Featured Post

HAWA NDIO MBUZI JAMII YA TOGGENBURG



MBUZI wa jamii ya Toggenburg, au Togg kama wanavyoitwa kwa kifupi, ni wa kundi la jamii ya mbuzi wanaofugwa kwa ajiliya maziwa ambao ni wapole na marafiki. Mbuzi hawa utawatambua kwa kuwa na masikio meupe, miraba myeupe usoni na miraba myeupe miguuni huku ngozi yao ikiwa ya rangi ya udongo.

Mbuzi jike mkubwa anaweza kuwa na uzito wa kilogramu 55 ama zaidi na beberu ana uzito wa kilogramu 68 ama zaidi.
Jike la Toggenburg lina uwezo wa kutoa lita 885 za maziwa kwa mwaka yenye wastani wa asilimia 3.2 ya mafuta.
Toggenburg wamepewa jina hilo kutokana na eneo la Bonde la Obertoggenburg huko Canton of St. Gallen nchini Uswisi ambako ndiko asili yao. Inaelezwa kwamba hawa ndio jamii kongwe zaidi ya mbuzi wa maziwa.
Mbuzi hawa wana umbile la kati, wakakamavu, na wanavutia kwa muonekano. Umbile lao ni dogo kulinganisha na jamii nyingine ya mbuzi kutoka Alpine. Manyoya yao ni mafuti ama marefu kidogo, laini, mazuri na yamelala.
Inaelezwa kwamba, kati ya jamii 300 ya mbuzi zilizoko duniani, Toggenburg ndio mbuzi waongwe zaidi ambapo walisajiliwa rasmi katika miaka ya 1600.
Mbuzi wa Toggenburg wakipandishwa na mbuzi wengine wa nyama kama Kalahari Red au Boer (Kaburu) wanaweza kuzaa chotara mzuri ambaye anafaa kwa nyama na maziwa.
Ukiwa unawahitaji mbuzi wa jamii hii, mtafute ofisa mifugo wa eneo lako ambaye atakupa ushauri wa namna ya kuwapata.

Baada ya kuzijua jamii bora za mbuzi wa maziwa, sasa tunaichambua jamii moja baada ya nyingine ili kama imetokea unataka kuwafuga, ama unawafuga tayari, uweze kuwaelewa tabia na uwezo wao pamoja na ustahimilivu wa magonjwa.
Ikiwa una maoni au ushauri, usisite kunipigia au kunitumia ujumbe wa simu au whatsapp kupitia namba 0656 331974 au nitumie barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.

Comments