Featured Post

TUNDU LISSU: UKUTA UMEDHIHIRISHA CCM SIO CHAMA CHA SIASA




Kwa muda mrefu watu wengi wamekuwa wanafikiri kwamba nchi yetu inatawaliwa na chama cha siasa, yaani CCM. Hata hivyo, wapo wachache ambao walishaanza kuhoji kama CCM ni chama cha siasa hata kabla mfumo wa vyama vingi vya siasa kuruhusiwa miaka 25 iliyopita.

        Ukisoma 'The State and the Working People in Tanzania', kilichohaririwa na Prof. Issa G. Shivji na kuchapishwa mwaka '87, utagundua kwamba tayari kuna wasomi ambao walishaanza kuhoji kama kweli CCM ni chama cha siasa.

        Chama cha siasa huongoza kwa hoja za kisiasa, sio kwa bunduki, mizinga na mabomu. Chama cha siasa hushinda mijadala ya kisiasa kwa kutumia ushawishi wa hoja za kisiasa na kiitikadi, sio kwa vitisho vya kuua au kuvunja miguu ya mahasimu wake wa kisiasa. Chama cha siasa huenda kwa wananchi kuwashawishi wakiunge mkono, hakijifichi nyuma ya vyombo vya ukandamizaji vya dola na kuwatisha wananchi.

        Miaka miwili iliyopita Jakaya Kikwete aliwaambia wanaCCM wenzake waende kwa wananchi wakafanye kazi ya siasa, waache kutegemea kubebwa na Jeshi la Polisi. Hili limewashinda, bila majeshi na bunduki na mabomu, CCM haiwezi kufanya kazi ya siasa. Bila ma-DC na ma-OCD, CCM haiwezi chochote. Zamani walikuwa wanatuita sisi wapinzani vyama vya msimu vinavyosubiri uchaguzi ndio tufanye kazi ya siasa. Sasa wanatukataza kufanya kazi ya siasa mpaka tusubiri msimu wa uchaguzi. Sasa sisi ndio chama cha siasa, maCCM yamegeuka kuwa chama cha msimu.

        Wanajifanya walishinda uchaguzi lakini hawadiriki kuturuhusu sisi tulioshindwa kwenda kuongea na wananchi. Wenye hatia huwa na hofu - the guilty are afraid. Wanatukataza siasa kwa sababu wanajua hawakushinda uchaguzi na wanajua wananchi wengi wanajua hivyo. Na wanajua hawana majibu ya hoja nyingi za kisiasa za utawala huu wa kidikteta.

        Kwenye 'The State and the Working People in Tanzania' kuna makala inayoitwa 'The State and the Party' ambayo inazungumzia uhusiano kati ya CCM na vyombo vya dola, hasa majeshi. Tangu mwaka '64 lilipoundwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kumekuwa na mwingiliano mkubwa sana kati ya chama na vyombo vya ukandamizaji vya dola. Mfano mzuri wa uhusiano huu ni makada wa chama kuingizwa jeshini na kufanywa maafisa wa jeshi, na maafisa wa jeshi kufanywa makada wa chama na kupewa kazi za kisiasa na/au za kiraia. Wafikirie akina Kikwete, Kinana, Makamba, Nsa Kaisi, Kiwelu, Nnauye, Kafanabo, n.k. Orodha ni ndefu sana.

        Wakati wa mfumo wa chama kimoja, majeshi yaligeuzwa kuwa Mkoa wa Chama, sawa na mikoa ya kijiografia kama Dar au Singida. Lengo lilikuwa ni ku-integrate zaidi majeshi katika mfumo wa kisiasa na kiraia ili kuulinda mfumo unaotawala. Katika era ya vyama vingi, majeshi yameondolewa katika siasa kikatiba na kinadharia tu. Katika hali halisi, mambo hayajabadilika kwa kiasi chochote cha maana. Angalia wanajeshi walioko katika nyadhifa za kisiasa za kiraia kama ma-DC, ma-RC na sasa hata maKatibu Wakuu wa wizara. Wote hawa ni maCCM kwa Katiba ya sasa ya CCM. Angalia wanajeshi walioko katika uongozi wa CCM ambao jana tu walikuwa wanakatazwa na Katiba ya nchi kuwa wanachama wa vyama vya siasa. Kwa hiyo, kinachoonekana sasa kwa majeshi kujitokeza hadharani ili kuzuia UKUTA, ni ushahidi wa wazi kwamba CCM haiwezi tena kujenga hoja ya kisiasa kwa wananchi na ikakubaliwa.

        Sasa ni wakati wa mabavu ya kijeshi tu. Na wala sio utii wa sheria bila shuruti tena. Kwa vile sheria ya mikutano ya kisiasa na maandamano iko upande wetu, sasa ni wakati wa shuruti ya kijeshi bila sheria. Tukishinda vita hii ya sasa, watesi wetu hawatakuwa ni silaha nyingine yoyote itakayobaki.

Tutashinda. Wakati ni UKUTA. Aluta continua!!!!!!

CHANZO: JAMII FORUMS

Comments