- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Bi. Esther Chiombola akionyesha uyoga ambao uko tayari kuvunwa. Uyoga huo unalimwa na kikundi cha Tunza Women Group cha Bunju jijini Dar es Salaam kwa ufadhili wa mradi wa Green Voices (Makala na Picha zimeandaliwa na www.brotherdanny.com).
Bi. Sauda Issa miaka 70 (kushoto) mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam akipokea zawadi ya kitabu maalum kinachozungumzia kilimo cha uyoga kutoka kwa Bi. Esther Chiombola ambaye ni Ofisa Kilimo Msaidizi Mwandamizi wa Manispaa ya Kinondoni.
Mratibu wa vikundi vya kilimo cha uyoga Bunju na Boko, Magdalena Bukuku (katikati) akiteta jambo na mratibu wa green Voices nchini Bi. Secelela Balisidya wakati wa uzinduzi wa mradi huo unaofadhiliwa na Green Voices. Wengine pichani kutoka kushoto ni Bi. Lucresia Tarimo aliyemwakilisha Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Kinondoni, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kilungule Seif Stambuli, na Ofisa Kilimo Kata ya Bunju, Rhoda Mruttu.
Bi. Sophia Chove, mwenyekiti wa kikundi cha wakulima wa uyoga Bunju, akitoa maelekezo kwa watu mbalimbali kuhusu namna ya uchanganyaji wa vimeng’enyo vya kuoteshea na kukuzia uyoga.
Mchanganyiko maalum wa vimeng’enyo vinavyotumika katika kilimo cha uyoga.
Uyoga ukiwa unaoteshwa katika eneo maalum kwa kufunikwa kaniki.
Mchuzi mzito wa uyoga ulioandaliwa kwa ajili ya chakula cha mchana. Uyoga huo umevunwa katika mradi wa kikundi cha akinamama wa Bunju chini ya ufadhili wa Green Voices.
Wageni waalikwa wakishiriki chakula cha mchana ambacho mboga kuu ilikuwa uyoga.
Akinamama sita, ambao ni sehemu ya akinamama 15 ambao wanatekeleza mradi wa
Green Voices baada ya kupatiwa mafunzo nchini Hispania mwanzoni mwa mwaka huu.
Kutoka kushoto ni Siddy Abubakar Mgumia, Farida Hamisi, Tukuswiga Mwaisumbe,
Secelela Balisidya, Magdalena Bukuku na Judica Losai.
WAKATI Magdalena Bukuku anaibua wazo la kilimo cha uyoga
akiwa mafunzoni jijini Madrid, Hispania mapema mwaka huu 2016 hakutegemea kama
angeweza kupata mwitikio mkubwa kutoka kwa akinamama wa maeneo ya Boko na Bunju
jijini Dar es Salaam anakoishi.
Lakini leo hii, Magdalena, ambaye ni miongoni mwa
akinamama 15 wanaotekeleza Mradi wa Green Voices maalum kwa kupaza sauti za
wanawake kwa ajili ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, anafarijika baada
ya wazo lake hilo kuzaa matunda.
Tayari wanakikundi cha ‘Tunza Women Group’ cha Bunju
wameanza kuvuna kidogo kidogo uyoga ikiwa ni takriban mwezi mmoja tu tangu
walipopatiwa mafunzo, huku wale wa Boko wakiwa katika hatua nzuri za kuendeleza
shamba lao.
“Ni mradi mzuri, unatumia gharama kidogo huku mavuno yake
yakiwa endelevu hasa ukiwa na nia, dhamira na jitihada, hapa Bunju tayari
akinamama wameanza kuvuna uyoga, ambao soko lake lipo kubwa,” anaeleza
Magdalena.
Magdalena ni mmoja wa akinamama wanaotekeleza kwa vitendo
mradi wa Green Voices, ambao unafadhiliwa na taasisi inayojihusisha na maendeleo ya wanawake wa Afrika, ijulikanayo
kama Foundation for Women of Africa inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa
Hispania, MarÃa Teresa Fernández de la Vega.
Akinamama wengine wanatekeleza
miradi mbalimbali ya ujasiriamali unaoendana na mapambano dhidi ya mabadiliko
ya tabianchi katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro,
Pwani na Mwanza.
Anasema, uyoga ni zao
linalohitaji eneo dogo na matumizi kidogo lakini endelevu ya rasilimali maji,
hivyo kuwa rafiki mkubwa wa mazingira licha ya umuhimu wake kwa afya ya
binadamu.
Uyoga ni aina ya kuvu (fungi)
na hauna uwezo wa kujitengenezea chakula kama ilivyo mimea mingine ya rangi ya
kijani, hivyo ili kuota na kustawi, inahitaji chakula ambacho
kimekwishatengenezwa kutoka katika mimea iliyooza.
Sophia Chove, mwenyekiti wa
kikundi cha ‘Tunza Women Group’ katika Mtaa wa Kilungule - Bunju, anaeleza
kwamba, wamepata fursa nzuri ya kuongeza pato la familia pamoja na kushiriki
katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira.
“Kikundi kina wanachama 10,
lakini kwa matokeo ambayo yameonekana, wanawake wengi zaidi wamevutiwa na
wanahitaji kujiunga nasi, tunaamini haya ni mafanikio na siyo vibaya kama kila
kaya itaendesha kilimo hiki ambacho hakihitaji ardhi kubwa,” anasema na
kupongeza hatua ya Green Voices kuwapatia mradi huo.
Kuhusu masoko, Sophia anasema
uyoga ni bidhaa inayohitajika sana ambapo ikiwa watauza reja reja, kilo moja
inauzwa kwa Shs. 10,000, ingawa alikiri kwamba wanahitaji kupata soko kubwa
zaidi kwa vile wanataka kupanua uzalishaji wao.
Akaongeza: “Tumekwishaongea na
super market moja ambapo wahusika wametutaka tupeleke kwa wingi mara
tutakapoanza uvunaji.”
Mradi wa Green Voices ni wa
pekee nchini Tanzania kufadhiliwa na taasisi ya Foundation for Women of Africa,
ambao lengo lake kubwa ni kuwasaidia akinamama kupaza sauti katika masuala ya
mazingira kwa kutumia njia ya ujasiriamali.
“Mama Maria Teresa, baada ya
kutoka madarakani, aliamua kuanzisha taasisi hiyo kwa nia ya kuwakomboa
wanawake wa Afrika, ambao ndio waathirika wakubwa wa athari za uharibifu wa
mazingira pamoja na mabadiliko ya tabianchi,” anaeleza Secelela Balisidya,
Mratibu na msimamizi wa mradi huo nchini.
Secelela, ambaye kitaaluma ni
mwandishi aliyejikita zaidi katika habari za mazingira, anasema ujio wa Green
Voices utawakomboa wanawake wengi wa Tanzania kupitia miradi waliyoibuni ambayo
itasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kama inayoelekezwa katika
Malengo Endelevu ya Dunia.
Anasema, katika uhalisia,
mwanamke ndiye muathirika mkubwa wa mazingira kwani anatumia muda mwingi
kutafuta maji na nishati, hasa kuni, kwa ajili ya matumizi ya familia, kuliko
kufanya shughuli zingine za maendeleo.
“Mradi kama huu wa kilimo cha
uyoga ni rafiki wa mazingira kwa sababu hauhitaji maji mengi, lakini una faida
kubwa kiafya hasa kutokana na ukweli kwamba, hivi sasa watu wengi wameathirika
kwa kula vyakula vinavyozalishwa kwa kemikali,” anaongeza.
Esther Chiombola ‘Mama Uyoga’,
Ofisa Kilimo Msaidizi Mwandamizi wa Manispaa ya Kinondoni ambaye ndiye
aliyewafunza wanakikundi hao wa ‘Tunza Women Group’, anasema uyoga ni lishe
bora ambayo imejaa kiasi cha asilimia 20 hadi 49 cha protini pamoja na Vitamini
B, C, D, E, na K, na madini joto, chuma, fosforas, potashi, zinki na shaba na
kwamba hauna lehemu (cholesterol).
Anasema kwamba, baadhi ya aina
za uyoga kama Ganoderma husaidia kuzuia na kupunguza kasi ya magonjwa sugu kama
saratani, kisukari, kifua kikuu, moyo, shinikizo la damu na figo.
“Lakini ikumbukwe kwamba kilimo
cha uyoga ni ajira kubwa kwa akinamama, vijana, wazee na wastaafu na ni kilimo
rafiki kinachopunguza uchafuzi wa mazingira kwa vile kinatumia mabaki ya
shambani na viwandani,” anafafanua.
Anataja faida nyingine kama
kilimo endelevu cha mwaka mzima na kwamba mabaki yake baada ya mavuno kukoma ni
mbolea nzuri na chakula cha mifugo.
“Kilimo cha uyoga kinasaidia
kupunguza vifo vinavyotokana na kula vyakula vyenye sumu kwani mbegu
zinazotumika zimefanyiwa utafiti na zinapatikana kutoka taasisi maalumu kama
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA), Kituo cha Utafiti wa Kilimo-Uyole, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo
cha Bustani Tengeru na Shirika la
TIRDO,” anasema.
Bi. Chiombola anasema kwamba, aina zinazofaa kwa Tanzania
ni zile ambazo hustawi vizuri, kwenye maeneo ya joto la wastani wa nyuzi joto
20C hadi 33C na kiasi cha unyevunyevu cha asilimia 75.
Hata hivyo, anasema kutokana na hali ya joto la Dar es
Salaam, aina inayolimwa Zaidi ni Chaza (Oyster mushroom) ambayo inastahimili
hali ya joto kwa nyuzi joto 12 – 30 ambapo kundi hilo linahusisha aina ya
Pleurotus sapidus (mweupe na mwingine rangi ya udongo) pamoja na Pleurotus
sajor – caju.
Mahitaji muhimu ya kilimo cha uyoga yanatajwa kwamba ni
banda la kuanzia ukubwa wa meta 4 kwa 5 ambalo linatosha kuotesha mifuko 450
hadi 500, vimeng’enywa ambavyo ni masalia makavu kama mabua ya mahindi, majani
makavu ya mgomba na ya viwandani kama maganda ya alizeti.
Pia inahitajika mifuko maalum inayostahimili joto ambayo
hutumika kujazia vimeng’enya, vifaa vya kazi kama mapipa ya kuchemshia maji,
turubai la plastiki, vipete, pampu ya kumwagilia, mbegu za uyoga, vifungashio
vya plastiki, visahani, virutubisho hasa pumba laini, sukari au molasses,
chokaa na dawa kwa ajili ya usafi, hasa Dettol na spiriti.
Kabla ya kuanza uzalishaji ni lazima kiwepo chumba chenye
paa linalozuia jua, mvua, na vumbi ambacho pia kinapaswa kiwe na sakafu
inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha
utando wa uyoga.
“Baada ya hapo kuandaa masalia na mambo mengine kama
utakavyoelekezwa na mtaalamu, jaza vimeng’enyo hivyo kwenye mfuko wa sandarusi wenye
upana wa sm 40 - 45 na kimo cha sm 75. Weka tabaka la mali ghafi ya kuoteshea yenye
kina cha sm 10 katika mfuko halafu tawanya mbegu ya uyoga juu yake. Baada ya
kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya vioteshea na kuweka mbegu juu yake.
Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifike ujazo wa robo tatu ya mfuko,”
anasema Bi. Chiombola.
Anasema baada ya hapo unatakiwa kufunga mifuko na toboa
matundu kwenye mifuko yenye kipenyo cha sm 1 kwa kila umbali wa sm 6 hadi 10
kwa kila mfuko ili yaweze ili kuingiza hewa ya kutosha ndani ya mifuko.
“Weka mifuko kwenye chumba cha giza. Kwa mkulima wa
kawaida waweza kutumia kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza au
funika kwa kaniki. Acha mifuko humo kwa muda wa wiki tatu hadi nne bila kufunua
ili ukungu mweupe uweze kutanda vizuri.
“Utando mweupe ukishatanda vizuri kwenye mali ghafi ya
kuoteshea fungua mifuko, visha viringi, hamishia kwenye chumba chenye mwanga na
hewa ya kutosha kisicho pigwa na jua. Mifuko inaweza kuwekwa kwenye, meza,
chanja la waya au miti. Anza kumwagilia
kwa pampu (mvuke wa maji baridi) na baada ya wiki moja na nusu uyoga utaanza
kuchomoza,” anaeleza Bi. Chiombola.
Bi. Chiombola anasema kwamba, uyoga huwa tayari kuchumwa
siku tatu baada ya vichwa /pini kuonekana. Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika
katikati ya shina la uyoga kisha zungusha hadi uyoga ung'oke.
“Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga kwani
kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea. Mkulima anatakiwa ajue soko la
uyoga kabla ya kuvuna ili kuepuka gharama za kuhifadhi kwani uyoga ukishavunwa
unatakiwa uliwe kabla haujaharibika,” anaeleza.
Inaelezwa kwamba, uyoga ukishavunwa unaweza kuhafadhiwa
kwenye jokofu kwa muda wa siku 7 kabla ya kuharibika, lakini haipaswi kuhifadhi
kwenye friza.
Comments
Post a Comment