Featured Post

WASANII WA TANZANIA UGHAIBUNI WAPAZA SAUTI KUPINGA MAANDAMANO YA UKUTA

 Ebraim Makunja

Ras Makunja anasema “Wanachi Tusikubali kufanywa chambo cha kuvunja amani tuliyoijenga”

Wasanii wa Kitanzania wanaoishi na kufanyia kazi zao nje ya nchi au ughaibuni, wametoa wito kwa wananchi wa Tanzania walio nyumbani na nje kupinga kwa nguvu zote maandamano yaliyopewa na jina la UKUTA yaliyopangwa kufanyika tarehe 1 Septemba 2016.
Wasanii hao wakikaririwa na vyombo vya habari walisema maandamano hayo hayana tija kwa Watanzania na zaidi yataleta mpasuko katika jamii.
Baadhi ya wasanii hao ni mwanamuziki Saidi Kanda anayeishi nchi Uingerea ambaye alisema: "Hakuna haja ya kuunga mkono maandamano yatakayo lisababishia taifa uvunjifu wa Amani.”

“Badala yake wanasiasa watuache wananchi tufanye shughuli zetu na kufurahia maisha,” alisema mwanamuziki Saidi Kanda, kiongozi wa Mvula-Mandondo Band ya Uingereza.
Kule Ujerumani nako Kiongozi wa Ngoma Africa Band mwanamuziki Ebraim Makunja, maarufu Kamanda Ras Makunja, alikuwa akiongea na vyombo vya habari kwa niaba ya wasanii waishio Ujerumani.
Mtazamo wa Kamanda Ras Makunja una hoja nzito kuhusu maandamano ya UKUTA alikaririwa akisema: “Watanzania tusikubali kufanywa mtaji au chanzo cha vurugu na uvunjivu wa amani ambayo kwa miaka tumeijenga, kwani hatuoni sababu yoyote ya msingi ya kuunga mkono maandamano ya UKUTA, sisi Watanzania ndio tuliopiga kura kuiweka serekali ya awamu ya tano, leo hii eti tuende mtaani kuandamana kuipinga kwa sababu ya watu wanaojiita UKUTA, kwa kweli itakuwa sawa na watoto walio juu ya tawi la mti na kuanza kulikata tawi walilokalia kwa shoka, ni sawa na ukichaa.”
Mwanamuziki huyo nguli alizidi kuhoji: “Hivi wanasiasa si tuliwapa muda wa kutushawishi kuwapigia kura katika kampeni zao na sasa uchaguzi umepita sasa kuna haja gani tena sisi raia tushawishiwe kuandamana maandamano ambayo tafsiri yake UKUTA kisheria hayakubaliki, yaani ukiyatazama kwa upana hayana nia ya AMANI! Yaani mfano wake yawe maandamano kama ya IRANI yaliyoshawishi kumtoa Shah?
“Lakini Tanzania sio Irani kwa sababu serikali ya Tanzania imechaguliwa na wananchi kihalali sasa leo sisi wapiga kura tena tuende mtaani kupinga kitu ambacho tumekichagua kihalali..?
“SHAH wa Iran alikuwa mfalme sio kiongozi wa kuchaguliwa ndio maana Khomein alishawishi wanafunzi waanze kuandamana. Maandamano ya India 1947 yakiongozwa na Gandhi yalikuwa ya kumuondoa mkoloni Mwingereza, sasa haya ya UKUTA na tafisiri yake ipo wazi ni yanini? Kwa faida zipi za taifa letu? TUNAWAOMBA WANANCHI TUSIKUBALI KABISA KUUNGA MKONO MAANDAMANO YA UKUTA, tusikubali kushawishiwa kuandamana kwa madai yasiyoleta maandeleo kwa taifa, tusikubali kila siku.
“Baadhi ya wanasiasa wanatuendesha mara tususie kupiga kura, mara tuandamane UKUTA, wakati nchi jirani wanachapa kazi sisi tupo katika siasa kila kukicha,” Ras Makunja alisisitiza kuwa anayo haki ya kutoa maoni yake kwani yeye ni raia halali wa Tanzania.



Comments