Featured Post

YANGA, KUFIKA KILELENI MBONA RAHA!

Na Waandishi WetuYanga  imehitimisha mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara ikiwa kileleni baada ya jana Oljoro JKT 'kukubali kutii sheria bila shuruti' kwa kuruhusu mabao 3-0 kuzama kimyani, wakati huo Azam FC ikilazimishwa sare ya 3-3 dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.
Katika mechi ya Yanga dhidi ya maafande hao iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, mapema Simon Msuva aliifungia timu hiyo mwenyeji bao la utangulizi dakika ya 23 akimalizia kwa kichwa krosi murua ya kiungo Mrwanda Haruna Niyonzima 'Fabregas'.
Nusu saa ya mchezo, winga hatari aliye katika kiwango cha juu, Mrisho Ngasa alipachika bao la pili la Yanga kwa shuti la umbali wa takriban mita 35 lililokwenda moja kwa moja langoni mwa Oljoro.
Bao hilo lillilozifanya timu hizo ziende mapumziko huku matokeo yakisomeka 2-0, lilimfanya mchezaji huyo wa zamani wa Kahama United, Kagera Sugar, Azam FC na Simba afikishe mabao sita na pasi za mwisho sita katika michezo nane aliyokichezea kikosi cha 'Wanajangwani' hao msimu huu tangu arejee kutoka kifungo cha michezo sita.
Mtokea benchi, Jeryson Tegete aliiandikia Yanga bao la tatu akiitendea haki pasi murua ya Ngasa katika dakika ya 53.
Ngasa alilimwa kadi ya njano baada ya kumcheza rafu Hamis Salehe dakika 51 huku Said Bahanunzi pia akionyeshwa kadi ya njano katika dakika ya 82.
Kwa upande wa mashabiki wa Yanga walionekana kushangilia matokeo ya Chamazi wakati timu yao ikitoka kwenye Uwanja wa Taifa na ushindi wa 3-0.
Baada ya mchezo huo, Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts alisema kikosi chake kilichokuwa na majeruhi wengi kitakuwa imara zaidi mzunguko wa pili na anaamini hakuna timu itakayowatoa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.
"Ni jambo jema tumepata ushindi leo (jana) huku tukifurahia matokeo ya Azam dhidi ya Mbeya City. Kikosi chetu kina wachezaji kadhaa ambao ni majeruhi lakini tumefanya kazi nzuri," alisema Brandts.
Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 28 ikifuatwa na Azam FC yenye pointi 27 sawa na Mbeya City lakini ikikizidi kikosi hicho cha Juma Mwambusi kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Yanga: Deogratius Munishi, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Simon Msuva, Frank Domayo/ Lusajo Reliants, Mrisho Ngasa, Hamis Kiiza/ Hamis Kiiza na Haruna Niyonzima/ Said Bahanunzi (dk 79).
Oljoro JKT: Damas Malipesa, Majaliwa Mbaga, Yusuph Machogote, Shaibu Nayopa, Nurdin Seleman, Expedito Kiduko, Swalehe Idd, Issa Kandulu, Babu Ally na Sanu Mwaseba.

Uwanja wa ChamaziAzam walipata bao la kuongoza dakika ya 13 kupitia kwa Mkenya Humphrey Mieno aliyejitwisha kichwa mpira wa faulo uliyochongwa na Farid Maliki. Refa Dominick Nyamisana kutoka Dodoma aliamru faulo hiyo huku akimwonyesha kadi ya njano kipa David Burhan baada ya kuushika mpira nje ya eneo lake.
Dakika ya 30 Mwagane Yaye aliisawazishia Mbeya City akimalizia kwa kichwa mpira  uliochongwa na Deus Kaseke. Uwanja wa Azam (Azam Complex) uliopo Chamazi nje kidogo mwa jiji la Dar es Salaam ulikuwa umefurika mashabiki huku baadhi yao wakizuiwa kuingia licha ya kuwa na tiketi halali.
Yaye alirudi tena nyavuni dakika saba baada ya mapumziko akimalizia kwa kichwa kingine krosi ya Peter Mapunda lakini bao hilo lilidumu kwa dakika nane tu kabla ya mfungaji bora wa ligi hiyo msimu wa 2011/12, John Bocco 'Adebayor' kuisawazishia Azam kwa kichwa akiunganisha krosi safi ya mfungaji bora msimu uliopita Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast.
Kwa mara nyingine Yaye alirudi nyavuni  wakati huu alikamilisha hat-trick yake katika dakika ya 73 baada ya kumtoka beki Said Morad kabla ya kumchambua kipa Mwadin Alli na kuiandikia Mbeya City bao la tatu.
Iliwachukua dakika 10 tu Azam kusawazisha bao hilo kwani katika dakika ya 83 Hamis Mcha alitikisa nyavu za Mbeya City baada ya kumzunguka beki Yusuph Lulinda na kumchambua vyema kipa Burhan ambaye alikuwa kipa bora msimu uliopita akiwa na Prisons ya Mbeya.
Hata hivyo, mara baada ya mpira kumalizika, licha ya Yaye kuitwa na refa Nyamisana huku wengi wakitarajia kuwa ilikuwa ni kwa lengo la kuzawadiwa mpira kutokana na kufunga mabao matatu, hali haikuwa hivyo kwani aliishia kupongezwa kwa kupeana mikono.
Hiyo ni mara ya pili tukio kama hilo kutokea kwani katika mechi ya Simba dhidi ya Mgambo Shooting, Septemba 18, Amisi Tambwe alipiga hat-trick lakini naye akaambulia patupu.
Mchezaji pekee alifanikiwa kupewa mpira haaba ya kufumania nyavu mara tatu katika mechi moja alikuwa ni Abdallah Juma wa Mtibwa Sugar ambaye alifunga hat-trick wakati wakicheza dhidi ya JKT Oljoro.
Azam: Mwadini Alli, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Aggrey Morris, Said Morad, Kipre Bolou, Salum Aboubakar, Kipre Tchetche, John Bocco/ Joseph Kimwaga (dk 72), Humphrey Mieno na Farik Maliki.
Mbeya City: David Burhan, Hassan Mwasapili, Yusuph Lulinda, Deo Julius, Deus Kaseke, Antony Matogolo, Richard Peter, Paul Nonga/ Hamad Kibopile (dk 89), Steve Mazanda/ Alex Seth (dk 89), Mwagane Yaye na John Kabanda. 
Nayo Rhino Rangers ilishindwa kuutumia vema uwanja wao wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora baada ya kulazimishwa suluhu na Tanzania Prisons.
Azam na Mbeya City ndizo timu pekee zilizomaliza mzunguko wa kwanza bila kupoteza mchezo wowote. Mzunguko wa pili wa ligi hiyo utaanza Januari 25, mwakani.
CHANZO: NIPASHE

Comments