- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
Mbuzi wa maziwa wanatoa maziwa,
lakini baada ya kuzaa. Hii maana yake ni kwamba lazima uwapandishe (breeding),
hivyo unahitaji kuwa na beberu au kwa Kiingereza buck.
Kama unazingatia ufugaji bora wa mbuzi, hakika kipengele hiki ni muhimu sana kwako,
vinginevyo itakuletea changamoto kubwa. Kuwalisha, kuwanyweshwa na kuwatibu tu
hakusaidii ikiwa utashindwa kuwaangalia katika masuala haya muhimu ya kuanzia
kuwapandisha, kuwazalisha na kuwatunza watoto wanapozaliwa.
Wafugaji wachache wanaoanza
ujasiriamali hushauriwa kutafuta beberu kwa sababu ya kuboresha uzao, kupunguza
gharama, na kuweka harufu ya beberu zizini.
Lakini ni rahisi kujua wapi
anapatikana beberu na kumsafirisha mbuzi wako jike wakati anapokuwa katika joto
tayari kwa kupandwa (heat period).
Mbuzi jike anaweza kupandishwa wakati
anapofikisha uzito wa kilogramu 39 hadi 40, hususan anapokuwa amefikisha umri
wa miezi tisa ambao ndio umri bora kumpandisha.
Mbuzi majike ni wepesi kushika mimba
wanapokuwa katika kilele cha joto ndani ya siku 2-3 kila baada ya siku 18-23,
hususan wakati wa masika au kipupwe. Wakati mwingine ni kati ya Septemba na
Januari kutegemeana na mazingira na hali ya hewa.
Dalili ambazo ni muhimu kuziangalia
ni pamoja na kuchezesha sana mkia, anakuwa hajatulia, anaweza kuwakimbiza
wenzake au wenzake wakamkimbiza, sehemu za uzazi kuvimba kidogo na wakati
mwingine kutoa majimaji, na kukojoa mara kwa mara.
Ukiona hivyo nenda katafute
lilipo beberu mpeleke huyo jike. Kama beberu atampanda halafu yeye akiwa
ametulia, tambua kwamba yuko katika joto.
Weka rekodi ya tarehe, na subiri
dalili hizo za joto wiki tatu baadaye ambao ndio mzunguko wake (siku 21). Kama
usipoziona dalili hizo, tambua kwamba tayari mbuzi wako ana mimba. Halafu weka
alama kwenye rekodi zako za tarehe ukitegemea kwamba anaweza kuzaa baada ya
siku 145 au 150 tangu ulipompandisha.
Chagua
beberu bora, na kama unajua mbuzi wako jike ana matatizo, kama vile ya miguu,
basi chagua beberu ambaye ni imara.
Mbuzi mwenye
mimba anahitaji uangalizi maalum na makini. Kama ulikuwa unamkamua, jaribu
kuwacha miezi miwili kabla ya kujifungua. Kimsingi inashauriwa baada ya
kupandwa usimkamue tena, lakini inakuwa vigumu kwa mbuzi ambaye unamtegemea na
anatoa maziwa mengi. Njia mbadala ni kupunguza kumpa chakula cha nafaka. Katika
mazingira mengi, mbuzi anapokuwa na mimba hupunguza utoaji wa maziwa na
inafikia mahali unaona hakuna haja ya kumkamua kwa sababu maziwa ni kidogo.
Hapo sasa
unapaswa kumpa chakula cha nyuzi nyuzi ambacho kina kiasi kidogo cha protini
hasa katika miezi mitatu ya kwanza ili kuruhusu watoto wakue tumboni,
vinginevyo atanenepeana na vitoto vitakosa afya na kukua taratibu. Theluthi
mbili ya ukuaji wa watoto tumboni huwa ni katika wiki nane za mwisho. Katika kipindi
hicho chakula chake kiongoezwe na kiboreshwe, lakini bila kuweka protini
nyingi, ili ajenge mwili pamoja na kusaidia watoto wajijenge. Vitamin na
madini, hususan iodine, kalsiumu na vitamin A na D ni muhimu sana.
Kuzaa
Siku chache kabla ya kuzaa, muweke
mbuzi huyo kwenye banda safi la peke yake ukimuwekea matandazo safi ya kulalia,
maji, na nyasi nzuri. Usije ukashangaa wakati utakapoamka asubuhi na kukuta
mbuzi ana watoto wawili au watatu, hata kama hakuonyesha dalili za utungu.
Ni jambo
muhimu sana kupanga kuwa karibu na mbuzi wako anapozaa – lakini kwanza lazima
uanze kuwa karibu naye kuanzia siku ya 140 baada ya kupandwa. Kuna dalili
nyingi za kuangalia. Unaweza kuwagusa watoto kwa mkono wakati mbuzi anapokuwa
ametulia na wanaweza kuwa katika kila upande wat umbo. Kama utafanya hivyo mara
mbili kwa siku utagundua kwamba ni wakati gani huwagusi. Basi hapo tambua
kwamba mbuzi huyo anaweza kuzaa ndani ya saa 12 zijazo. Wakati mtoto wa kwanza
anapokaribia kuzaliwa, mbuzi atalazimika kulala ubavu. Kadiri muda
unavyokaribia, mbuzi ataanza kulalamika. Anaweza kutoa ute wa manjano.
Wakati anapokuwa na utungu anaweza
kukwangua sakafu na kulala na kusimama tena mara nyingi huku akihangaika. Kama
atakuwa na utungu kwa zaidi ya saa mbili au anaonekana kuwa na matatizo, mwite
mtu mwenye uzoefu na mifugo hata jirani, na kama wewe mwenyewe ni mzoefu, basi
ni jambo jema. Njia nzuri ya kujifunza kukabiliana na nyakati hizo ngumu ni
kujifunza kwa kumwangalia mtu mzoefu anavyofanya.
Uzazi wa
kawaida unaweza kudumu kwa saa nne au zaidi, lakini ukiona kwamba kuna matatizo
ya uzazi kwa mbuzi – kama kutokeza mguu mmoja ukiwa umejikunja, au kitovu
kikiwa kimejiviringa – na unataka kumsaidia mbuzi, hakikisha unanawa mikono
yako kwa sabuni yenye dawa (germicidal soap) na kupaka mikono mafuta yenye
madini, kabla ya kuingiza mikono yako kumsaidia.
Kwa bahati
nzuri, mambo kama haya yanaweza yasitokee mara ya kwanza unapokuwa umejianza
ufugaji wako, lakini ikiwa yatatokea wala usishangae. Ingiza mikono yako,
jaribu kuangalia mikono ya mbele na kichwa halafu saidi kuvivuta taratibu
ukisubiri mbuzi asukume kwanza.
Ninazungumza
haya kutokana na uzoefu wangu katika ufugaji, kwa sababu nimekwishawahi
kusaidia hata ng’ombe kuzaa. Kama una uzoefu na ujasiri ni jambo
linalowezekana.
Mara ya
kwanza haikuwa rahisi kwangu. Nakumbuka ilitokea mwaka 1978 wakati nikiwa
mdogo. Nilikuwa nachunga kundi la mbuzi, kondoo na ndama. Mbuzi mmoja mwenye
mimba akapata uchungu. Sikujua nifanye nini kwa sababu tayari mbuzi wengine –
kama walivyo wasumbufu – walikuwa wakiendelea kusonga mbele porini wakichunga.
Kumwacha
huyu anayetaka kuzaa sikuona jambo la busara, ikabidi nimsubiri. Kwa kuwa sikuwa
na uzoefu, huku nikifikiria kwamba mbuzi wengine wamekwishasonga mbele,
nikaanza kulia peke yangu.
Baadaye
nikaona ujinga kwa sababu kilio changu kisingeleta maana yoyote. Pamoja na
kutokuwa na uzoefu, nikamsogelea mbuzi yule aliyelala akihangaika. Silaha zangu
za jadi nikaziweka chini. Kitoto cha mbuzi kilikuwa kinagoma kutoka kwa sababu
mguu mmoja ulitangulia na mwingine ulikuwa umejikunja. Nikaingiza mkono na kumshika
taratibu na kufanikiwa kuuvuta mguu, hatimaye kitoto kikatoka salama.
Nikasubiria kitoto cha pili, nacho kikatoka salama baada ya kumsaidia mbuzi
yule kwa mara nyingine.
Baada ya
kuvisafisha na kuviacha vinyonye kidogo, nikavibeba na kuondoka huku yule mama
yao akipiga kelele. Kumwongoza haikuwa rahisi kwa sababu anawataka watoto wake,
hivyo nikaamua kutangulia mimi na yeye akanifuata kueleka waliko mbuzi wengine
ambapo nilimpatia watoto wake akawanyonyesha. Kwa vile watoto wale hawakuwa na
nguvu na uwezo wa kutembea, kazi yangu ya kuchunga ikawa ngumu kwa sababu muda
wote nililazimika kuwabeba. Na niliwabeba vivyo hivyo hadi kwenye boma muda wa
kurudi ulipofika.
Nakumbuka
baba yangu alinizawadia. Akaenda kuninunulia kaptura ya khaki mnadani! Zawadi
kubwa sana enzi hizo katika mazingira yetu ya kushinda ukiwa umevaa lubega tu!
Baada ya hapo sikuwa na hofu tena, na niliwasaidia hata ng’ombe walipokuwa
katika matatizo ya kuzaa.
Hatua muhimu baada ya kuzaa ni
kuondoa utando kwa watoto ili kuwafanya wapate hewa (mama yao anaweza kufanya
hivyo kwa kuwalamba kama wewe haupo), wawekee iodine kwenye vitovu ili kuzuia
maambukizi hasa ya bakteria na uwakaushe watoto.
Taratibu jaribu kukamua maziwa kutoka
kila titi ili kujiridhisha kwamba linafanya kazi na siyo limeziba.
Safisha matandazo ya kulalia na weka
mengine safi. Hakikisha kwamba watoto wanapata maziwa ya kwanza (colostrum),
ikibidi yakamue na uwanyweshe watoto kwa kutumia chupa maalum yenye nyonyo kama
zile za watoto. Maziwa hayo mazito ya njano yanayotoka katika siku za kwanza ni
muhimu kwa ukuaji wa watoto.
Mbuzi
anayenyonyesha huhitaji chakula kingi zaidi ili kukidhi mahitaji ya mwili na
kuzalisha maziwa kwa ajili ya watoto. Pamoja na nyasi, mikunde na majani ya
miti, malisho kilo 1.8 – 2.5 kwa siku ni muhimu apewe chakula cha nyongeza kilo
0.3 – 0.8 kwa kila lita ya maziwa inayoongezeka baada ya lita 2 na maji safi,
salama na ya kutosha wakati wote.
Utunzaji
wa watoto
Kwa kawaida,
utunzaji wa watoto wa mbuzi huanza mara tu baada ya kuzaliwa. Kuna nadharia
nyingi za kuwalea watoto wa mbuzi, lakini njia ya asili ni kuwaacha na mama
yao. Hiyo haiwezi kuwa namna bora kama unafuga mbuzi kwa ajili ya maziwa.
Lakini kama
nilivyosema hapo awali, mfugaji ahakikishe kitoto cha mbuzi kinapata maziwa ya
mwanzo (manghanda) ndani ya saa 24 tangu kuzaliwa na kwa muda wa siku 3. Kama
kinanyweshwa maziwa, kipewe lita 0.7- 0.9 kwa siku. Maziwa haya, ni muhimu
kwani yana viinilishe na kinga dhidi ya magonjwa.
Ikitokea mama hatoi
maziwa au amekufa, inashauriwa kutengeneza maziwa mbadala ya aina hiyo au kama
kuna mbuzi mwingine aliyezaa anaweza kusaidia kukinyonyesha kitoto hicho.
Hata hivyo,
wafugaji wengi wa mbuzi wa maziwa huwaondoa watoto kwa mama yao mapema baada ya
kuzaliwa na kuwapatia maziwa kwa kuwakamulia.
Watoto hao lazima walazwe kwenye
sehemu safi, kavu na salama, na ikiwezekana wawe mbali na mama yao. Kuwanywesha
maziwa badala ya kunyonya kunahitaji ustahimilivu na muda kwa sababu lazima
uwafundishe watoto namna ya kunywa maziwa hayo.
Wafugaji wengi wanawanywesha watoto
maziwa ya vugu vugu kulingana na joto la mama, mara tatu au nne kwa siku.
Wiki 2 baada ya kuzaliwa, pamoja na maziwa, kianze
kupewa vyakula vingine kama nyasi laini na chakula cha ziada ili kusaidia kukua
kwa tumbo. Uwaachishe watoto kwa kuangalia uzito, siyo umri, na ni
lazima wanapokuwa wamefikia uzito wa kilogramu 9, bila kusahau
kuvipatia kinga na tiba ya magonjwa kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.
Lakini
hakikisha kwamba kitoto kinapewa maji wakati wote na vyombo vinavyotumika
kulishia vinakuwa safi muda wote.
Comments
Post a Comment