- Get link
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- Other Apps
Ofisa Nyuki wa Wilaya ya Mvomero, Oscar
Kunambi (aliyechuchumaa kushoto) akisaidiana na mwanakikundi cha Dakawa Green
Voices, Neema Obeid, kuweka vizuri mzinga.
Mwanahabari Judica Losai (wa pili kushoto)
akimuuliza maswali Ofisa Nyuki wa Wilaya ya Mvomero, Oscar Kunambi, wakati
wakiwa kwenye eneo la ufugaji wa nyuki.
Baadhi ya mizinga ya akinamama wa Dakawa
Green Voices ikionekana kuning’inia kwenye miti. Mizinga hii tayari ina nyuki.
Akinamama wa Dakawa Green Voices wakisikiliza
maelezo kutoka kwa mtaalam wa ufugaji nyuki, Oscar Kunambi, ambaye hayupo
pichani.
Ofisa nyuki wa Wilaya ya Mvomero,, Oscar Kunambi, akiwaelekeza akinamama wa Dakawa Green Voices namna ya ufugaji bora wa nyuki.
TAKRIBAN kilometa 10 kutoka Kijiji cha Dakawa
kuna kitongoji cha Magogo kilichoko msituni kabisa ambako pia kuna mashamba ya
mpunga.
Msitu huu ambao bado ungali na miti mingi ya
asili ambayo imenusurika kucharangwa na wachoma mkaa na wanaotafuta ardhi yenye
rutuba kwa ajili ya kilimo, ndiko akinamama wapatao 30 wameamua kutundika
mizinga kwa ajili ya ufugaji wa nyuki katika shamba lenye ukubwa wa ekari nne.
Licha ya kujikwatua vilivyo, lakini wanapoingia
katika msitu huu akinamama hawa hawana mchezo kabisa, baadhi yao wanavaa mavazi
maalum ya kujikinga na nyuki na kuanza kukagua mizinga yao kama tayari nyuki
wamekwishaingia.
“Kujipamba ni jambo la kawaida, lakini tunapokuja
huku tuko kikazi zaidi,” anasema Neema Obeid huku akipenya kwenye vichaka
kuiendea mizinga ambayo iko juu ya miti mikubwa.
Akina mama hao wa kikundi cha Dakawa Green Voices
Women Group wameamua kuingia kwenye ujasiriamali wa ufugaji wa nyuki kwa
malengo makubwa mawili – kupata fedha kutokana na mazao ya nyuki pamoja na kupambana
na mabadiliko ya tabinchi.
“Misitu inateketea, watu wanaendelea kuchoma mkaa
na wengine wanafyeka miti ili wapate mashamba, lakini kwa kuanzisha ufugaji huu
wa nyuki, kamwe hatutakubali kuona yeyote akikata hata fimbo, achilia mbali
miti mikubwa,” anasema Bi. Mariam Bigambo, mshiriki kiongozi wa mradi huo.
Mariam
Bigambo ni miongoni mwa akinamama 10 waliopatiwa mafunzo nchini Hispania mapema
mwaka huu na wanatekeleza kwa vitendo mradi wa Green Voices, ambao unafadhiliwa
na taasisi inayojihusisha na maendeleo
ya wanawake wa Afrika, ijulikanayo kama Women for Africa Foundation inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa
Hispania, María Teresa Fernández de la Vega. Hapa nchini, mradi huo unasimamiwa na asasi ya
Environment Media Agenda (EMA) chini ya uratibu wa Bi. Secelela Balisidya
Akinamama wengine wanatekeleza miradi mbalimbali ya
ujasiriamali unaoendana na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika
mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro, Pwani na Mwanza.
Mama
Bigambo anasema kwamba, ufugaji huo unahitaji kutunza mazingira ili kuwawezesha
nyuki kupata chakula chao hasa nekta na maji, hivyo ni vizuri kuhakikisha
mazingira yanakuwa salama.
Aidha,
anasema kwamba, kwa kuwa Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine duniani,
inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi, ni vizuri kufanya shughuli za uchumi
zinazohakikisha kwamba mazingira yanatunzwa na wakati huo huo shughuli hizo
zikichangia kupambana na mabadiliko ya tabiachi, huku ufugaji wa nyuki ukiwa
miongoni mwa shughuli hizo.
“Bila
kutunza mazingira hata hao wanaokata mkaa na wanaotafuta mashamba watalia
baadaye kwa kuwa miti itakwisha, tutabaki na jangwa ambao halitatoa mazao tena.
Tutakufa,” anasisitiza.
Kuhusu
ufugaji huo wa nyuki, Mama Bigambo anasema kwamba, ingawa zamani ilionekana
kama shughuli za akina baba, lakini kama wanawake watafundishwa wanaweza
kuendesha ujasiriamali huo bila shida.
“Gharama
kubwa ya ufugaji wa nyuki iko mwanzoni tu – kutafuta mizinga pamoja na eneo
bora linalofaa kwa ufugaji ambalo maua na maji yanapatikana kwa urahisi, baada
ya hapo kazi yako ni kutembelea na kuangalia maendeleo.
“Nyuki
hawachungwi kama ng’ombe, mbuzi au nguruwe wala hawaangaliwi kama kuku,
hawahitaji chanjo ya ugonjwa wowote, hivyo ni rahisi kutundika mizinga yako
katika eneo husika na kuendelea na shughuli zako nyingine,” anafafanua.
Akizungumzia umuhimu na faida za nyuki, Mama
Bigambo anasema kuwa licha ya kusaidia kutunza mazingira, lakini nyuki ni
muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe hai vyote, kwani ndio wanaofanya
uchavushaji wa mimea.
Anazitaja faida za ufugaji nyuki kuwa ni asali na
nta, mazao ambayo yana faida kubwa hata katika soko la kimataifa.
Katibu wa kikundi hicho, Amina Buteta, ana
matumaini makubwa kwenye mradi huo na anasema kwamba unaweza kuwakomboa
wanawake wa Dakawa na vijiji vya jirani kwa kujipatia kipato kikubwa.
“Tunakuja huku shamba kila baada ya wiki, wakati
mwingine tunakuja kwa zamu kuangalia maendeleo, hivyo hatubanwi na ufugaji wa
nyuki na tunaendelea na shughuli zetu nyingine,” anasema.
Amina anasema kwamba, wameanza na mizinga 30,
lakini malengo yao ni kuwa na mizinga 4,000, lakini changamoto wanayokabiliana
nayo ni mtaji wa kununulia mizinga hiyo.
Inaelezwa kwamba, mzinga mmoja unauzwa Shs.
70,000, lakini kutokana na uchumi kuwa mdogo, wengi wanashindwa kupata fedha za
kununulia.
“Lakini ipo siku
tutafanikiwa tu, hakuna shida, kwa sababu tumedhamiria,” anasema.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha
Dakawa, Andrea Muhando, anasema ufugaji wa nyuki siyo tu utawakomboa kiuchumi
wanawake hao na jamii nzima kwa ujumla, lakini utasaidia kutunza mazingira
katika eneo hilo ambalo limeshindwa kuzalisha mazao vya kutosha kutokana na
mafuriko ya mara kwa mara pamoja na mvua zisizo za uhakika.
Anasema, kukosekana kwa mvua
katika misimu tarajiwa kama ilivyokuwa zamani pamoja na mafuriko makubwa
yanayosababisha maafa ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni vyema
wananchi wakaangalia miradi mingine endelevu yenye kipato lakini inayoweza
kutunza mazingira.
“Kila mwaka mvua zinashindwa
kunyesha kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa, na zinaponyesha zinakuja kwa
nguvu na kuleta madhara hata kwa mimea kama tunavyoshuhudia katika eneo hili
kila mwaka.
“Mwaka huu mafuriko
yameharibu hekta 240 za mazao mbalimbali, ukiwemo mpunga ambao umekuwa mkombozi
wa mkulima, na sasa tunategemea tu katika maeneo ya kondeni pekee,” anasema.
Kwa upande mwingine, Ofisa
Nyuki wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Oscar Kunambi, anasema kwamba
kuanzishwa kwa mradi wa akinamama hao kutachochea jamii kuingia kwenye ufugaji
wa nyuki wilayani humo badala ya kutegemea kilimo na mifugo pekee.
Anasema kwamba, soko la
asali ni kubwa nchini Tanzania, ambapo tayari kuna kiwanda kikubwa wilayani
Kibaha kinachohitaji malighafi lakini asali inayozalishwa haitoshelezi
mahitaji.
Aidha, anasema kwamba,
wilaya hiyo ina maeneo mengi yenye misitu ambayo ikitumiwa kwa ufugaji wa nyuki
inaweza kuleta faida kubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
“Unapofuga nyuki, mbali ya
kupata faida kutokana na mazao yake, lakini unasaidia kuyalinda maeneo hayo kwa
sababu hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kwenda kukata miti sehemu
ambayo kuna nyuki, kwanza usalama wake utakuwa mdogo,” anasema.
Vyanzo vya habari vinaeleza
kwamba, asali ina soko zuri kwani kilo moja inauzwa kwa Shs. 15,000 ikiwa
shambani.
Kwa mujibu wa Kunambi,
mzinga mkubwa wa kisasa una uwezo wa kutoa kati ya kilo 10 hadi 20 za asali
baada ya miezi sita tangu nyuki kuingia kwenye mzinga.
Amewataka wananchi katika
wilaya hiyo kujitokeza na kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki, huku akiahidi
kwamba yuko tayari kufanya kazi usiku na mchana kuwasaidia utaalamu na ushauri.
Mkurugenzi wa Wilaya ya
Mvomero, George Mkindo, amewapongeza akinamama hao kwa jitihada zao na akasema
halmashauri yake itawaunga mkono kwa kila hali.
“Nimeambiwa kwamba
wanahitaji shamba, nadhani itakuwa vyema kama tukiongea na vijiji ili kutenga
mashamba kwa ajili ya ufugaji wa nyuki kwa sababu inatupunguzia hata sisi kazi
kubwa ya kupambana na waharibifu wa mazingira, kwa kuwa wananchi wenyewe
watakuwa walinzi,” anasema.
<Mwisho>.
Comments
Post a Comment