kugombea Kombe la Taifa. Pamoja naye walikuwemo wanasoka wengine
mashuhuri wa nyakati hizo, akina Emmanuel Albert Mbele 'Dubwi', Abrahaman
Lukongo, golikipa Kitwana Ramadhan Manara 'Popat' ambaye baadaye alikuja
kubadilisha nafasi na kuwa mshambuliaji hatari wa Yanga na Taifa Stars, Arthur Mambetta, Mustafa Choteka, na
wengineo. Hakuwahi kuachwa katika orodha ya Dar-Kombaini (mara nyingine Pwani)
mpaka alipoamua kutundika njumu ukutani. Anakumbuka mwanandinga huyo katika
mahojiano yaliyofanyika mwaka 1984.
Mwaka
1967 alipata fursa ya kuliwakilisha taifa katika mashindano ya Kombe la Afrika
Mashariki (Kombe la Chalenji) na Kombe la Nchi Huru za Afrika (sasa Kombe la
Mataifa Afrika), Madagascar na hapa nyumbani na aliendelea kuichezea Taifa
Stars kwa miaka mitatu.
"Nilivutiwa
sana na mchezaji Ramadhan Abdallah 'Kitumbo' aliyekuwa mshambuliaji wa timu ya
Mkoa wa Tabora na timu ya Taifa (Tanganyika), ambapo sifa zake zilinifanya niwe
mwanasoka. Kweli nilifanikiwa," alisema Kitenge Baraka.
Mchezo
mgumu kuliko yote ambayo Kitenge amewahi kucheza katika historia yake ni baina
ya Yanga na Asante Kotoko ya Ghana mwaka 1969 kuwania Kombe la Klabu Bingwa
barani Afrika. Katika mchezo huo wa robo fainali timu zilikwenda sare baada ya
dakika 210 za mchezo ugenini na nyumbani (Kumasi na Dar es Salaam). Kwa kuwa
sheria ya penati tano tano ilikuwa haijaanza kutumika, Asante Kotoko, mabingwa
wa Afrika mwaka 1969 na 1970, walipata ushindi wa shilingi. Michezo yote
ilikuwa migumu kwa kuwa timu zote zilicheza mtindo unaofanana.
Akizungumzia
kuhusu wacheza wa enzi zake, aliwasifu sana Maulidi Dilunga 'Mtoto wa Mexico'
na Gilbert Mahinya 'Mashine', ambao alisema kwamba aliwahusudu kutokana na
bidii yao uwanjani na uwezo wa kupachika mabao. "Japokuwa Gilbert Mahinya
alikuwa mchezaji wa kiungo, lakini aliweza kucheza mbele na nyuma bila kuchoka
na kufunga mabao ya pembeni sana (impossible angles) tokea umbali wa mita 30 na
zaidi," alisema.
Wachezaji
wa miaka ya '80 waliokuwa wakimvutia walikuwa Athumani Juma 'Chama' mchezaji
bora kwa mwaka 1983 na 1984 na Hamisi Ramadhani 'Kinye' golikipa wa Yanga na
Taifa Stars.
"Kumekuwa
na hali ya kuridhisha katika kabumbu hivi sasa kutokana na mbinu za kisasa
wanazofundishwa wachezaji wetu na walimu mbalimbali. Isipokuwa wachezaji bado
wanashindwa kuzingatia miiko inayotawala mchezo wa mpira hasa nyakati za
mashindano makubwa. Fedha zimetawala mawazo ya wachezaji wengi, lakini pamoja
na tamaa ya baadhi ya wachezaji hali ya soka imepanda," alipata kusema
Kitenge.
Baraka
Kitenge ambaye pia ni baba wa mtangazaji maarufu Maulidi Baraka Kitenge alifariki
dunia Agosti 20, 2013 akiwa na umri wa miaka 74!
Comments
Post a Comment