Featured Post

MBUZI AINA YA LAMANCHA NI WAPOLE SANA NA HUTOA LITA 862 ZA MAZIWA KWA MWAKA!





Mbuzi jamii ya LaMancha

Na Daniel Mbega
Mbuzi wa maziwa jamii ya LaMancha wanafahamika kwamba ndio mbuzi rafiki zaidi kati ya jamii zote za mbuzi wa maziwa na wanapatikana katika rangi zote ambazo unaweza kuziona kwa mbuzi. LaMancha ni mbuzi ambao wanatambulika sana kutokana na kuwa na masikio mafupi kana kwamba yamekatwa, ni wapole, wakimya na marafiki wa binadamu, siyo wakorofi.
Mbuzi jike mkubwa huwa na uzito wa kilogramu 59 au zaidi na beberu huwa na uzito wa zaidi ya kilogramu 73. Mbuzi jamii ya LaMancha hutoa lita 862 za maziwa kwa mwaka yenye wastani wa siagi asilimia 3.9.
Mbuzi jamii ya LaMancha ni mzao chotara ambao ulipatikana katika miaka ya 1930 huko Oregon, Marekani wakati Bi. Eula F. Frey alipowachukua mbuzi majike waliokuwa na masikio mafupi waliodhaniwa kuwa na asili ya Hispania na kuwapandisha na mabeberu ya Uswisi na Nubia.


Mbuzi jamii hii wanatoa maziwa bora na wanaweza kustahimili mazingira yoyote magumu na bado wakaendelea kutoa maziwa ya kutosha.
Uso wa mbuzi jamii ya LaMancha ni mwembamba, huku masikio yao mafupi yakiwa alama ya kudumu inayowatambulisha. Pua ya Kirumi ambayo ni sifa ya mbuzi wa Nubia, na wanaweza kuwa na rangi tofauti, wakiwemo wenye mabaka na michirizi. Manyoya yao ni mafupi na laini.
Mbuzi hawa wanayo masikio; mfereji na muundo mwingine wa ndani wa masikio upo kama kawaida. Ni masikio yanayotokeza nje ambayo yanaonekana mafupi mno. Kwa hiyo kama unataka kuwawekea alama (tags) huwezi kuweka kwenye masikio bali utaweka mikiani. Tags ni alama za utambulisho kwa mbuzi ikiwa unatunza rekodi zao na ni muhimu kuwa nazo.
Masikio ya LaMancha yapo ya aina mbili kubwa: kuna yale mafupia kabisa (Gopher ear) ambayo urefu wake ni kama inchi moja (sentimeta 2.5) kana kwamba yamekatwa. Mara nyingi mabeberu ndio wenye masikio ya aina hiyo. Pia kuna wale wenye masikio marefu kidogo (Elf ear) ambayo yana urefu wa inchi 2 na yamechongoka, yaani yana ncha. Majike ndio ambao huwa na masikio ya aina hii.
Ukiwasiliana na ofisa wako wa mifugo aliye karibu anaweza kukushauri wapi pa kuwapata mbuzi hao kama unataka kuwafuga.

Ikiwa una maoni au ushauri, usisite kunipigia au kunitumia ujumbe wa simu au whatsapp kupitia namba 0656 331974 au nitumie barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.


Comments