Featured Post

MHIFADHI MWANDAMIZI TANAPA ASHIKILIWA BAADA YA KUKUTWA NA JINO LA TEMBO

HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUSHIKILIWA NA KIKOSI KAZI MAALUM CHA KUPAMBANA NA UJANGILI KWA MHIFADHI MWANDAMIZI GENES SHAYO

Mhifadhi Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Genes Shayo (60) anashikiliwa na Kikosi Kazi Maalum cha kupambana na ujangili nchini kufuatia taarifa za kuhusishwa kwake na upatikanaji wa jino la tembo wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Shirika la Hifadhi za Taifa kupitia taratibu za utendaji kazi lilipokea taarifa za kintelijensia tarehe 14.05.2016 zikimhusisha mwananchi mmoja mkazi wa Ngarenanyuki, Arumeru Emmanuel Nassari (46) ambaye ni Mchungaji wa Kanisa TAG kumiliki jino la tembo na kuwa alihitaji kupata mtu wa kufanya naye biashara. Baaada ya kupata taarifa hizi shirika liliwasiliana na Kikosi Kazi Maalum cha Kitaifa kinachohusika na masuala ya ujangili ili kushirikiana kwa ajili ya ufuatiliaji.

Kikosi Kazi hiki mara baada ya kupata taarifa hizi kiliendelea na taratibu zake za kiuchunguzi na baada ya ufuatiliaji walifanikiwa kumkamata Emmanuel Nassari tarehe 15.05.2016 akiwa na jino moja la tembo ambapo katika mahojiano yaliyofanyika alimhusisha Mhifadhi Mwandamizi wa TANAPA Genes Shayo kuwa anazo taarifa za yeye kuwa na jino hilo na hivyo kukamatwa tarehe 16.05.2016 kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Shirika la Hifadhi za Taifa linaendelea kutoa wito kwa raia wema wa nchi hii kuendelea kutoa taarifa za kufichua vitendo vya ujangili na kwamba halitasita kuchukua hatua stahiki kwa yeyote anayehusika na vitendo hivi ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wake watakaobainika kisheria kuhusika na vitendo hivi.

Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
S.L.P 3134
ARUSHA
Simu: +255 027 254 4082
Baruapepe: dg@tanzaniapaks.go.tz
Wavuti: www.tanzaniaparks.go.tz

23.05.2016


Comments