- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne akijibu
hoja na michango mbalimbali ya wabunge zilizoelekezwa kwenye wizara hiyo wakati
wa Majumuisho ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2016/2017
ambayo imetengewa kiasi cha shilingi
bilioni 135.7.
Baadhi ya wabunge wakimpongeza wa Maliasili
na Utalii Prof. Jumanne Maghembe mara baada ya Bajeti ya Wizara hiyo kupitishwa
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2016/2017 ambayo
imetengewa kiasi cha shilingi bilioni
135.7.
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof.
Jumanne Maghembe akimweleza jambo Mbunge wa Bunda mjini Mhe. Esther Matiku (CHADEMA) nje
ya ukumbi wa Bunge mara baada ya kupitishwa kwa Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Wizara hiyo kwa mwaka 2016/2017.
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof.
Jumanne Maghembe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji wa Wizara
ya Maliasili na Utalii bungeni mjini Dodoma.
Na Aron Msigwa - Dodoma.
Serikali imesimamisha utoaji wa vibali na uuzaji wa
wanyama hai kutoka katika hifadhi za Taifa kwenda nje ya Tanzania kwa kipindi
cha miaka 3 mpaka hapo itakapotangazwa tena.
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe
ametoa agizo hilo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu hoja na michango
mbalimbali ya wabunge iliyoelekezwa kwenye wizara hiyo wakati wa Majumuisho ya
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2016/2017 ambayo
imetengewa kiasi cha shilingi bilioni
135.7.
Prof. Maghembe ameiagiza Idara ya Wanyamapori ipange
na kuweka utaratibu mpya utakaotumika kusimamia biashara hiyo pindi
itakaporejeshwa tena baada ya kumalizika kwa muda wa zuio la Serikali la miaka
3 ikizingatia mazingira ya uhifadhi wa
wanyama hao.
USAFIRISHAJI WA WANYAMA HAI
NJE YA NCHI.
Amesema kumekuwa na taarifa za baadhi ya watanzania
wasio waaminifu ambao wamekua wakijihusisha na vitendo vya kusafirisha wanyama
hai waliokatazwa kinyume cha utaratibu jambo ambalo limeisababishia Serikali
ipoteze mapato kutokana na wanyama hao.
Akielezea kuhusu wanyama wanaoruhusiwa kusafirishwa nje ya nchi kama nyani,
Kenge,ndege, kobe, wadudu na tumbili amesema wanyama hao wamekuwa wakisafirishwa kinyume na utaratibu na baadhi ya
wafanyabiashara wasio waaminifu kwa ajili ya kutumiwa na makampuni ya kimataifa
kwenye shughuli za utafiti wa kisayansi wa tiba na chanjo.
Amesema makampuni hayo yamekuwa yakinufaika binafsi
kwa kupata fedha nyingi pindi yanapofanikiwa kupata chanjo au tiba husika huku
maeneo waliokotoka yakipata fedha kidogo jambo ambalo serikali ya awamu ya tano
imeamua kulifanyia kazi.
UTALII KUSINI MWA TANZANIA NA MAENEO MENGINE.
Amesema Serikali itatekeleza miradi mbalimbali ya
uboreshaji wa Utalii wa Kusini ili kuweka mazingira wezeshi na kuondoa vikwazo
vilivyokuwa vikisababisha watalii kushindwa kufika katika maeneo ya hifadhi za
Taifa eneo la ukanda wa kusini mwa
Tanzania.
Baadhi ya
maeneo yatakayoshughulikiwa ni gharama ya usafiri wa ndege kwenda na kurudi katika maeneo hayo kuwa
kubwa hadi kufikia Dola za kimarekani 1800 jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa
watalii hao.
Amesema Serikali itaanzisha vituo vya kuwekea mafuta
ya ndege mahali vilipo vivutio vya utalii ili kuziwezesha ndege ndogo kufika
kwa urahisi na kupata huduma ya kuongeza mafuta hivyo kupunguza gharama kwa
wasafiri wanaotembelea hifadhi za eneo hilo na ndege ambazo hulazimika kurudi jijini.
Aidha amesema katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali
itanunua ndege ndogo abiria ili kuwezeha
watalii kufika kwa urahisi katika maeneo ya hifadhiza Taifa.
UTAMBUZI WA MAENEO MAPYA YA UTALII.
Serikali kwa kushirikiana na Wakuu wa wilaya, mikoa na
Wabunge itaanzisha mpango mpya kuviorodhesha vivutio vyote vya utalii vilivyo
katika maeneo yao ili viweze kutangazwa ipasavyo na kuongeza kuwa mara baada ya
kukamilika kwa mpango huo itaandaliwa orodha ya vivutio hivyo ili vianzwe
kutangazwa rasmi.
Katika kuimarisha shughuli za utalii nchini serikali
itaweka mkazo katika uimarishaji wa utalii wa utamaduni, uimarishaji wa maeneo
ya historia na Malikale ili kuwezesha eneo hilo kuchangia zaidi katika pato la
taifa.
ULINZI NA USALAMA WA HIFADHI ZA TAIFA.
Prof. Maghembe ameeleza kuwa suala la ulinzi na
usalama wa hifadhi zote za Taifa liko kwa mujibu wa sheria na kubainisha kuwa
serikali imeanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA)
litakalochukua mbuga zote zilizokuwa na uongozi ambazo ziko nje ya TANAPA.
Jeshi hilo
litapambana kikamilifu na ujangili, kuimarisha maadili na nidhamu ya askari wa
ulinzi wa hifadhi za taifa pamoja na kushughulikia maslahi yao na kuondoa
migogoro kati ya askari na wananchi.
Amesisitiza kuwa mara baada ya Bunge la Bajeti, Wizara
itakutana na wahifadhi wakuu wote ili kuweka vigezo vya kuzingatia katika
majukumu yao na kusisitiza kuwa wahifadhi wote watakaoshindwa kwenda na kasi ya
vigezo vilivyowekwa hawatajumuishwa kwenye jeshi hilo.
Aidha, amekemea vikali vitendo vinavyofanywa na baadhi
ya askari wa hifadhi kupiga raia na kuchoma nyumba za wananchi kuwa
havikubaliki na ni kinyume cha majukumu yao.
" Nimesikiliza kwa makini michango ya wabunge na
nimesikia wafanyakazi katika hifadhi zetu wanapiga raia wanaua mifugo na kuchoma
nyumba za wananchi jambo ambalo halikubaliki, hatukuwatuma kufanya hivyo"
Amesisitiza Prof.Maghembe.
MIGOGORO YA MIPAKA MAENEO YA HIFADHI.
Serikali imesema mpaka sasa kuna migogoro ya ardhi
281, kati ya hiyo 35 ambayo ni sawa na asilimia 12.5 ni migogoro ya hifadhi na
kuita Mikoa yenye migogoro hiyo kuwa ni
pamoja na Mara , Tanga na Kagera inachukua jumla ya asilimia 50.
Aidha, amesema kuwa mkoa wa Tabora unaongoza kwa kuwa
na eneo kubwa la ardhi na unaongoza kwa kuwa na migogoro mingi ya hifadhi kwa
asilimia 40.
Katika kuishughulikia migogoro hiyo Serikali
imeziagiza wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maji na Umwagiliaji,
TAMISEMI, Nishati na Madini, Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira pamoja na
Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana pamoja katika kutatua migogoro yote
ya ardhi nchini.
UBORESHAJI WA MAENEO YA HIFADHI NA MAMLAKA ZA
UHIFADHI.
Amesema katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 kiasi cha
shilingi bilioni 1 kimetengwa kushughulikia usafi wa mazingira na ujenzi wa
vyoo vya kisasa katika hifadhi ya mlima
Kilimanjaro vitakavyokuwa na uwezo wa kugeuza maji taka kuwa poda ili kuweka
mazingira yote ya mlima huo kuwa safi.
Aidha,amesema kuwa Mamlaka za hifadhi za Taifa
zimeendelea kuchangia katika maendeleo ya wananchi katika maeneo mbalimbali
nchini ikiwemo ujenzi wa madarasa, miundombinu ya barabara, utoaji wa madawati
katika halmashauri mbalimbali nchini.
Comments
Post a Comment