Featured Post

RC SINGIDA AKABIDHI MADAWATI 630 KWA WAKURUGENZI WA WILAYA NA MANISPAA

Na Mathias Canal, Singida

Wakurugenzi wa Manispaa na Halmashauri za Mkoa wa Singida wamekabidhiwa jumla ya madawati 90 kwa kila Halmashauri ili kuondoa adha waliyokuwa wanakumbana nayo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Mkoani humo ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kampeni ya kuchangia madawati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli alipowaagiza wakuu wa mikoa yote nchini wakati akiwaapisha Ikulu, jijini Dar es Salaam Machi 15, 2016.


Wakurugenzi hao wametakiwa kuyachukua haraka madawati hayo na kuyapeleka Katika shule zenye kadhia hiyo ikiwa ni ishara ya kuamsha taswira ya elimu kwa wanafunzi mchini kuondokana na mateso ya kukaa chini wakiwa darasani.

 Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe wakati wa makabidhiano hayo katika Ukumbi wa Ofisi za Mkoa huo huku akisifu wadau na Taasisi mbalimbali kujitolea kuunga mkono uchangiaji wa madawati ambao awali ulianza kwa ngazi ya Halmashauri kabla ya kuhusisha taasisi mbalimba sambamba na wadau wa maendeleo Mkoani humo.
Mtigumwe amesema kuwa Hali ya Madawati katika Mkoa ilikuwa chini ya asilimia 40% lakini chini ya uongozi wake kwa kushirikiana na wadau 67 wa Maendeleo wameweza kuchangia jumla ya shilingi milioni 42,626,500 hivyo kufanikisha lengo la utengenezaji wa madawati kufikia asilimia 98% ambapo hata hivyo upungufu Mkubwa ulikuwa zaidi katika Halmashauri za Singida na Manyoni.


Alisema kuwa mwanzoni mwa mwezi June mwaka huu aliteua kamati ndogo ya uratibu wa madawati kwa kushirikisha wadau mbalimbali katika Mkoa baada ya kuona juhudi za serikali kupitia mamlaka za Halmashauri yaManispaa na Wilaya.
Ameeleza kuwa kamati hiyo iliweza kukusanya Jumla ya shilingi milioni 42,626,500/= kutoka kwa wadau 67 (Pesa taslimu ikiwa ni 29,046,500) wadau watano walitoa madawato 60 yenye thamani ya shilingi 3,580,000/= na madawati 100 kutoka bonite Bottles Ltd yenye thamaniya shilingi 10,000,000/= ambapo jumla ya madawati yaliyotengenezwa ilikuwa ni 470.
 Akisoma Taarifa ya utengenezaji wa madawati Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Afisa Mifugo wa mkoa wa Singida Elias Donaty Seng’ongo amesema kuwa kupitia kamati ya kuratibu madawati walishirikisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Taasisi za serikali (TBA,Gispa, Tanroads, Sido, Veta, Temesa, Sekretarieti ya Mkoa (RS), Takukuru na TRA, Mashirika ya huduma (NHC, Tanesco, Suwasa, Posta, Taasisi za fedha (NMB, na CRDB), Mifuko ya hifadhi ya jamii (NHIF, NSSF, na PSPF), Mashirika yasiyo ya serikali (NGO’s, SEMA, HAPA, TUNAJALI, na HELVETAS).
Amewataja wadau wengine waliochangia kuwa ni Vyuo vya idara za serikali (NAO, Madini, Hazina Ndogo, Chuo cha Uhasibu, TIA, Utumishi wa Umma, Chuo cha walimu Singida, Abet English Medium School, Maasai English medium  School, Lake School, Viwanda vya usagishaji mafuta (Mount Meru na Umoja wa wakamuaji mafuta Mkoa wa Singida, Wafanyabiasharambalimbali, wauzaji wa vinywaji baridi) Bonite Bottles Ltd, Wauzaji wa vipuri vya magari, Makandarasi, Wakala wa huduma za misitu TFSAmaduka ya vifaa vya ujenzi, Hoteli na Baba na Mama Lishe Mkoani humo.
Seng’ongo alisema kuwa kupitia taarifa kutoka Ofisi ya Elimu Mkoa uliweza kufikia lengo la utengenezaji wa madawati kwa asilimia 98% ambapo juhudi bado zinaendelea kuhakikisha kuwa zoezi hilo linakuwa endelevu kwa siku zijazo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Wakurugenzi wote wa Halmashauri za mkoa wa Singida amewashukuru wadau wote waliochangia fedha Taslimu ama Madawati yakiwa tayari yametengenezwa huku akiwasihi wadau wote kuendelee kujitolea katika kuchangia shughuli za maendeleo katika Mkoa huo.
Pia amesema kuwa madwati hayo ana imani yatatunzwa vizuri ili wanafunzi waweze kusoma vizuri wakiwa wamekaa kwenye madawati kwani mwanafunzi akiketi kwenye dawati hata mwandiko na ufahamu wake unakuwa mzuri tofauti na mwanafunzi ambaye atasoma akiwa amekaa sakafuni hivyo kupitia upatikanaji wa madawati hayo ana imani kubwa kuwa mkoa wa singida utaimarika kielimu na kuimarisha ufaulu wa wanafunzi.
Naye Mfanyabiashara, Mkulima na Mfugaji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi Hassan Tati akizungumza kwa niaba ya wadau wote waliochangia amesema kuwa Mkuu wa mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe amebuni njia nzuri ya kuwapa motisha kwa kutoa Hati kwa wadau wote waliochangia jambo ambalo litaamsha ari zaidi katika kuchangia shughuli za Maendeleo ya Mkoa na taifakwa ujumla.
  Tati alisema kuwa anasikitika sana pale anaposikia kuwa mkoa wa Singida unashika nafasi ya Tano kwa umasikini katika Mikoa yote nchini ilihali ni mkoa wenye rutuba ya kutosha na eneo pana katika uwekezaji hivyo amewasihi wananchi na wadau kwa pamoja kushirikiana kwa pamoja katika kukomesha umasikini huo.


Comments