Featured Post

KILA KONA AZAM... MBEYA CITY

MECHI ya kufunga mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom iliyopigwa Chamazi Complex, Mbagala kati ya wenyeji Azam FC na timu gumzo, Mbeya City na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 jana iliwateka mashabiki lukuki.
Mapema mchana, mashabiki kutoka ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam, walionekana Barabara ya Kilwa wakielekea Chamazi, ambako ilikuja kuthibika wakati wa mchezo ambako walifurika uwanjani hadi wengine kusimama, jambo ambalo linaelezwa halijawahi kutokea tangu dimba hilo lianze kutumika.
Mpira ulianza kwa kasi na dakika ya 5, John Boko na John Banda waligongana na kuumia, ambako Boko alifungwa plasta kichwani na Banda juu ya jicho na kuendelea na mpira.

Walikuwa ni Azam FC walionza kujipatia bao dakika ya 13, likifungwa na Humphrey Mieno akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Farid Maliki, baada ya kipa wa City kupangua mpira nje ya eneo lake.
City wakishangiliwa kwa nguvu na mashabiki wao, walichomoa dakika ya 30, kwa bao la kichwa la Mwagane Yeya akimalizia kwa ustadi, krosi ya Deus Kaseke. Mabao yaliyodumu hadi mapumziko.
Alikuwa Yeya tena dakika ya 55, alipofunga bao la pili kwa kichwa tena akiunganisha krosi ya Peter Mapunda, aliyeingia badala ya Richard Peter aliyeumia, kabla ya Boko naye kusawazisha kwa kichwa dakika ya 59, akiitumia vema krosi ya Kipre Tchetche.
Kama haitoshi, dakika ya 73, Yeya alipiga ‘hat trick’ baada ya kuifungia City bao la tatu akiyatumia vema makosa ya beki Said Morad, kabla ya dakika ya 83, Hamis Mcha ‘Viali’ aliyeingia badala ya Boko kuisawazishia Azam FC baada ya kuwachambua mabeki wa City.
Mara baada ya mchezo kumalizika, Kocha wa Azam FC, Stewart Hall, aliwapungia mikono ya kwa heri mashabiki.
Akizungumza na Tanzania Daima, Hall alibainisha kuwa, amepata ulaji sehemu hivyo jana ilikuwa mechi yake ya mwisho na Wana lambalamba hao. Hata hivyo, habari kutoka ndani ya timu hiyo zinaeleza kuwa kumetokea kutoelewana kisera, jambo lililosababisha waachane na kocha huyo raia wa Uingereza.
Kwa matokeo hayo, wakali hao waliokuwa wakiongoza ligi kwa muda mrefu, Azam FC na Mbeya City zilizokuwa na pointi 26, zimefikisha pointi 27 na kukamata nafasi ya pili na tatu.
Azam FC: Mwadini Ali, Erasto Nyoni, Wazir, Aggrey Morris, Said Morad, Kipre Balou, Kipre Tchetche, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Boko, Hamphrey Mieno, Farid Maliki.
Mbeya City: David Baruani, John Kabanda, Hassan Mwasa, Deo Julius, Yusuf Abdallah, Anthony Matogoro, Mwagane Yeya, Steven Mazanda, Paul Nonga, Deus Kaseke, Richard Peter.
Kwenye dimba la Taifa, Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga walimaliza mzunguko wa kwanza kwa kishindo baada ya kuibugiza JKT Oljoro ya Arusha mabao 3-0 na kukaa kileleni. Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 28 ndani ya mechi 13.
Katika pambano hilo ambalo lilishuhudiwa na mashabiki wachache tofauti na ilivyozoeleka Wana Jangwani wanaposhuka katika dimba hilo, kutokana na kudaiwa wengi kwenda Chamazi Complex kuzishuhudia Azam FC na Mbeya City, Yanga ilianza kujipatia bao dakika ya 23 likifungwa Simon Msuva kwa kichwa akiitendea haki krosi safi ya Haruna Niyonzima, kabla ya Mrisho Ngasa kufunga la pili dakika ya 30 na Jerry Tegete kuhitimisha la tatu dakika ya 53.
Yanga: Deo Munishi, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Canavaro’, Kelvin Yondani, Athumani Idd ‘Chuji’, Simon Msuva, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Hamis Kiiza, Haruna Niyonzima.
JKT Oljoro: Damas Kugesha, Paul Malipesa, Majaliwa Mbaga, Yusuph Machogote, Shaibu Nayopa, Nurdin Selemani, Expedito Kiduko, Swaleh Idd, Issa Kanduru, Babu Ally, Sanu Mwaseba.
CHANZO; TANZANIA DAIMA

Comments