Featured Post

SEPTEMBA MOSI NI KUPATWA KWA JUA AU KUPOTEA KWA CHADEMA?



 
  
Na Daniel Mbega
SEPTEMBA Mosi, 2016 saa 3:14 asubuhi hadi saa 8:00 mchana Watanzania na watu wengine hasa wa maeneo ya Afrika Mashariki, Afrika ya Kati, eneo la Madagascar na maeneo ya Bahari ya Atlantic na Bahari ya Hindi watashuhudia tukio la kupatwa na jua, ambalo kilele chake kitatokea saa 6:01 mchana na kitadumu kwa dakika 3 na sekunde 06.
Hili litakuwa tukio la pili la kupatwa na jua kutokea mwaka 2016 baada ya lile la Machi 9 ambalo lilitokea huko Mashariki ya Mbali hasa katika visiwa vya Palau, Papua New Guinea, Sulawesi, Indonesia, Sumatra, Singapore na Sri-Lanka na maeneo mengine ya kaskazini mwa Australia.

Lakini kwa kiza kitakachoonekana kwa takriban saa tano nzima, huenda kikaleta taswira nyingine ya kupotea kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika medani ya siasa, kwani ndiyo siku ambayo viongozi wa chama hicho wanawahamasisha wafuasi wao waandamane nchi nzima wakati wamekatazwa.
Nani atakwenda kuandamana ‘gizani’ na kukabiliana na mkono wa dola ni swali ambalo majibu yake huenda yakapatikana siku hiyo, kwani viongozi wa Chadema wameendelea kusisitiza kwamba wataandamana licha ya kwamba tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli, amekwishawaonya kwamba wasiandamane kwa kuwa maandamano na mikutano yote ya hadhara ya kisiasa imepigwa marufuku.
Wakati Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akipanga mikakati ya maandamano akiwa Kanda ya Kaskazini, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia chama hicho kwa mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa, naye yuko Kanda ya Nyanda za Juu Kusini akihamasisha maandamano hayo hayo na kuwataka wafuasi wa chama hicho wasiwe na wasiwasi.
Kinachofanywa na chama hicho, hususan viongozi wake, ni kupandikiza mbegu ya chuki na ukaidi kwa vijana wasiojitambua kwamba kukaidi maagizo ya serikali uwe ndio utamaduni wa kizazi kijacho, jambo ambalo ni la hatari kwa sababu litaweka tabaka la kizazi kisichofuata na kuzingatia taratibu na miongozo inayotolewa na serikali husika.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ametoa angalizo na kuwataka Chadema waachane na azma yao hiyo ya kushinikiza maandamano kinyume cha agizo la mkuu wa nchi, lakini badala yake amepuuzwa na viongozi hao ndiyo kwanza wanaendelea na mikakati yao bila kurudi nyuma.
Kama tukio hili lingekuwa la kwanza, pengine Watanzania wengi wangekuwa upande wao, lakini kwa bahati mbaya chama hicho kimekwishajipambanua muda mrefu kwa vitendo vyake na kauli za viongozi kwamba bila kufanya maandamano na figisu, kamwe hakiwezi kufanya siasa nchini.
Historia ni mwalimu mzuri sana, kwa sababu inatuonyesha tu katika kipindi cha takriban miaka nane iliyopita chama hicho kimekuwa kikiendesha siasa za kiharakati kwa maandamano bila chembe ya subira na simile.
Tulishuhudia katika awamu ya nne namna chama hicho kilivyosuguana na vyombo vya dola kila mara kinapoona mambo yake hayaendi, matokeo yake Watanzania wasio na hatia wamepoteza maisha na wengine wakapata ulemavu wa kudumu wakati walipokaidi amri ya vyombo vya dola kwenye maandamano ama mikutano.
Hili si jambo la kulichekea hata kidogo, hasa kama tunapenda kudumisha Amani, utulivu na mshikamano wetu.
Inawezekana Chadema hawafurahishwi na Amani iliyopo, ndiyo maana baadhi ya viongozi wamesikika mara kadhaa wakikejeli hata Amani hiyo kwamba si kitu na inatokana na wananchi kuwa wapole. Sasa nadhani wanataka kuwahamasisha wananchi wasiwe wakimya, tena waingie mitaani bila utaratibu rasmi kuondoa ukimya huo kwa kuchafua Amani.
Chadema ilikuwa mstari wa mbele kupinga ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, uzembe wa kutokusanya kodi na safari nyingi za viongozi nje ya nchi, lakini baada ya Rais John Magufuli kuyashughulikia masuala hayo kwa vitendo, wapinzani hao wamegeuka tena na kusema rais ni dikteta.
Maandamano na mikingamo imekuwa sehemu ya siasa za Chadema, chama ambacho awali kilionekana kuwa mkombozi na mbadala wa Chama cha Mapinduzi (CCM), na sasa taswira hiyo imepotea kwa Watanzania walio wengi kutokana na hatua yao ya kupinga kila kitu kinanchofanywa na serikali.
Watanzania wanaona kuna mabadiliko ya kiutendaji katika serikali hii na zilizotangulia, wana matumaini makubwa hata kama kuna wengine wanaumia kwa ‘kutumbuliwa’ kutokana na kutoendana na kasi iliyopo.
Inaonekana Chadema walikuwa na Imani kubwa kwamba mwaka 2015 lazima wangeingia Ikulu, lakini kitendo cha kushindwa licha ya jitihada za ‘kukodi majeshi yaliyotemwa CCM’ kimeonekana kuwachanganya na utendaji wa serikali ya awamu ya tano ndio umemaliza spidi yao, hivyo wamekuwa wakitafuta namna yoyote ya kukwamisha jitihada hizo.
Walianza kwa kugomea kuhudhuria sherehe za Dk. Magufuli kukabidhiwa hati ya ushindi, wakagomea kuapishwa kwake, alipokwenda kuzindua Bunge la 11 wakatoka, baada ya hapo wamekuwa wakigomea hata vikao vingine vya Bunge, likiwemo Bunge la Bajeti ambapo walimtuhumu Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson Mwansasu, kwamba ni mbabe.
Na hapo ndipo walipoanzisha harakati zao za kutaka kufanya maandamano, lakini tayari Rais Magufuli alikuwa amepiga marufuku mikutano ya kisiasa kwa maelezo kwamba siasa zilimalizika wakati wa kampeni na sasa Watanzania wanataka kuona maendeleo tu.
Uamuzi huo wa Rais Magufuli kwa Chadema umekuwa mtaji mkubwa wa kisiasa na wanautumia siyo tu kutaka warudi kwenye chati, bali wanataka kuiyumbisha serikali iache kuwatumikia wananchi na kupambana nao. Kwa kufanya hivyo tayari malengo yao yatakuwa yametimia, maana wapinzani siku zote kazi yao ni kupinga kila kitu kinachofanywa na serikali.
Katika mukhtadha huo, kuna wasiwasi kwamba, ikiwa Chadema wataendelea na mikakati yao hiyo na wakasababisha kutetereka kwa Amani na usalama, basi Sheria ya Vyama vya Siasa inaweza kutumika kuangalia uhalali wao wa kuendelea kuwepo kwenye orodha ya vyama vya siasa ama la.
Na kwa vile siku ambayo wamepanga kufanya maandamano itakumbwa na giza la kupatwa kwa jua (annular solar eclipse) kwa takriban saa tano, basi huenda giza hilo la kisayansi likatoa pia mwelekeo wa hatma ya Chadema.

CHANZO: TAZAMA

Comments