- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
Nigerian Dwarf ni
mbuzi wadogo wanaotoa maziwa kidogo na nyama ambao asili yao ni Nigeria, Afrika
Magharibi. Mbuzi hao mbilikimo wanafaa sana kwa familia ndogo kama inataka
kuwafuga kwa maziwa lakini ni lazima wawe wanatoka katika zizi ambalo lilikuwa
linawafuga kwa maziwa na siyo mapambo.
Mbuzi hao mbilikimo wana matiti
madogo kuliko mbuzi wa kawaida mkubwa, hivyo hata ukamuaji wake ni mgumu. Mbuzi
hao wanapatikana katika rangi zote na mbuzi jike mkubwa ana uzito wa kati ya
13.61 kilogramu hadi 22.68 kg wakati beberu ana kilogramu kati ya 35 hadi 60.
Mbuzi bora jike wa jamii hii anaweza
kutoa kiasi cha lita 340.19 za maziwa kwa mwaka ambayo yana wastani wa siagi na
mafuta asilimia 5 na yana protini nyingi. Maziwa ya mbuzi wa jamii hiiyanaelezwa kwamba ni matamu zaidi kuliko maziwa ya aina nyingine za mbuzi.
Mbuzi jamii ya Nigerian Dwarf hivi
sasa wamepata umaarufu mkubwa duniani kutokana na maumbile yao madogo na rangi
zao pia. Udogo wao unamaanisha kwamba hawahitaji eneo kubwa sana la kuwafugia
kama zilivyo jamii nyingine za mbuzi wa maziwa na upole wao unawafanya wawe
wanyama rafiki kwa jamii wanayoishi.
Ni rahisi kuwahudumia, kwani hata
watoto wadogo wanaweza kucheza nao bila hofu.
Japokuwa maumbile yao ni madogo,
lakini mbuzi hao hawana tofauti na mbuzi wengine. Miili yao imekaa vizuri, pua
imecongoka na masikio yamesimama. Ngozi yao ni laini yenye manyoya mafupi na
marefu kiasi na wanapatikana katika rangi mbalimbali.
Kimo cha mbuzi jike wa jamii hii ni
kati ya inchi 17 hadi 19 ingawa jike lenye kimo cha inchi 21 ndilo linafaa
zaidi kwa ufugaji wa maziwa. Bebeeru ana kimo cha inchi 19 hadi 21 huku wenyewe
inchi 23 ndio wanaofaa kwa ufugaji.
Mbuzi wa jamii ya Nigerian Dwarfs ni
wapole na unaweza kucheza nao. Sifa hiyo inawafanya wawe rafiki wa familia
nzima kuanzia watoto hadi watu wenye ulemavu na wazee. Hata mabeberu wake siyo
wakorofi.
Wafugaji wa jamii nyingine ya mbuziwa maziwa wanaweza kuwachanganya Mbilikimo hao na mbuzi wengine bila shida.
Wanachunga pamoja na wanyama wengine kama ng’ombe, punda, farasi, llama na
wengineo na wanakula vyakula vingine ambavyo wanyama hao wanakula.
Mbuzi wanapaswa kuwekwa kwenye
mabanda masafi ambayo hayana uchafu wala wadudu wengine kama inzi, kupe na
kadhalika. Pia wanahitaji kuwekewa kingo (fence) kutokana na maumbo yao madogo.
Mbuzi hao hawatakiwi kuwekwa katika
eneo ambalo halina hewa ya kutosha, wanahitaji hewa na mwanga kwa ajili ya
afya. Banda la mbwa mkubwa linaweza kuwatosha mbuzi hata watatu wa jamii hii.
Lakini ni muhimu kuhakikisha kwamba
mabanda ni masafi daima na yametandikwa matandazo mazuri kwa ajili ya kulalia.
Wafugaji wengine wanaona kuwawekea vitu kama magogo ama mawe kwa ajili ya
kucheza na kurukaruka kunawafanya mbuzi hao wawe huru zaidi. Hakikisha
unawaweka mbali na uzio ili kuzuia wasitoroke maana ni wepesi wa kukimbilia
hata nyumba za jirani!
Uzalishaji wa mbuzi jamii hii ni wa
mwaka mzima, hawana msimu. Wafugaji wengi wanahakikisha mbuzi hao wanazaa mara
tatu ndani ya miaka miwili na kulipatika mbuzi jike muda wa kupumzika wa miezi
sita. Hata hivyo, huo ni utashi wa mfugaji mwenyewe kwa sababu mbuzi hao
wanazaa baada ya siku kati ya 145 hadi 153 (miezi mitano).
Kwa sehemu kubwa, Nigerian Dwarfs ni
mbuzi wanaozaa vyema bila matatizo ya uzazi. Watoto wanakuwa na uzito wa
wastani wa paundi 2 wanapozaliwa lakini wanakua haraka. Kuwa makini na mabeberu
wadogo kwa sababu wanakomaa na kuweza kuzalisha wakiwa na wiki 7 tu! Hakikisha
unawaachisha kunyonya majike na madume kwa nyakati tofauti ili kuepuka wasije
wakabebeshana mimba bado wadogo.
Majike wanaweza kuwa tayari kubeba
mimba wanapofikisha miezi 7 hadi 8 kama wamekua vyema. Wafugaji wengine
husubiri mpaka wafikishe walau mwaka mmoja. Mbuzi wa jamii hii wanaweza kuzaa mapacha
watatu au wanne kwa mara moja. Mbuzi hao mbilikimo ni mama wazuri na wanaweza
wakawalea watoto wao hata kama utawaachia. Pia wanaweza kutoa kiasi cha kutosha
cha maziwa kwa familia kama utakuwa unalenga kuwafuga kwa ajili ya uzalishaji
wa maziwa na unaweza kutengeneza siagi ya kutosha kwa maziwa hayo.
Mabeberu wanaweza kutumika
kupandishwa wanapofikisha umri wa miezi mitatu ingawa ni vyema kusubiri
wafikishe miezi 7 hadi 8. Ni mabeberu wazuri hata kama utachukua beberu mmoja
kwa ajili ya kundi la majike kadhaa.
Wafugaji wengi wanawalisha mbuzi hao
wastani wa asilimia 12% – 18% wa vyakula vya protini au vyakula maalum vya
mbuzi wa maziwa. Hakikisha chakula hicho hakina Urea kwa sababu hivyo ni sumu
kwa mbuzi.
Wafugaji wengi wanawapa nafasi kidogo
kama nyasi zipo za kutosha. Nyasi au malisho lazima yawepo ya kutosha. Maji
safi lazima yawekwe kwenye vyombo safi na inabidi yapatikane wakati wote.
Kama ilivyo kwa jamii nyingine yambuzi, hawa mbilikimo nao wanahitaji uangalizi mzuri ili kutunza afya zao
waishi kwa muda mrefu. Ni vyema kupunguza pembe zao kila mara, wangalau kila
baada ya wiki 4 hadi 8. Pembe zao zinatakiwa kupunguzwa ili zifanane kama za
mbuzi watoto.
Kinga ya magonjwa kama pepopunda na
aina nyingine kama kifua ni jambo la msingi sana. Wasiliana na ofisa mifugo wa
eneo lako ili akueleze ni kinga gani ambao mbuzi wako wanahitaji kupatiwa na
kwa wakati gani.
Baadhi ya wafugaji wanawakinga mbuzi
wao kwa magonjwa mbalimbali kwa kuwapeleka ama kuwaita maofisa mifugo na
wengine huwaogesha kwenye Dip ili kupambana na kupe na wadudu wengine wa ngozi.
Tiba ya minyoo inatakiwa kutolewa
kila mara katika mwaka. Ofisa mifugo wa eneo lako anaweza kushauri kuhusu tiba
ya ziada kama selenium, na kupendekeza kinga na tiba ya minyoo katika ratiba
inayoeleweka kulingana na kiwango cha mifugo uliyonayo pamoja na eneo ulilopo.
Wengi huwa wanawafananisha mbuzi aina
ya Nigerian Dwarfs na African Pygmy. Hata hivyo, mbuzi hao wako tofauti ingawa
wote asili yao ni moja. Pygmy ni wafupi lakini wana mifupa mizito wakati Dwarf
warefu kidogo na miili iliyorefuka katika maumbo kama ya mbuzi wengine wa
maziwa, ingawa yao ni madogo zaidi.
Utajiri wa rangi ndiyo sababu
inayowafanya mbuzi jamii ya Nigerian Dwarf wawe maarufu. Huwezi kujua watoto
watakaozaliwa wanaweza kuwa na rangi gani mpaka watakapozaliwa; n ahata wakati
huo huwezi kuwa na uhakika kwa sababu mara nyingi rangi zao hubadilika. Rangi
za msingi ni nyeusi, chocolate na dhahabu na wakati mwingine rangi hizo
zinaweza kuwa mchanganyiko, bila kusahahu rangi nyeupe. Wengi rangi ya macho yao
ni ya udongo, lakini hivi sana wengi wana macho ya bluu na ndio wamekuwa
maarufu zaidi duniani.
Bei ya mbuzi hawa inategemea na eneo
ulilopo, lakini unaweza kuwasiliana na maofisa mifugo wa eneo lako ambao
watakuelekeza na kukushauri vyema.
Ikiwa una maoni au ushauri, usisite
kunipigia au kunitumia ujumbe wa simu au whatsapp kupitia namba 0656 331974 au
nitumie barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.
Comments
Post a Comment