Featured Post

TBN YALAANI VYOMBO VYA HABARI KUIBA KAZI ZA BLOGGERS


TAARIFA YA TBN KWA UMMA

Chama cha Wamiliki/Waendeshaji wa Mitandao ya Kijamii nchini 'Tanzania Bloggers Network' (TBN) kinasikitishwa na kulaani vitendo vya baadhi ya Vyombo vya Habari kutumia kazi za wanachama wake (picha, video, habari) bila idhini na bila kutoa maelezo stahiki ya vyanzo vya kazi hizo.

Mfano mmoja ni Gazeti la kila siku la Majira, toleo namba 8217 la Alhamisi Julai 7, 2016 ambalo bila aibu lilichukua picha katika Mtandao wa Michuzi Blog ina kuitumia pamoja na malezo yake bila ridhaa wala kutoa  kueleza chanzo cha hiyo picha.

Vile vile Wahariri wa Majira kwa makusudi waliondoa alama maalum ya kumbukumbu iliyowekwa katika picha hiyo (watermark-logo) na kuichapisha katika ukurasa wa mbele wa gazeti hilo, bila kutaja chanzo chake, jambo ambalo ni ukiukwaji wa Sheria na kinyume na taaluma ya habari.

Kitendo hicho ambacho pia kimekuwa kikifanywa na baadhi ya magazeti hapa nchini kimeonesha dhahiri ni jinsi gani baadhi ya vyombo vyenye tabia hiyo visivyothamini kazi za ‘bloggers’ na mchango wake kwenye tasnia nzima, huku wakiendelea kulea waandishi na wapiga picha wavivu na wazembe wanaotumia blogs kama njia ya mkato kupata material.

TBN inatambua wazi si vibaya vyombo vya habari kutegemeana/kushirikiana kwa kutumia kazi za chombo kingine lakini ni vema chombo kinachotumia kazi ya mtu mwingine kumtambua kwa kumtaja katika kazi hiyo ama kukubaliana na chombo husika kabla ya kufanya hivyo.

Chama cha Wamiliki/Waendeshaji wa Mitandao ya Kijamii nchini hakitafumba macho kuona kazi za wanachama wake zikitumiwa na vyombo vingine vya habari bila utaratibu na wala makubaliano ya kabla kwa wahusika. 

Imetolewa na:-
Kamati ya Uongozi TBN Taifa,
Tarehe: 11/07/2016,
Dar es Salaam.

Comments