Featured Post

AFYA, MAGONJWA NA NAMNA YA KUWAHUDUMIA MBUZI




Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini 
Mbuzi, kama walivyo wanyama wengine wa kufugwa, wanahitaji uangalizi makini hasa katika suala la afya na ustawi wao. Yapo pia magonjwa mengine ambayo husababishwa na upungufu wa viinilishe, vitamini na protini. Hii hutokana na ulishaji duni wa mifugo.
Mbuzi wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali ambayo yanasababishwa na bakteria, virusi, protozoa, riketsia, na vyanzo vingine. Utambuzi wa magonjwa ni mgumu kwa sababu magonjwa mengi yanaweza kuwa na dalili zinazofanana. 
Dalili ambazo zinaonyeshwa katika makala haya ndani ya MaendeleoVijijini ni za muhimu kitaalam ili kuwasaidia wafugaji kutambua kama mbuzi ni mgonjwa mapema kabisa. 
Tiba inaweza isiwe kamilifu kwa sababu dawa nyingine zinaweza kuleta ukakasi, hasa kama tatizo limekuwa kubwa. Mfugaji anapaswa kuchukua hatua zaidi kwa kumuona mtaalam wa mifugo kwa msaada.
Kabla ya kuendelea na kuyatazama magonjwa mbalimbali, hebu tuangalie kwanza dalili za mbuzi ambaye ni mgonjwa:

Manyoya husimama

Kuzubaa, kusinzia, kukohoa na kupiga chafya

Kukosa hamu ya kula na kunywa maji

Kujitenga na kundi

Kuvimba taya la chini

Kupumua kwa shida

Kutokwa na machozi na makamasi

Kuwa na upele au uvimbe kwenye sehemu ya mwili

Kutupa mimba, na

• Kuvimba midomo na miguu


Kama mfugaji utaona dalili hizo unatakiwa kuchukua hatua za haraka ikiwa ni pamoja na kumuona ofisa mifugo ili awapatie tiba. Lakini kinga ni bora kuliko tiba, hivyo ni vizuri kuwachanja mbuzi wako dhidi ya magonjwa mbalimbali kama homa ya mapafu, ugonjwa ambao ni hatari sana na huenea kwa njia ya hewa ambapo unaweza kusababisha vifo kati ya asilimia 60-100. Usipokuwa makini unaweza kuwapotea mbuzi wako katika kipindi kifupi mno.
Hakikisha kwamba kila baada ya miezi 6 mbuzi wako wanapatiwa kinga dhidi ya ugonjwa wa miguu na midomo na magonjwa mengine kama kimeta, bonde la ufa, kutupa mimba na chambavu (BQ) kulingana na ushauri wa mtalaam wa mifugo.
Ikiwa kuna wanyama walioathirika watengwe kwenye kundi, wasisafirishwe
au kuuzwa. Hakikisha unawapatia mbuzi dawa ya minyoo. Vitoto vya mbuzi vipatiwe dawa ya minyoo vinapofikia umri wa mwezi 1 na viendelee kupatiwa dawa ya minyoo kila mwezi hadi vinapofikia miezi 5 na baada ya hapo vipatiwe dawa ya minyoo kila baada ya miezi 3 – 4.
Jambo muhimu zaidi ni kuzingatia usafi wa banda ili kuwakinga na ugonjwa wa kuharisha na kuharisha damu na magonjwa mbalimbali. Mazingira safi ya banda – mahali pa kulishi na pa kulala – yatapunguza kwa kiasi kikubwa magonjwa ya mifugo.
Kumbuka tu kwamba, mbuzi waliotunzwa vizuri wanakuwa na afya bora na wavumilivu mno kuliko hata binadamu mwenye afya. Lakini nimeeleza hapo mwanzo kwamba, mbuzi huugua hata kama ni mstahimilivu wa magonjwa.
Huhitaji kuwa mtaalam wa tiba za mifugo ili uweze kuwaangalia, lakini unapaswa kuwatunza na kutambua dalili kwamba mbuzi wako wana matatizo. Kama mbuzi amenyongea, amevimba macho, hataki kula ama anaonyesha tabia zisizo za kawaida, lazima uwe makini na umwite mtaalam wa mifugo mara moja.
Kuna magonjwa mbalimbali ambayo yanaweza kumfanya mbuzi akawa na mabadiliko ya kiafya:

Kuvimba kiwele (Mastitis)
 Ugonjwa wa kuvimba kiwele (mastitis) ni wa kawaida kwa mbuzi, hasa wa maziwa. Ni uvimbe ambao huonekana mara ya kwanza kwamba kiwele kimekuwa kigumu kama jipu (ingawa ugumu wa kiwele ni wa kawaida kwa mbuzi wa maziwa hasa baada ya kuzaa) au wakati mwingine hutoa maziwa yasiyo ya kawaida.
Kuna aina tatu za ugonjwa wa kuvimba kiwele, na mbuzi wengi huonyesha dalili kidogo miongoni mwazo. Wanaweza kutoa maziwa yenye povu jingi ambalo siyo la kawaida.
Ugonjwa huu mara nyingi husababishwa na uzembe na kutozingatia kanuni za ukamuaji wa maziwa.
Ugonjwa wa mastitis unasababishwa na vimelea kama Staphylococci, streptococci, E. coli, Mycoplasma agalactiae, M. arginini, na Ukungu.
Dalili zake: Homa kali wakati uvimbe ni mkubwa, kiwele kinakuwa kikubwa sana, anapata joto sana, maziwa yanakuwa na majimaji, maziwa yanaweza kuwa na damu damu, maziwa yanakuwa kidogo, kiwele kinakuwa kigumu.
Kama maambukizi ni makubwa sana: Maziwa yanachachuka haraka, yanaganda, yanatoa harufu mbaya.
Tiba: Kwanza inahitajika kupima kwa kutumia kipimo cha Rapid - Mastitis Test, inahitajika kumtibia kwa terramycin, orbenin L/A au aureomycin, lakini epuka kutumia chlorampehnical kwa sababu inapunguza uzalishaji wa maziwa.
Kinga: Osha kiwele kwa kutumia dawa maalum ya maji maji ya KMnO4 solution, na baada ya kuitumia yakamue maziwa kwenye kiwele hicho. Mwanzishie mbuzi dawa ya antibiotic 1/mammary infusion, acha kwa saa 24 na rudia tena kwa siku 3. Lakini kila wakati mbuzi apimwe kama ana uvimbe kwenye kiwele
Angalizo: Kuutibu, kama unavyotibu magonjwa mengine, kunaweza kusababisha dalili nyingine na siyo chanzo cha tatizo. Hapo unamhitaji mtaalam wa mifugo ambaye atasaidia kutambua aina ya ugonjwa huo, chanzo na tiba yake sahihi.

Uvimbe au Majipu (Lymphadentitis)
Uvimbe (Lymphadentitis) au majipu, ni tatizo jingine linalojitokeza mara kwa mara. Uvimbe huu au jipu hutokea kwenye bega, ingawa unaweza kutokea mahali popote kama kwenye mbavu au paja.
Mbuzi wengi hupatwa na uvimbe huu mapema tu, na siyo ajabu katika mazingira yetu ya ufugaji wa asili, unaweza kukuta kundi la mbuzi limeenea na uvimbe huo. Baadhi ya watu huwa hawapo makini kuhusu uvimbe huo na huona ni jambo la kawaida.
Inapotokea mmoja ana uvimbe wa aina hiyo ni lazima kumtenga na wenzake. Kiafya inashauriwa pia kwamba hata maziwa kutoka kwa mbuzi hao hayafai kunywewa kabla ya kuchemshwa na ikiwezekana yagandishwe. Na kama uvimbe uko kwenye kiwele, acha kabisa kumkamua.
Uvimbe huo hauwezi kumsumbua mbuzi, lakini unakuwa hatari zaidi kama utakuwa kwenye koo na unaweza kuzuia koromeo kupitisha hewa na chakula, hivyo mnyama anaweza kufa.
Mtafute mtaalam wa mifugo ambaye anaweza kukushauri tiba inayostahili au nini cha kufanya.

Brucellosis (Brucella organisms)
Huu ni ugonjwa unasababishwa na vijidudu.
Dalili zake kuu: Kuharibu mimba mwishoni kabisa wakati anakaribia kuzaa ni dalili kwamba ana ugonjwa huo, maumivu kwenye placenta ni dalili nyingine. Kwa mbuzi dume, kutokuwa na uwezo wa kurutubisha mimba na vifundo kuvimba.
Kinga: Mbuzi lazima wapimwe kuona kama wana ugonjwa wa brucellosis na walioambukizwa watengwe na wengine.

Kichwa Kikubwa (Big-Head)
Hii hutokea wakati mbuzi anapokuwa ameshambuliwa sana na minyoo, kutoa ute, kuvimba kichwa na kupauka kwa ngozi.

Bloat
Ugonjwa wa Bloat unasababishwa na kuwa na gesi nyingi tumboni, hasa kwenye utumbo mpana (rumen) na utumbo wa kati (reticulum). Hii mara nyingi hutokea wakati mbuzi wanapoachiliwa kwenda malishoni au wanapokula vyakula vingi vyenye kiwango kikubwa cha succulents, hasa nyasi aina ya Lucerne.
Mbuzi anakosa raha, anakita miguu kama anafanya gwaride, anakojoa mara kwa mara, anatembea kwa ukakamavu.
Kama ilivyo ada, kinga ni bora kuliko tiba. Walishe mbuzi nyasi kavu kabla ya kuwaachilia wachunge kwenye malisho nyakati za masika. Usiwalishe mbuzi wako majani mabichi kama hawajazowea.
Bloat inasababishwa na kujaa kwa gesi ambayo imezuiiliwa katika mfumo wa mapovu madogo madogo na kumfanya mbuzi ashindwe kucheua.
Kikombe kimoja cha nafaka hasa mahindi, kunde au mafuta yenye madini kitaliondoa tatizo hilo.
Kama hali ni mbaya, ni muhimu kuondoa gesi kumchanja (incision) katikati ya mbavu ya mwisho na paja, na kuliacha wazi jeraha hilo wazi kwa kupenyeza mpira.

Ndui ya Mbuzi (Goat Pox)
Ndui ya mbuzi au goat pox inanahusisha vivimbe ambavyo hubadilika na kutoa majimaji, kisha kunata na majipu kwenye kiwele au katika maeneo ambayo hayana manyoya. Ndui ya mbuzi inaweza kudhibitiwa kwa kuzingatia utunzaji bora. Muda na huduma bora ni mambo ya msingi.
Dalili: Homa, uvimbe unaotokea kwenye masikio, pua na kiwele. Kwa mbuzi wadogo, joto kali hutokea, lakini kifo kinaweza kutokea kabla hata ya ngozi kuvimba.
Kinga: Watenge mbuzi wagonjwa na kila siku waoshe kwa mchanganyiko wa hydrogen peroxide dilute yenye mchanganyiko wa maji ya vuguvugu ikifuatiwa na kuwapaka cream maalum. Mikono ya wakamuaji ipakwe dawa maalum. Hakikisha mbuzi wenye ugonjwa huo wanakamuliwa mwishoni kabisa ili kuepuka kuusambaza ugonjwa.
Hata hivyo, muone mtaalam wa mifugo kwa ushauri, tiba na kinga.

Ketosisi (Ketosis)
Ketosisi au Acetonemia ni ugonjwa ambao hutokea kwa mbuzi mwenye mimba katika mwezi wa mwisho kabla ya kuzaa. Mara nyingi huwashambulia mbuzi wenye uzito mkubwa au ambao hawajalishwa vyema na waliko katika mazingira hafifu, lakini unaweza kuchangiwa na mazoezi makali, kama kufukuzwa na mbwa.
Mbuzi mwenye ugonjwa huo amezubaa, na mara nyingi hana hamu ya kula. Anaweza akapatwa na kiharusi na kuharibu mimba.
Hata kwa tiba kama kumpatia kikombe cha molasses mara mbili kwa siku au wakia (ounces) sita za glycerin au propylene glycol kila siku, mbuzi huyo ana asilimia 50/50 za kupona.

Kula sumu
Wafugaji wengi wapya wa mbuzi wanahofia sana suala la kula sumu, lakini siyo tatizo kubwa sana. Mbuzi wengi hutengewa chakula na wamiliki wao, hivyo ni imani kwamba chakula hicho kitakuwa safi na salama.
Kwa mbuzi wengine wanaachiliwa malishoni, utaratibu wao wa kula hiki na kile mara nyingi huwazuia kula mimea ambayo ina sumu.
Ingawa mimea yenye sumu ni michache kwa asilimia ya malisho ya mbuzi, lakini hata mimea ya kawaida inaweza kuwa na sumu katika mazingira fulani. Usiwalishe mbuzi wako nyasi au majani ambayo yamepuliziwa kemikali ama dawa za kuulia wadudu, au kuwachunga katika shamba ambalo limemwagiliwa mbolea za kemikali. Mbuzi wanaweza kula na kupata madhara.
Ikitokea kama wamekula sumu, wape maji mengi sana, lakini mtafute mtaalam wa mifugo ikiwa tatizo linakuwa sugu.

Minyoo na vijidudu
Wadudu kama minyoo na kupe wanahitaji umakini wako. Mbuzi wote wana minyoo kama nilivyoeleza kwenye makala ya Ufugaji Bora WaMbuzi Wa Maziwa. Lakini mfugaji bora wa mbuzi anaweza kuwadhibiti. Kwa vile kuna aina mbalimbali za minyoo na hakuna dawa ambayo inaweza ikawaua wote, ni muhimu kumtumia mtaalam wa mifugo mwenye uzoefu anaweza kutambua ni minyoo gani unayopaswa kuwa makini nayo, dawa gani za kutumia, na mara ngapi.
Wafugaji wengi wanawapa kinga mbuzi mara mbili kwa mwaka katika majira ya masika na vuli.
Kuwapa dawa kila wakati bila mpangilio ni mbaya kama kutowatibu kabisa. Tiba ya asili kama kuwalisha mbuzi majani ya tumbaku haisaidii. Kupe, chawa na vijidudu vingine vidogo vinashambulia kwenye ngozi. Vinaweza kumtesa mbuzi. Ukiona mbuzi wako hawana manyoya wakati walipaswa kuwa nayo, wamenyonyoka na hawatulii, ujue wadudu hao wamewavamia.

Kuharibu mimba
Kuharibu mimba mara nyingi hutokea wakati mbuzi ana mimba ya miezi 6-8. Tiba ya kitaalam inahitajika wakati huo ili kuzuia urutubishaji duni.
Tatizo hili linaweza kutokea kutokana na kunywa maji yenye wadodo aina ya salmonella typhinmurium. Kuharibu mimba pia husababishwa na mbuzi kulishwa chakula hafifu ingawa yapo pia matatizo mengine.

Anaemia
Anaemia au upungufu wa damu hutokea pia kwa mbuzi. Ngozi inaweza kupauka na unaweza kuona kubadilika kwa ngozi katika macho na midomo, kiwele pamoja na sehemu nyingine zisizo na manyoya.
Unaweza kuwatibu mbuzi wenye upungufu wa damu kwa kuwachoma sindano yenye madini joto kwa kiwango cha 5ml Dexavin (Pfizer) au Ferrofax (Duphar).

Sotoka au Ndigana (Rinderpest)
Kwa wafugaji wanaelewa nini maana ya sotoka, ugonjwa ambao unaweza kushambulia zizi lako mara moja na unawapata ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Dalili za mnyama wenye sotoka ni homa za kushtukiza na kuhara. Sehemu ya haja kubwa inaweza kuwa imevimba ama kuchubuka.
Kinga na tiba: Kama kuna mnyama ameambukizwa, mchome na sindano ya rinderpest vaccine S/C.
Lakini ni muhimu sana ukamuona mtaalam wa mifugo, kwa sababu ugonjwa huo unaweza kusambaa.
Jitahidi kutoruhusu watu kuingia ovyo zizini (bandani) n ahata kwa wanaoingia, chimba shimo dogo kwenye mlango, weka maji na weka dawa maalum ili kila anayeingia na kutoka lazima aingize miguu yake humo kuua vijidudu.

Kimeta (Anthrax)
Kimeta ni ugonjwa hatari sana kuliko hata sotoka. Unaweza kufagia kundi zima la mifugo katika muda mfupi na unaambukizwa na bakteria waitwao Bacillus anthracis.
Dalili kwa mnyama mwenye ugonjwa huo ni: Kupanda ghafla kwa joto hadi kufikia nyuzi joto 108°F, kukosa hamu ya kula, kutoka povu mdomoni, vifo vya ghafla. Mbuzi anaweza kuishi kwa siku moja na kuanza kuhara damu kabla ya kufa.
Inashauriwa mnyama aliyekufa kwa kimeta mfukie kwenye shimo kubwa kwa sababu bakteria hao wanaweza kusambaa na kushambulia wanyama wengine.
Kinga na tiba: Watenge wanyama walioambukizwa. Hakikisha kila mwaka unawachanja mbuzi wako hasa katika maeneo ambayo yanakumbwa mara kwa mara na ugonjwa huo. Dozi kubwa ya penicillin 1/M inaweza kuwatibu mbuzi.

Cystitis
Huu ni ugonjwa ambao dalili zake ni kuvimba kwa kibofu cha mkojo, maumivu ya nyonga, kutoa mkojo kidogo, mbegu za uzazi zikiwa zimechanganyika kwenye mkojo, mnyama kukosa zmani na kusikia kiu sana.
Tiba: Mtibu mnyama kwa kutumia antibiotic ukichanganya na lita mbili za maji ya uvuguvugu na kijiko kimoja cha hibitane au Dettol.

Collibacillosis/collisopticaemia (E. coli)
Huu ni ugonjwa unaowapata zaidi watoto mbuzi wenye umri chini ya mwezi mmoja. Dalili zake ni homa na kuhara, au kuhara damu. Kukosa hamu ya kula, kuchachamaa kwa manyoya na kukauka kwa ngozi katika hatua ya baadaye ni mambo yanayojitokeza.
Kinga na tiba: Pulizia dawa kwenye mazingira unayoona yanaweza kuwa na bakteria wa E. coli na uchunguze kila wakati uwepo wake. Mbuzi wote wadogo wapatie dozi ya antibiotic maalum. Dawa kama Darzin yenye mchanganyiko wa neomycin chloromycetin, Septran na quixalin bolus hutumika zaidi.

Klamidia
Ugonjwa wa Klamidia (au Chlamydiosis) unasababishwa na wadudu wa klamidia. Dalili mojawapo ni homa ya mapafu (pneumonia), wakati mwingine kuhara.
Mbuzi wenye mimba wanaweza kuharibu mimba mapema wakiwa na ugonjwa huo. Kwa mbuzi watoto wanaweza kuwa na kifua cha kukoroma (arthritis).
Wakinge mbuzi kwa kuwachoma sindano ya penicillin.

Coccidiosis
Kama ulidhani Coccidiosis ni ugonjwa unaowapata kuku na jamii nyingine ya ndege pekee, basi umekosea. Ugonjwa huu huwapata hata mbuzi.
Dalili kubwa ni kuhara damu, upungufu wa damu, udhaifu na kifo kwa watoto. Kwa wale wakubwa, maziwa yanayokamuliwa yapungua na yanakuwa na kiharufu kikali.
Kinga tiba: Lazima kipimo cha Faecal kifanyike kwa mbuzi wako. Wapatie dawa ya Sulphamezathine au sulphadimidine 0.2 gm/kg kwa kuangalia uzito wao. Wape pia Amprosol 20% ya majimaji 100 mg/kg kwa uzito wa mnyama kwa siku 4-5 au wapatie zoaquin.

Ugonjwa wa Miguu na Midomo (Foot and Mouth Diseases)
Ugonjwa huu unasababishwa na Virus na unakuja katika aina mbalimbali (O, A, C na Asia one type). Unawashambulia zaidi mbuzi wakubwa.
Dalili zake ni kwamba, wanakuwa na michubuko kwenye ulimi, midomo, mashavu, fizi, kwenye ngozi, katikati ya kwato, uvimbe mdogo kwenye matiti na ndani ya mapaja. Kushindwa kutembea ni dalili inayoweza kutokea kwa mbuzi wakubwa. Mbuzi wadogo wakipatwa ugonjwa hufa.
Kinga tiba: Watenge mbuzi wagonjwa na wape kinga wengine wote mara ugonjwa unapoibuka. Safisha midomo ya mbuzi walioathirika kwa kutumia dawa ya majimaji kama Alum au Potassium permanganate.

Kuoza miguu
Kuoza miguu ni ugonjwa unaoenea haraka sana kwenye kundi la mbuzi, unasababishwa na mchanganyiko wa bakteria huko mojawapo wakiwa Dichelobacter nodosus. Kuna aina mbili kubwa za kuoza miguu - virulent na benign, na wanaambukizwa kwa namna tofauti na bakteria wa Dichelobacter nodosus.
Maambukizi ya bakteria hao yanasababisha madhara makubwa kwenye miguu hasa kwato na kuwafanya wawe walemavu, wanashinda kusimama na hupungua uzito haraka. Huanza kwa kuonekana uvimbe mdogo katikati ya kwato.
Mtafute mtaalam wa mifugo kwa usaidizi Zaidi.

Hitimisho
Malengo ya makala haya ni kwamba, mfugaji walau anaweza kuona baadhi ya dalili zinazoonekana na kutoa huduma ya kwanza ambayo siyo tu inazuia kuenea kwa ugonjwa na kumuathiri mbuzi husika, lakini inaokoa maisha.
Mfugaji lazima aelewe tatizo lililopo ili amtafute mtaalam wa mifugo na kumweleza hali halisi ilivyo.

Kwa mafunzo zaidi ya gharama nafuu, usisite kunipigia ama kuwasiliana name kwa whatsapp kupitia namba 0656-331974. Au barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.



Comments