- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
John Bosco, nyanda wa Simba.
Na Daniel Mbega
SIMBA, siyo tu kwamba iliokoka na kuteremka daraja msimu huo ukiwa ni msimu wa pili mfululizo kunusurika, bali ushindi wao wa magoli 2-1 dhidi ya mahasimu wao wakubwa, Yanga Jumamosi Julai 23, 1988 mwaka huo kwenye Uwanja wa Taifa uliifanya ilinde hadhi yake. Mchezo huo ulikuwa ni wa marudiano wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, ambapo katika mchezo wa kwanza timu hizo zilifungana 1-1.
Kwa Coastal Union kuchapwa magoli 2-0 na African Sports siku hiyo, Yanga ilihitaji sare tu ili iweze kutetea ubingwa wake, lakini timu ya Tanga pamoja na kipigo hicho ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa tofauti ya idadi ya magoli ya kufunga. Yanga na Coastal zilikuwa na pointi 26 kila moja, lakini Coastal ilikuwa na magoli 27 na Yanga ilikuwa na magoli 24.
African Sports ilishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 26 pia lakini ilikuwa na magoli 23 ya kufunga. Timu hii, hata hivyo, iliingia kwenye Ligi Kuu ya Muungano na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Tanzania nzima mwaka huo. Simba ilikuwa ya tatu kutoka mwisho ikiwa na pointi 20.
Baada ya John Makelele kufunga goli la ushindi mapema katika kipindi cha pili, Yanga ilishindwa kuuvunja ukuta wa Simba. Mashabiki wa Simba walikuwa na furaha kubwa jioni hiyo, kwani kwa msimu wote hawakuwa na imani kama timu yao ingeweza kunusurika isishuke daraja.
Siku hiyo vijana hao wa Msimbazi walionyesha mpira mzuri na ari ya ushindi ilikuwepo tangu mwanzo. Yanga ilichanganyikiwa sana siku hiyo baada ya kutamba kwamba wangeifunga Simba kwa kuwa timu hiyo msimu huo ilikuwa dhoofulhali, lakini wakajikuta wakiwa katika wakati mgumu sana.
Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana 1-1, kama walivyofanya katika mchezo wa kwanza Aprili 30, mwaka huo. Kama ilivyokuwa katika mchezo wa kwanza, Edward Chumila tena ndiye aliyeanza kufunga goli la Simba katika dakika ya 21. Malota Soma alimhadaa mlinzi wa Yanga kwenye wingi ya kulia na krosi yake ilisogezwa kidogo tu na walinzi wa Yanga na hivyo kumwezesha Chumila kufunga kirahisi baada ya kufumua shuti kali mara mpira ulipodunda.
Dakika tisa baadaye mwamuzi Msafiri Mkeremi aliinyima Simba penati ya wazi baada ya Godwin Aswile wa Yanga kuunawa mpira huo ndani ya eneo la hatari. Badala yake Mkeremi akaamuru ipigwe ‘free - kick’ kuelekea goli la Simba, huku mashabiki wa Simba wakiwa hawaamini.
Mpaka wakati huo Yanga haikuonyesha kama ilikuwa inajiamini na mara nyingi ilikuwa ikitumia mbinu za kuotea kuwavunja nguvu washambuliaji wa Simba. Katika dakika ya 36 Yanga ilifanikiwa kusawazisha goli hilo kupitia kwa nahodha Issa Athumani aliyemzidi ujanja Mkandawire kabla ya kuunganisha wavuni kwa kichwa krosi ya Athumani China. Mkandawire akabaki chini amelala asiamini yanayotokea langoni mwake.
Bao hilo liliwapa imani Yanga na mchezo ungeweza kuwa hivyo kama siyo makosa ya kipa Sahau Kambi wa Yanga yaliyowapa ushindi Simba katika dakika ya 58. Kambi aliuona mpira wa kichwa wa Malota Soma hauna madhara sana, akaudharau, lakini ghafla akatokea Makelele aliyeukwamisha wavuni kabla haujamfikia kipa huyo.
Pamoja na jitihada zote, ngome ya Simba ikawa makini zaidi kulinda bao lake. Mwamuzi Msafiri Mkeremi kutoka Tabora hakuweza kutoa hata kadi moja katika mechi hiyo.
Mgeni rasmi katika pambano hilo alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Salim Ahmed Salim. Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Spika wa Bunge, Chifu Adam Sapi Mkwawa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Utamaduni na Michezo, Zahra Nuru na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo (BMT), Hamza Kasongo. Jumla ya watazamaji 30,000 walihudhuria pambano hilo.
YANGA: Sahau Said Kambi, Fred Felix/Yusuf Bana, Kenneth Mkapa, Godwin Aswile, Lawrence Mwalusako, Athumani China/Abdallah Burhani, Justin Mtekele, Said Mwamba ‘Kizota’, Issa Athumani, Dennis Mdoe na Celestine Mbunga.
SIMBA: John Bosco, Raphael Paul, Twaha Hamidu, Deo Njohole ‘OCD’, Pazi Ally, Daniel Muhoja, John Makelele, Adolf Kondo/Francis Mwikalo, Edward Chumila na Augustine Haule.
NB: Makala haya ni kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘MIAKA 50 YA UBINGWA WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za mwisho kuchapishwa. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu +255 787 426161 au brotherdanny5@gmail.com.
Comments
Post a Comment