- Get link
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- Other Apps
Anna Salado, Mkurugenzi wa taasisi ya Women for Africa Foundation kutoka Hispania, akiwa na uyoga aliouvuna.
“SIJAWAHI kuvuna uyoga katika
maisha yangu, achilia mbali kushuhudia namna unavyolimwa,” anasema Anna Salado,
Mkurugenzi wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika (WAF) kutoka Hispania, wakati
akikwanyua kikonyo cha uyoga katika shamba la akinamama wa kikundi cha Tunza
Women Group, Bunju jijini Dar es Salaam.
Anaongeza: “Kwa hakika ninyi
wanawake mmefanya jambo kubwa na muhimu katika jamii, kwa sababu mbali ya
kufanikiwa kulisha familia zenu, lakini sasa mtaweza kuongeza kipato kwa
kuwauzia wengine zao hili.”
Akiwa ameongozana na maofisa
wengine wa taasisi hiyo Alicia ambaye ni mratibu na Noelia ambaye ni mkurugenzi
wa miradi, Anna Salado anasema kwamba, wamehamasika sana na kilimo hicho na
katika kuunga mkono juhudi za akinamama hao watawasaidia kutatua changamoto
zinazowakabili pamoja na kuwawezesha kupanua mradi wao.
Mradi huo wa kilimo cha uyoga
ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mama wa Green Voices nchini Tanzania
unaofadhiliwa na taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika, ambayo rais wake ni
Mama Maria Teresa Fernandez de la Vega Sanz ambaye ni Makamu wa Rais mstaafu wa
Hispania.
Anna na wenzake wamekuwa
wakitembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Green Voices nchini
Tanzania tangu mradi huo ulipozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Julai 11, 2016 katika Hoteli ya
Serena jijini Dar es Salaam.
Uyoga ukiwa umeota vizuri ndani ya banda.
Wakati wa ziara yao kwenye
mradi wa kilimo cha uyoga, viongozi hao walioambatana na Mratibu wa Green
Voices Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, walijifunza mambo mbalimbali kuanzia
utaarishaji wa shamba, upandaji, uvunaji pamoja na namna ya kufungasha huku pia
wakielekezwa mapishi ya uyoga.
“Tunakunywa supu kwenye
mahoteli, tunauona tu kwenye picha, lakini leo tumeweza kuuona namna
unavyolimwa, tena tumeonja mapishi mengine tofauti,” alisema Anna Salado baada
ya kula uyoga ulioungwa kwa nazi.
Mratibu wa mradi wa Green
Voices kutoka Hispania, Bi. Alicia akizungumza na washiriki wa mradi huo,
alisema kwamba mradi huo ulikuwa wa majaribio, lakini sasa umewahamasisha na
wako tayari kusaidia awamu ya pili ili kuwawezesha wanawake wengi wajikite
kwenye kilimo hicho cha uyoga.
“Tumefarijika sana, kwa sababu
ni kipindi kifupi tu tangu tulipowapa mafunzo wanawake 15 kule Madrid, lakini
leo hii mmeweza kufanya mambo makubwa kama haya, hakika tuko nanyi bega kwa
bega,” alisema Alicia.
Mshiriki kiongozi wa mradi wa
kilimo cha uyoga, Magdalena Bukuku, alisema kwamba tangu walipoanza kilimo
hicho mwezi Machi, tayari wamekwishaona faida yake baada ya kuvuna na kuuza
sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam.
Magdalena, ambaye yeyé na
wanawake wengine 14 walipatiwa mafunzo Hispania mapema mwaka huu, amesema
kwamba kutokana na wingi wa akinamama waliojitokeza, amewagawa katika makundi
mawili, ambapo kimoja kipo Mtaa wa Kilungule, Bunju na kingine kipo Boko, vyote
vikiwa na wanachama 10 kila kimoja.
Hata hivyo, amesema kuwagawa tu
hakukuwazuia wanawake wengine kwenda kujifunza, kwani tayari wanajamii katika
maeneo hayo wamekuwa wakimiminika kujifunza namna ya kuanzisha mashamba ya
uyoga majumbani mwao.
“Mpaka sasa
nimekwishawafundisha wanawake wengine zaidi ya 50, wengine wanatoka Zanzibar,
Kibaha na Bagamoyo,” alisema.
Mwenyekiti wa kikundi cha Tunza
cha Bunju, Sophia Chove, anasema hivi sasa wanafikiria kuongeza shamba jingine
la uyoga, ingawa changamoto ya mtaji ndiyo inayowapa shida.
Anasema ili kuweza kupata faida
ni muhimu kuongeza shamba hasa ikizingatiwa kwamba mahitaji ya uyoga
yameongezeka katika jamii.
“Wateja ni wengi sana kuliko
tunachozalisha, hivyo tunaona ni vyema tukaongeza banda jingine, lakini
changamoto hapa ni mtaji, tukiwezeshwa tunaweza,” anasema.
Anasema kwamba, tayari wamepata
wateja wa maduka makubwa ya bidhaa (super markets) pamoja na jamii
inayowazunguka, mahitaji ambayo ni makubwa kuliko uwezo wa kuzalisha.
“Uyoga una faida kubwa, fikiria
robo kilo ya uyoga inauzwa Shs. 2,500 wakati kilo moja ni Shs. 10,000,”
anaongeza Sophia.
Bi. Sophia Chove, Mwenyekiti wa kikundi cha Tunza Women cha Bunju jijini Dar es Salaam, akiwaelekeza wageni namna ya kuandaa mahitaji mbalimbali ya kilimo cha uyoga.
Mratibu wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia, akizungumza na wanawake wakulima wa uyoga wa Bunju na Boko (hawapo pichani).
Mhazini wa kikundi hicho ambaye
pia ndiye mwalimu wa ukulima wa uyoga na Ofisa Kilimo Msaidizi Mwandamizi wa
Manispaa ya Kinondoni, Esther Chiombola, anasema kwamba kila wiki wamekuwa
wakiwafundisha akinamama kati ya watano hadi 10 kutoka maeneo mbalimbali.
“Hapa pamekuwa kama kituo cha
mafunzo, wanawake wengi wamehamasika na tunawafundisha namna ya kuanzisha
kilimo hiki ambacho ni rafiki wa mazingira na kina tija kubwa kwa uchumi,”
anasema Mama Chiombola.
Anaongeza: “Ni
mradi unaotumia gharama kidogo huku mavuno yake yakiwa endelevu, hapa Bunju tayari
akinamama wameanza kuvuna.”
Miradi mingine ya Green Voices inatekelezwa katika mikoa
ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Mwanza, Kigoma na Kilimanjaro ambayo yote
inaendana na mkakati wa mapambano dhidi
ya mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, miradi hiyo ya Green
Voices nchini inalenga pia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 pamoja na
Malengo Endelevu ya Dunia katika kuondoa umaskini, kuongeza ajira, kuwawezesha
wanawake kiuchumi, kuhakikisha usalama wa chakula pamoja na kupambana na
uharibifu wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mambo ya msosi, na kuna rosti la uyoga hapo.
Noellia (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa mwakilishi wa wakulima wa uyoga wa Bunju na Boko jijini Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment