Featured Post

MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA SULUHU HASSAN AZINDUA MRADI WA GREEN VOICES TANZANIA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) akiwa na kinyago cha mwanamke baada ya kuzindua mradi wa Green Voices Tanzania. Katikati ni mfadhili wa mradi huo, Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza Fernandes de la Vega, na kushoto ni Mkuu wa Wilaya Ilala, Sophia Mjema.

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itahakikisha mradi wa kutunza mazingira nchini wa Green Voices unakuwa endelevu na kwamba ni vyema akinamama wote nchini kushirikishwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo wa Green Voices Tanzania katika ukumbi wa Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, Mhe. Samia amesema kipindi cha miezi mitatu ambacho mradi huo umeanza kutekelezwa nchini kimeonyesha mafanikio makubwa na kutia hamasa kwa jamii na serikali kuona umuhimu wa kuuendeleza licha ya kwamba ufadhili wa mradi huo ulikuwa wa mwaka mmoja tu.
Mradi huo wa Green Voices umefadhiliwa na taasisi ya Women for Africa Foundation inayoongozwa na makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza Fernandes de la Vega Sanz (67).
“Mimi kama kiranja wa mazingira, ninaahidi kwamba serikali itahakikisha mradi huu unakuwa endelevu, usiishie hapa tu, na tunataka kila mkoa na hata wilaya zote nchini wanawake washiriki kwa sababu wao ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa jamii huku mazingira yakiwa yanaharibiwa,” alisema.
“Tumeuzindua mradi huu kuashiria kwamba kazi imeanza, lakini ni lazima tuhakikishe unakuwa endelevu na usiishie hapa,” aliongeza.
Makamu wa Rais amesema kwamba amefarijika na ongezeko la wanawake wanaojihusisha na miradi ya utunzaji mazingira katika kipindi kifupi tu tangu wapatiwe mafunzo nchini Hispania.
“Kutoka wanawake 15 waliopatiwa mafunzo miezi mitatu iliyopita, leo nimefarijika kusikia kwamba tayari hawa wamekwishawafundisha wanawake wengine 250, haya ni mafanikio makubwa na lazima serikali iyaunge mkono,” alisema.
 Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania Mama Maria Tereza, wakisikiliza maelezo ya ukaushaji wa mboga mboga kutoka kwa Esther Muffui wa Morogoro.
 Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania Mama Maria Tereza, wakisikiliza maelezo ya ufugaji nyuki kutoka kwa akinamama wa Dakawa, Morogoro.
Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania Mama Maria Tereza, wakisikiliza maelezo kutoka kwa wanahabari wanawake wanaofanya mradi wa Green Voices Tanzania.

Awali, Mratibu wa mradi wa Green Voices Tanzania, Secelela Balisidya, alisema kwamba, baada ya kurejea kutoka Hispania, wanawake 10 wanaofanya miradi mbalimbali inayolenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi katika mikoa sita ya Tanzania Bara, wameweza kuwafundisha wenzao wengine 250 na kasi yaw engine kujifunza inaendelea.
Alisema lengo la Green Voices ni kuhakikisha wanapanua uelewa kwa wanawake na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, lakini wakati huo huo kuona kwamba wanawake wanafanya miradi inayoendana na dhima hiyo pamoja na kuwaongezea kipato.
Naye Balozi Getrude Mongella, amesema kwamba mradi wa Green Voices na miradi mingine ambayo inashughulikiwa katika Bara la Afrika inaonyesha ushirikiano wa kimataifa siyo tu kwa serikali bali kwa wanawake.
Amesema ni vyema ushirikiano wa maendeleo usiachiwe tu kwa serikali, bali unaweza ukafanywa hata kwa watu binafsi.
 Bidhaa mbalimbali zinazotokana na mazao ya muhogo.

Kuhusiana na ushirikishwaji wa wanawake, Balozi Mongella ambaye ndiye Mwafrika wa kwanza kuwa mwenyekiti wa Mkutano wa Dunia wa Wanawake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995, amesema jitihada za kwanza zilianza katika Mkutano wa Rio de Janeiro, Brazil mwaka 1992 kuhusu mazingira na mkutano wa maendeleo wa Cairo, Misri 1993 pamoja na ule wa Beijing, ambapo maazimio yaliyofikiwa ni kuhakikisha wanawake wanahusishwa katika maendeleo.
“Jambo muhimu ni kwamba, miradi hii yote inawahusisha wanawake, na kwa hakika wanawake ndio wenye nafasi kubwa ya kuleta maendeleo,” alisema.
Naye Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza Fernandes de la Vega, amewapongeza wanawake hao wa Tanzania kwa jitihada kubwa walizozionyesha kuhusu mradi huo na kuahidi kuendelea kuwasaidia.
Alisema kwamba, mradi huo ni wa majaribio, lakini umeweza kuleta matumaini makubwa tofauti na walivyofikiria awali.
“Julai mwaka jana wakati nilipokuja hapa Tanzania ndipo nilipata wazo la kuleta mradi huu kwa majaribio, lakini inatia imani kubwa kuona wazo lile tulilotaka kulijaribu leo hii limepata mwitikio mkubwa namna hii,” alisema Maria Tereza, ambaye ndye Rais wa taasisi ya Women for Africa Foundation.
Mama Maria Tereza alikuwa makamu wa rais wa Hispania kati ya Aprili 18, 2004 hadi Oktoba 20, 2010, na ndiye alikuwa msemaji wa serikali ya Waziri Mkuu Jose Luis Rodriguez Zapatero. Yeye ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo katika historia ya Hispania.



Comments