Featured Post

UMWAGILIAJI WA MATONE WAWANUFAISHA WAKULIMA TANANGOZI




Na Daniel Mbega, Iringa

MIAKA mitatu iliyopita, hali ya uchumi ya Nobert Rajab Kikoti (57) ilikuwa ya kawaida kama walivyo wakulima wengi wa kijijini kwake Tanangozi mkoani Iringa.
Hii ni kwa sababu alikuwa akifuata ‘kilimo cha mazoea’ kisichozingatia utaalam katika uandaaji wa shamba, uchaguzi wa mbegu bora, uandaaji wake na hata utunzaji wa mimea.
“Lakini sasa mambo yamebadilika, mavuno ninayoyapata ni makubwa kiasi kwamba najiuliza nilikuwa wapi siku zote… Nimepata mafanikio makubwa katika kipindi kifupi na nitahakikisha naongeza juhudi,” anasema Kikoti, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Tanangozi.
Mabadiliko hayo, anasema, yametokana na mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa kutumia matone hasa wakati wa kiangazi unaohusisha kaya 200, ambao unawafanya wakulima wengi wa nyanya kujishughulisha na kilimo kwa mwaka mzima.
Anasema mradi huo ulioibuliwa na wananchi wa Tanangozi tangu mwaka 2007, ulifanikishwa kwa asilimia kubwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) baada ya serikali ya kijiji kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa ajili ya msaada.
“Wananchi walichangia nguvu kazi tu za kuchimba mitaro ya kupitisha mabomba, lakini gharama zote, ambazo ni zaidi ya Sh 700 milioni, zilitolewa na Tasaf. Leo hii wakulima zaidi ya 200 wananufaika na mradi huu wakimiliki eneo la robo ekari na kwa hakika hali ya uchumi imebadilika,” anaongeza Kikoti ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mradi huo wa Umwagiliaji.
Tasaf iliweza kuwajengea tanki kubwa la maji lenye uwezo wa kujaza lita 100,000 na pampu ya kutumia umeme, lakini pia kuwatengenezea mfumo mzima wa umwagiliaji kwa kuweka mabomba na mipira ambayo kila mkulima ameitandika shambani kwake.
Anasema binafsi amenufaika na mradi huo kwa kujenga nyumba yenye thamani ya Sh 40 milioni mpaka itakapokamilika, lakini pia anaweza kulipa ada ya watoto wake bila shida, amenunua ng’ombe watatu wa kisasa na ana mtaji wa kutosha kuendesha kilimo chake.
“Miaka mingi nimekuwa nikilima lakini sikuwahi kupata mafanikio kama haya. Kwa mwaka ninazalisha nyanya mara mbili, sijatoka bado wala siwezi kuridhika na mafanikio haya, bali hii inanipa changamoto kubwa ya kuendelea kulima nyanya,” anasema.
Anaongeza; “Msimu wa masika, kwa mkulima mwenye eneo la ukubwa wa ekari moja anaweza kuvuna mpaka matenga 700, ambayo endapo atayauza kwa Sh 10,000 anaweza kupata Sh 7 milioni.”

Elimu ya kilimo
Kikoti anaongeza kwamba, mradi huo usingeweza kufanikiwa bila msaada wa elimu kutoka kwa wadau mbalimbali hasa wa masuala ya kilimo na ujasirimali.
Anaitaja taasisi ya Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (Muvi) kuwa ndiyo iliyowawezesha kuwapa elimu na mafunzo ya vitendo katika kilimo bora, hasa cha nyanya, kwa kuwapatia mbinu za kisasa ambazo ndizo zinazowaelekeza kwenye mafanikio makubwa.
“Muvi imetupatia mafunzo ya kilimo bora, kuboresha njia za mawasiliano baina yetu na kutuunganisha na masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi,” anaeleza.
Hali kadhalika, Kikoti anasema Muvi wamewasaidia kupata mbegu bora za kisasa hasa aina ya Eden na Asila zinazotengenezwa na kampuni ya Monsanto ya Kenya, ambazo, mbali ya kutoa mavuno mengi kwa wakati mmoja, lakini pia matunda yake yanastahimili, ambapo yanaweza kukaa kwa takriban siku 40 bila kuharibika, tofauti na mbegu za kawaida.
“Kwa msingi huo, mkulima anakuwa na muda wa kutafuta soko mwenyewe badala ya kulanguliwa na wafanyabiashara, hivyo atauza kwa bei nzuri inayolingana na gharama alizotumia katika kilimo,” anafafanua.
Lakini mbali ya Muvi, wadau wengine waliowasaidia, ambao wanaendelea kuwasaidia, ni mradi wa TAPP (Tanzania Agriculture Productivity Program), ambao wanatoa mafunzo ya vitendo kwa kuwalekeza namna ya kuandaa mbegu, kutunza mimea na hata uvunaji.
“Jana (wiki iliyopita) nilikuwa Ilula kwenye mafunzo ya vitendo, kwa hakika elimu niliyoipata kwa siku moja tu imenifanya nijione nimechelewa na nimekuwa nikikosea kwenye kilimo changu. Mategemea kwamba msimu huu nitaitumia elimu hii kwa ukamilifu ili iniletee tija,” anasema.
Hata hivyo, mkulima mwingine aliyeona mafanikio ya mradi huo ni Mtokambali Mgimba, ambaye anasema bila shaka kwamba kilimo hicho cha nyanya chini ya mradi huo kimempa faida kubwa katika kipindi kifupi.
Mkazi huyo wa Tanangozi anasema kwamba, katika msimu uliopita ameweza kuondokana na nyumba ya nyasi na kujenga nyumba ya bati hapo hapo kijijini yenye thamani ya Sh 6 milioni, lakini pia ameweza kununua nyumba mjini Iringa kwa Sh 50 milioni.
“Watoto wangu hawana hofu ya kufukuzwa shule kwa kukosa ada, lakini bado ninao mtaji wa kutosha kuendelea na kilimo cha kisasa,” anasema Mtokambali.
Mtokambali anasema, baada ya kupewa mafunzo ya kilimo bora cha nyanya, akajiunga katika mtandao wa wakulima wa Nyanya wilayani Iringa, ikiwa ni pamoja na kuelekezwa mbegu bora ya nyanya ambazo baada ya mavuno zinaweza kuhimili muda mrefu bila kuharibika.
Kutokana na aina ya nyanya wanazolima, soko la nyanya hizo linapatikana kwa urahisi kwa vile wafanyabishara wengi wamekuwa wakizipenda kutokana na sifa ya kukaa muda mrefu bila kuharibika.
Mkulima huyo anasema, alianza kujishughulisha zaidi na kilimo baada ya kustaafu, ingawa mwanzoni hali haikuwa rahisi. “Nilipostaafu sikuwa na uhakika kama ningeweza kumudu kuyaendesha maisha yangu. Nilizowea kuajiriwa, sikuwa na matumaini kama maisha yangeweza kuendelea bila ajira, nikakata tamaa. Nilikonda kwa mawazo na kujua huo ulikuwa mwisho wangu, kama ilivyo kwa wastaafu wengi.”
Lakini akili ya kurudi kijijini ilipomjia, aliamua kufanya hivyo na kuanzisha mashamba ya mahindi. Hii ilikuwa ni baada ya kushindwa kumudu kulipa hata pango la nyuma, kununua chakula wala kulipa ada ya watoto wake.
Anabainisha kwamba, kilimo cha mahindi hakikumletea tija kwa sababu pamoja na kuvuna mazao mengi, hakuweza kuuza kwa bei nzuri kwa sababu soko lenyewe lilikuwa la kubahatisha.
Hatimaye miaka mitano iliyopita, Mtokambali, mwenye mke na watoto wane, akaamua kubadili kilimo chake na kulima nyanya hasa baada ya kuona jirani yake akipata mavuno mengi na kumletea kipato kikubwa.

Changamoto zinazowakabili
“Elimu bado ni tatizo kwa wakulima wengi. Bado wanasita kuutumia vyema mradi huu na hata wale walioko kwenye mradi, baadhi yao hawazingatii maelekezo ya wataalam,” anasema Kikoti.
Pamoja na uzalishaji kujongezeka, lakini soko bado ni la kubahatisha ingawa Muvi wamejitahidi kuwaunganisha na masoko ya nje. Muvi kwa kushirikiana na viongozi wa shirikisho la wakulima wa nyanya wamefanya ziara za ndani na nje ya nchi katika harakati za kutafuta masoko zaidi, ambapo wamefika Kenya, Malawi na hatimaye Zambia.
Jambo ambalo Muvi wameligundua kupitia kitengo chake cha biashara na masoko ni kukosekana kwa taarifa za biashara na masoko kutoka ngazi zote, hali inayoleteleza kushuka kwa bei ya zao la nyanya.
Ili kukabiliana na tatizo hiyo, Muvi sasa wanahakikisha kunakuwepo na mawasiliano ya kutosha kutoka mikoa yote ya Tanzania na kujua ni bei gani inayotembea sokoni kila siku ili kuwawezesha wakulima kuuza mazao yao kw abei nzuri.

Kauli ya Muvi
Willima Mwaikambo Mtui, Mratibu wa Muvi Mkoa wa Iringa, anasema wamefanya utafiti kuhusu nyanya zinazozalishwa na Mtokambali na wakulima wengine wa Tanangozi na kubaini kwamba zinaweza kukaa kwa siku 35 bila kuharibika katika eneo lenye hali ya hewa ya kati na hadi siku 40 katika maeneo ya baridi.
Anasema wameweza kuwaunganisha wakulima wa zao hilo na mitandao ya masoko hapa nchini na nje ya nchi, ambapo anasema nyanya nyingi zinazozalishwa Iringa zinasafirishwa Visiwani Zanzibar pamoja na Visiwa vya Comoro.
“Hata Kenya nao wanakuja kuchukua nyanya huku. Tunajitahidi kuwahamasisha wakulima wa nyanya kutumia kilimo cha kisasa na mbegu bora ili waweze kupata tija,” anasema.
Hata hivyo, Mtui anawakumbusha wakulima kuweka kumbukumbu za kuanzia uzalishaji hadi uuzaji wa mazao yao na pia kuandaa mpango wa biashara ili kuweza kujua nini wanachopata kwenye kilimo hicho.
“Wajasiriamali wengi wanasahau kuweka kumbukumbu za uzalishaji, hali hii inawafanya wasijue wametumia gharama kiasi gani na faida kiasi gani baada ya mavuno. Hili lazima walielewe, vinginevyo watakuwa wanalima bila kujua kama wanapata hasara ama faida,” anasema.


Comments