Featured Post

RC MAKALA AAGIZA KUKAMATWA KWA MKANDARASI WA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE WA SONGWE BAADA YA KUSHINDWA KULIPA MAFAO YA VIBARUA ZAIDI YA 50

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla,akitolea ufafanuzi na kujibu kero mbalimbali zilizotolewa na wananchi wa Mkoa wa Mbeya, katika kikao maalum cha kupokea kero za wananchi kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mkapa, ambapo kubwa zaidi katika siku hii, Makala amesema serikali itahakikisha inamkamata mkandarasi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Songwe kutoka kampuni ya Kundan Sigh, baada ya kushindwa kulipa mafao ya vibarua zaidi ya 50.


Na Emanuel Madafa, Mbeya
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla ameagiza kukamatwa kwa  mmiliki wa kampuni ya Kundan Singh, ambaye alipewa tenda ya kujenga uwanja wa ndege wa Songwe, baada ya kushindwa  kulipa mafao ya vibarua zaidi ya 50.



Mkuu huyo wa Mkoa wa Mbeya ametoa kauli hiyo , wakati akijibu na kutatua kero mbalimbali za wananchi ambazo hazijapatiwa ufumbuzi kwa kipindi kirefu, hali iliyochangia wananchi kuichukia serikali kwa madai ya kushindwa kuwatendea haki.



Awali, akitoa malalamiko  hayo kwa Mkuu wa Mkoa, Joshua Mwasilonde kwa niaba ya vibarua wenzake, amesema wamekuwa wakidai mafao yao tangu mwaka 2012/2013 katika mfuko wa hifadhi ya jamii NSSF na kwamba kila wanapofuatilia wamekuwa wakipigwa kalenda.



Akilizungumzia hilo, Makala amesema, kwakua serikali iliingia mkataba na kampuni hiyo na kumalizana nayo bila ya kuacha deni lolote hivyo mkandarasi huyo anapaswa kuwalipa vibarua hao na kuutaka uongozi wa NSSF, kuhakikisha unavishirikisha vyombo vya dola katika kumkamata mkandarasi huyo.



Meneja NSSF Kanda ya Nyanda za Juu kusini, Robert Kadege, akilitolea ufafanuzi suala hilo, amesema suala la vibarua hao linafanyiwa kazi na kwamba tayari mahakama imetoa hukumu na kuupa ushindi mfuko huo..

Mwisho.
Katibu tawala Mkoa wa Mbeya Mariam Mtunguja, akitolea ufafanuzi baadhi ya masuala ya kiutendaji katika kikao  hicho.
Baadhi ya wananchi waliofika kutoa kero na malalamiko katika kikao hicho.
Baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali katika kikao maalum cha kupokea kero za wananchi kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mkapa June 29 mwaka huu.
Baadhi ya wananchi wakitoa malalamiko na kero zao katika kikao maalum cha kupokea kero za wananchi kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mkapa June 29 -2016 ambapo MKuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla ndiye aliyepokea kero hizo sanjali na watendaji wa serikali na taasisi  mbalimbali za serikali .

Kikao kikiendelea.(Picha E. Madafa)

Comments