- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Dk. Robert Malima akitoa maelezo ya namna watafiti wanavyofanya utafiti na kuwakusanya mbu katika chumba maalum cha kufanyia utafiti kwa waandishi wa habari kutoka Kituo cha Waandishi wa Habari wa Kimataifa (ICFJ) na Taasisi ya “Malaria No More” kutoka nchini Marekani walipotembelea Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) cha Amani mkoani Tanga kujionea namna Tanzania inavyopambana na ugonjwa huo.
Watafiti wakiweka vitambaa vyenye viatilifu kwenye nyumba. Kitambaa hiki hudumu Kwa miaka 3 hadi 4 vikifanya kazi ya kuuwa mbu.
(PICHA NA ELEUTERI MANGI-MAELEZO)
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
“SAFARI moja huanzisha nyingine” na “Safari ni
hatua”, hii ni misemo inayoonesha ili kufika hatua fulani katika maisha ni
lazima kuanza na hatua ya moja inayopelekea hatua nyingine kufuata na kundelea
hadi utakapofikia malengo uliyojiwekea.
Juhudi za kufikia malengo haijalishi zinanzia
wapi, kwani kila mtu anakipaji ambacho ni tofauti na cha mwengine, lengo ni
kupambana na changamoto zinazoikabili jamii na kuzipatia majawabu.
Kulingana na historia, neno adui si geni kwa
Tanzania kwani Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema miongoni mwa
maadui wanaolikabili taifa aliloliongoza ni magonjwa.
Tanzania ikiwa miongoni mwa mataifa ya dunia hii
na taifa lililo kusini mwa Jangwa la Sahara, halikwepi magonjwa abayo husababishwa
na mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo malaria.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za Shirika la
Afya Duniani (WHO) malaria ni ugonjwa hatari unayosababisha vifo vya watu wengi
duniani na unawaathiri akinamama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka
mitano.
Ndiyo maana Wataamu wa masuala ya afya
wanasisitiza kuwa kila mtu anatakiwa kuchua tahadhari ili kupunguza idadi ya
vifo vinavyoweza kuzuilika kwa kufuata kanuni za afya na maelekezo ya kitabibu
kama yalivyotolewa na watoa huduma ya afya.
Ili kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa la mfano
duniani katika kupambana na adui malaria wataalamu wa afya nchini wanaendelea
kunoa vichwa vyao kuhaikikisha wanapunguza au kumaliza tatizo la malaria
linaloathiri watu wa rika zote ambao ni nguvu kazi ya taifa la sasa na lijalo.
Hadi sasa Tanzania imefanikiwa kuanza kufanya
majaribio na kuwa nchi ya kwanza duniani kupambana na mbu waenezao magonjwa
mbalimbali ikiwemo malaria kwa kutumia kitambaa kilichowekewa viatilifu ili
kudhibiti mbu waenezao ugonjwa malaria ambao ni tishio kwa afya ya wananchi
wengi wanaoishi vijijini.
Hatua hiyo ya utafiti imefikiwa na watafiti wa
magonjwa ya Binadamu katika kituo cha Taifa cha Magojwa ya Binadamu (NIMR) cha
Amani mkoani Tanga hatua ambayo imeanza kuonesha matunda kwa kuweza kuwadhibiti
mbu waenezao ugonjwa huo.
Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu
(NIMR) cha Amani mkoani Tanga Dkt. William Kisinza aliwadhihirishia Waandishi wa Habari wa Kimataifa (ICFJ) na
Taasisi ya “Malaria No More” kutoka nchini Marekani walipotembelea kituo hicho hivi
karibuni na kuwadhihirishia kuwa hatua hiyo iliyofikiwa na watafiti hao
inaridhisha na inaendelea vizuri katika kupambana na ugonjwa huo.
Katika kufanikisha majaribio hayo, Dkt. Kisinza aliwaambia
waandishi hao wa habari kuwa kituo hicho kinaendelea vizuri na majaribio ambapo
wanatarajia kufanya mchanganuo wa utafiti huo mwishoni mwa mwaka 2016 na
taarifa kamili itatolewa rasmi mwaka 2017 ili viatilifu hivyo viweze kutumika
nchi nzima hatua itakayosaidia kuwapunguzia adha Watanzania ili waweze kutumia
muda mwingi kuzalisha mali badala ya kutumia muda mwingi kuhudumia wagonjwa wa
malaria.
Tanzania likiwa taifa linalojali masuala ya
ushirikiano na mataifa au taasisi nyingine duniani na kuthamini nafasi ya
washirika hao, inapelekea kuamini kuwa taifa haliwezi kusonga mbele peke yake,
juhudi za mataifa na taasisi nyingine zinahitajika katika kufikia mafanikio
hayo.
Ndio maana waswahili husema “Umoja ni nguvu
utengano ni udhaifu”, hiyo haikuwa shida kwa NIMR, Dkt. Kisinza anasema kuwa
mafanikio ya taasisi yake yanayohusisha majaribio hayo ya kudhibiti mbu
waenezao nmalaria yanatokana na ushirikiano mzuri uliopo na taasisi nyingine za
kitaaluma ndani na nje ya nchi.
Miongoni mwa taasisi hizo ni Chuo Kikuu cha Afya
cha Kilimanjaro (KCMC), Kituo cha Kudhibiti Kuzuia na Magonjwa cha Marekani
(CDC), Taasisi ya Tiba, Dawa na usafi wa mazingira ya London nchini Uingereza
(LSHTM) na Chuo Kikuu cha Brandeis cha nchini Marekani.
Juhudi za Serikali kupitia tasisi ya Amani na washrika
zimekuwa ni nyota njema inayosaidia kupelekea mafanikio ya kupunguza maambukizi
ya malaria nchini.
Takwimu zinaonesha kuwa malaria bado ni tatizo kubwa
nchini katika maeneo ya vijijini ikilinganishwa na maeneo ya mjini ambapo
maambukizi maeneo ya vijijini ni asilimia 10.7 na mjini ni asilimia 3.4
Tofauti hiyo inaonesha kuwa maambukizi ya malaria
yamepungua kwa asilimia 50 kutoka asilimia 18 mwaka 2007/2008 hadi asilimia 10
mwaka 2011/2012.
Katika kuonesha Serikali ipo mstari wa mbele
katika kupambana na adui malaria, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia
Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alipokuwa akitoa tamko wakati wa kilele cha Siku
ya Malaria Duniani mjini Dodoma Aprili 25 mwaka huu alisema kuwa Tanzania
inafanya kila juhudi kuhakikisha maambukizi ya malaria yanapungua hadi asilimia
5 mwaka 2016 na asilimia 1 ifikapo mwaka 2020.
Kituo cha Utafiti cha Amani mkoani Tanga kimeanza
kwa vitendo kuonesha matumaini hayo na kuunga mkono juhudi za Serikali ambapo Mtafiti
Mkuu anayesimamia zoezi la majaribio ya kuweka vitambaa vyenye viatilifu
vijulikanavyo kama “insecticide treated wall liners”, Dkt. Joseph Mugasa amesisitiza
kuwa zoezi hilo linahusisha vijiji 44 ambapo kaya zaidi ya 25,000 zipo kwenye
mradi na idadi ya watu wanaonufaika na majaribio hayo ni zaidi ya 100,000
katika maeneo mbalimbali ndani ya wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Mbali na kuangalia uwezo wa vitambaa hivyo, mradi
huo unaangalia pia uwezo wa vitambaa hivyo katika kukabiliana na upugufu wa
damu kwa watoto chini ya miaka 11, uwezo wa vitambaa kupambana na mbu sugu
kwenye viatilifu vingine na pia kufanya tathmini ya gharama anazoingia
mwananchi katika kugharamikia tiba za malaria.
Ili kupambana na mbu waenezao malaria katika
makazi ya watu, Kitambaa hicho huwekwa kwenye kuta za nyumba kwa ndani kitatumika
sambamba na chandarua ili kuweza kutoa kinga madhubuti mara mbili kumkinga
binadamu dhidi ya mbu waenezao magonjwa.
Mradi huo wa majaribio ya kutokomeza ugonjwa wa
malaria nchini umeanza kufanyiwa utafiti nchini miaka mtatu iliyopita kuanzia
2013 na unafadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) chini ya Mpango
wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Malaria (PMI) ambao hadi kukamilika kwake
utarajiwa kugharibu zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 3.
Meneja wa Mawasiliano Taasisi ya “Malaria No More”
ya nchini Marekani Dena Gudaitis ambaye pia alikuwa Mkuu wa msafara wa
waandishi hao waliokuja Tanzania waliofanya ziara kujionea namna Tanzania
inavyopambana na malaria kuanzia Mei 9 hadi 13 mwaka huu amesema kuwa Tanzania imeonesha
nia ya dhati katika kusimamia afya za wananchi wake hasa wale wa kipato cha
chini ambao wengi wao wanaishi vijijini.
Aidha, Rais Mstaafu Awamu
ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete ambaye ni
mshindi wa tuzo ya “White House Summit Award” aliyoipata mwezi Aprili mwaka huu
inaudhihirishia Ulimwengu akiwa madarakani alitumia hekima na busara katika
mapambano dhidi ya malaria kupitia kampeni mbalimbali ikiwemo “Zinduka Maleria
haikubaliki”
aliyoizindua February 13, 2010
zilionesha ujasiri wake wa kupambana na ugonjwa wa malaria nchini.
Ni dhahiri tuzo hiyo
aliyopewa Dkt. Kikwete imetokana na kutambua jitihada na kuthamini mchango wake
ambao yeye ni miongoni mwa waasisi walioasimamia uanzishwaji wa Muungano wa Viongozi
wa Afrika katika mapambano dhidi ya malaria (ALMA), muungano ambao hadi sasa
una viongozi 49.
Hatua ya iliyofikiwa na Tanzania kupitia kituo cha
Amani kufanya majaribio ya utafiti katika ugonjwa wa malaria unaakisi taswira
ya hatua mbalimbali zinazoendelea duniani ambapo uhalisia unaonesha kuwa idadi
ya watu waliokufa kwa ugonjwa wa Malaria kimeshuka chini ya nusu milioni mnamo
mwaka uliopita.
Hatua hiyo inaonesha mafanikio makubwa yanayofikiwa
na nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara dhidi ya ugonjwa huo unaoenezwa na
mbu.
Ripoti mpya ya Shirika la Afya Ulimwenguni
inaonyesha kuwa vifo vilivyotokana na ugonjwa wa Malaria vimeshuka hadi 438,000
mnamo mwaka 2015, ikiwa ni idadi ndogo ikilinganishwa na mwaka 2000, ambapo
watu 839,000 waliuawa na Malaria.
Aidha, WHO inaeleza katika ripoti yake kuwa katika
muda wa miaka 14 iliyopita, mikakati ya kupambana na ugonjwa huo katika nchi
nyingi za Afrika, ikiwemo matumizi ya vyandarua wakati wa kulala na kupuliza
dawa ya kuuwa wadudu nje na ndani ya nyumba imeokoa mamilioni ya maisha ya watu
na fedha nyingi ambazo zinaweza kutumiwa kuwatibu wagonjwa wengine.
Ni dhahiri zaidi ya asilimia 35 ya vifo vyote vinavyotokana
na Malaria ulimwenguni vinatokea katika nchi mbili za Kiafrika ambazo ni Nigeria
na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hatua hiyo imepelekea Shirika la Afya Ulimwenguni
kujiridhisha kuwa katika mwaka wa 2013, zaidi ya watu milioni 198,
waliambukizwa ugonjwa wa malaria na ambapo imekadiriwa watu 584,000 walikufa
kutokana na ugonjwa huo.
Taswira hiyo inaonesha karibu watu 4 kati ya 5
waliokufa ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Ugonjwa huo unatishia
mamia ya nchi na maeneo mbalimbali ulimwenguni, na watu bilioni 3.2 wanakabili
hatari ya kuambukizwa.
Tanzania ikiwa mojawapo ya nchi zilizo Kusini mwa
Jangwa la Sahara, imejiwekea mikakati ya kuudhibiti ugonjwa huo inayotekelezwa
na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Mikakati hiyo ni kutumia viandarua vyenye
viatilifu vya muda mrefu, kusafisha mazingira na kuua viluwiluwi vya mbu kwa
kutumia viuadudu vya kibailojia katika maeneo ya mijini, unyunyiziaji wa viatilifu
ukoko katika kuta za ndani ya nyumbaambao unatekelezwa katika baadhi ya wilaya
za mikoa ya Kanda ya Ziwa zenye maambukizi makubwa ya malaria.
Zoezo hilo la dawa ya ukoko limefanyika katika
halmashauri nane za mikoa ya Musoma, Butiama, Ngara, Misenyi, Kwimba, Bukoba
Vijijini Chato na Sengerema ambapo jumla ya kaya 459,212 zimepuliziwa viatilifu
hivyo na kukinga takribani jumla ya wakazi 2,296,260.
Mikakati mingine ni kuendelea na uchunguzi na kutoa
matibabu ya ugonjwa wa malaria mara unapogunduliwa kwa wagonjwa, kuongeza kasi
ya upimaji kwa kutumia kipimo kinachotoa majibu haraka (MRDT) ndani ya dakika
15 au kwa kutumia hadubini na kutumia dawa sahihi kulingana na maelekezo ya
daktari na mtoa huduma.
Hatua hiyo ya kuboresha vipimo kwa kutumia MRDT
Mtaalamu wa Maabara kutoka Zahanati ya Ithna-Asheri iliyopo jijini Arusha
Apolinary Mushi anasema kuwa ni kizuri na kinaweza kutumiwa katika mazingira
yeyote nchini mijini na vijijini.
Kwa mujibu wa tamko la Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alilolitoa mjini Dodoma wakati
wa kilele cha maadhimisho ya siku ya malaria duniani, Serikali inaendelea kuwapatia
utaalamu wataalamu ili waweze kujengewa uwezo na weledi katika kutekeleza
majukumu kulingana na taaluma yao.
Hatua hiyo ya Serikali itaendelea kusaidia kuboresha
ongezeko la upimaji wa malaria nchini kufikia asilimia 83 ambapo kiwango hicho cha
upimaji kinazidi lengo ambalo Serikali imejiwekea la angalau asilimia 80.
Akiwasilisha taarifa ya namna Tanzania
inavyopambana na kudhibiti magonjwa mbalimbali wakati wa mkutano wa 69 wa afya
duniani unaofanyika Geneva nchini Uswisi hivi karibuni, Waziri Ummy amesema
kuwa Tanzania imeweza kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria kutoka
asilimia 18 hadi 9.5 kwa Tanzania bara na kwa upande wa Zanzibar imefanikiwa
kupunguza idadi ya wagonjwa hadi kufikia asilimia 0.6 .
Juhudi zinazofanywa na Serikali katika kujali na
kusimamia afya za watu wake zinapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania kwa
nafasi yake ili kutokomeza ugonjwa wa malaria ambao ni hatari kwa maendeleo ya
jamii na taifa kwa ujumla.
Shime Watanzania, tukumbuke Zama zimebadilika,
“Sio kila homa ni malaria nenda ukapime” na “lala kwenye chandarua kila siku”
kujikinga na malaria, kumbuka Tanzania bila malaria inawezekana.
Comments
Post a Comment