Zaidi
ya watanzania 56 katika vijiji vya Chamchuzi na Buguluka vilivyoko
katika kata ya Bwelanyange iliyoko wilayani Karagwe mkoani Kagera
waliokuwa wakijihusisha na shughuli za uvuvi ndani ya mto Kagera na Ziwa
Hiema wanadaiwa kutekwa na kuuawa kikatili na watu wanaodhaniwa kuwa ni
askari wa nchi jirani Rwanda ambao mara kwa mara hufanya doria ndani ya
mto huo na ziwa hilo.
Vitendo vya watanzania kutekwa na kuuwawa kikatili vimeshtua mkuu wa
wilaya ya Karagwe Godfrey Muheruka anayelazimika kufanya ziara ya
kutembelea mwalo wa Rukombe ambao hutumiwa na wananchi wa vijiji vya
Chamchuzi na Buguluka na baadae kukutana na wananchi wa vijiji hivyo
viwili miongoni mwao wakiwemo wajane 59 ambao wanaume wao wanasadikiwa
kuuwawa, baadhi ya watanzania walionusurika kifo wenye majeraha
mbalimbali ya risasi na Mtanzania aliyekombolewa hivi karibuni toka
nchini Rwanda ambao wametoa shuhuda mbalimbali.
Afisa mtendaji wa kata ya Bwelanyange Nicolaus Lubambala kwenye taarifa
yake iliyosomwa na Godwin Mbeikya ambaye mratibu elimu kata ya
Bwelanyange ameeleza kuwa matukio ya watanzania kuuwawa yamekuwa
yakiongezeka kila kunapokucha, kufuatia matukio hayo mkuu wa wilaya ya
Karagwe Godfrey Muheruka amepiga marufuku shughuli za uvuvi ndani ya mto
Kagera na ziwa hiema hadi ufumbuzi wa tatizo hilo utakapopatikana.
Hivi karibuni watanzania 9 katika wilaya ya Kyelwa waliokuwa wakifanya
shughuli za uvuvi ndani ya mto Kagera waliuwawa na watu wanaodhaniwa
askari wa nchi jirani ya Rwanda hali ambayo ilimsikitisha waziri wa
mambo ya ndani Mwigulu Nchemba aliyepata taarifa hiyo wakati akiwa
mkoani Kagera.
Chanzo: ITV
Comments
Post a Comment