Featured Post

MBUZI WA MAZIWA JAMII YA SABLE




Na Daniel Mbega
Mbuzi jamii ya Sable wanatokana na mbuzi jamii ya Saanen ambao asili yao ni Uswisi. Wanafanana sana na Saanen hata kwa rangi.
Kama ilivyo kwa mbuzi jamii ya Saanen, Sable wanaweza kuwa na uzito wa kilogramu 65 kwa jike na dume linaweza kufikisha kilogramu 77. Jike la Sable lina uwezo wa kutoa lita 862 za maziwa kwa mwaka ambayo yana wastani wa asilimia 3.5 ya mafuta.

Sable ni matokeo ya mchanganyiko wa jeni. Ikiwa mtoto atakuwa na jeni zenye nguvu za rangi nyeupe, basi mbuzi huyo atakuwa Saanen na siyo Sable. Mlinganisho wa rangi unachanganya na inaonekana kwamba kama mbuzi mtoto atakuwa na jeni mbili zenye nguvu, moja kutoka kwa kila mzazi, lazima ngozi yake itakuwa ya rangi mchanganyiko. Kwa kuwa jeni za rangi zilikuja na mbuzi wa asili wa Saanen kutoka Uswisi, basi mbuzi jamii ya Sable wataendelea kuzaliwa kwa kadiri Saanen wanavyofugwa.
Majike wa Sable ni wazazi wazuri na wazalishaji wazuri wa maziwa. Kama ilivyo kwa Saanen, mbuzi jamii ya Sable wana maumbile ya wastani na makubwa na kama nilivyoeleza hapo mwanzo, jike anaweza kufikisha kilogramu 65 akiwa na minofu ya kutosha. Kimo chake kutoka mabegani ni inchi 30 kwa jike na 32 kwa beberu. Ukimtazama tu utamuona mrefu, mkubwa na amechangamka huku mwili wake ukiwa mkubwa, mpana na mrefu. Umbile lake kwa ujumla ni kama mstatili.
Sababu mojawapo ya kufuga mbuzi jamii ya Sable ni utajiri wake wa rangi. Saanen weupe, wenye ngozi laini, hawawezi kuishi kwenye mazingira ya joto na jua kali. Ngozi yao laini inawafanya wawe hatarini kupata ugonjwa wa saratani ya ngozi.
Wafugaji wengi kutoka nchi zenye mazingira ya kitropiki huwa hawapendi kuwanunua hao kwa sababu wanatambua tatizo hilo licha ya uwezo wa Saanen katika uzalishaji wa maziwa pamoja na ukubwa wao wa umbo na upole wao. Lakini mbuzi jamii ya Sable hawana tatizo hilo. Ngozi zao nyeusi kulinganisha na zile za Saanen zinawafanya wasiwe hatarini kupata ugonjwa wa saratani ya ngozi lakini wakati huo huo wakiwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha maziwa kama wa Saanen.
Ukitaka kuwafuga, mtafute ofisa mifugo wa eneo lako atakupatia maelezo na namna ya kuwapata.

Ikiwa una maoni au ushauri, usisite kunipigia au kunitumia ujumbe wa simu au whatsapp kupitia namba 0656 331974 au nitumie barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.




Comments