- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Rais wa Sudan, Jenerali Gaafar Mohamed el-Nimeiry akisalimiana na wachezaji wa Taifa Stars. Hapa anasalimiana na Hassan Gobbos 'Wa Morocco' na kushoto kabisa ni beki mstaarabu Mohammed Chuma. Anayemtambulisha kwa wenzake ni nahodha wa Stars Abdulrahman Juma. Mwingine pichani ni Kitwana Manara na anayeonekana uso wake ni Abdallah Kibadeni.
Na Daniel Mbega
KATIKA historia ya soka Tanzania kuna mambo ya kufurahisha kutokana na matoeo ya timu zetu uwanjani kama kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 1980 na kuna mambo ya kusitikisha kama Simba kushindwa kutwaa Kombe la CAF mwaka 1993.
Hata hivyo, kuna mambo ya kufedhehesha ambayo hayasimuliki. Mambo haya, ni afadhali yatokee kwetu wenyewe, lakini yanapotokea mbele ya wageni aibu yake haifutiki kirahisi.
Tukio la Taifa Stars kucheza vifua wazi mbele ya marais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Jenerali Gaafar Mohamed el-Nimeiry wa Sudan mwaka 1972 lilikuwa na fedheha kubwa.
Ndiyo maana, waliokuwa kwenye jukwaa kuu waliwahi kunidokeza kilichotokea katika mzungumzo baina ya Mwalimu Nyerere na Nimeiry. Inaelezwa kwamba, baada ya timu kujipanga uwanjani huku wachezaji wa Taifa Stars wakiwa vifua wazi, Nimeiry alimtania Mwalimu na kusema: “Ndugu yangu, yaani umefilisika kiasi kwamba hata wachezaji wako hawana jezi?” Mwalimu naye akamjibu: “Wewe subiri, tutawafunga tu…” Ulikuwa ni mzaha, lakini naamini Mwalimu Nyerere na Watanzania kwa ujumla – japo hawakusikia mazungumzo hayo – walifedheheka mno.
Mechi hiyo iliyochezwa Julai 4, 1972 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Shamba la Bibi) ulikuwa wa kuadhimisha sherehe za Saba Saba ambapo timu kadhaa, ikiwemo Nigeria, zilikuwa zimealikwa.
Zamani ulikuwa ni utamaduni wa kawaida kwa timu za soka za taifa kualikwa kwenye sherehe mbalimbali za kitaifa kwa mataifa ya Afrika.
Kilichotokea siku hiyo, kwa mujibu wa waliokuwepo, ni kwamba mtu aliyekuwa amepewa dhamana ya kukaa na jezi alichelewa kufika uwanjani. Unajua zamani jezi za timu – iwe klabu au timu ya taifa – zilikuwa ni pea moja na alikabidhiwa mtu maalum kwa ajili ya kuzitunza. Mtu huyo alifika uwanjani wakati tayari mchezo ukiwa unaendelea, hivyo ikabidi abaki na furushi lake mpaka kipindi cha kwanza kilipomalizika. Stars waliingia uwanjani kipindi cha pili wakiwa wametinga jezi hizo.
Hata hivyo, katika mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Gration Matovu, Stars waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 ambayo yalipatikana kipindi cha pili kupitia kwa Gibson Sembuli (dakika za 65 na 68) na Abdallah Kibadeni 79.
Stars, ambayo ilikuwa inanolewa na Pak Jung Yang wa Korea aliyesaidiwa na Marijani Shaabani Marijani (kaka yake Marijani Rajabu Marijani kwa baba mkubwa na mdogo), siku hiyo iliwakilishwa na Omar Mahadhi, Juma Mzee, Mohammed Chuma, Hassan Gobbos, Omar Kapera (nahodha), Nassoro Mashoto, Abdallah Kibadeni, Abdulrahman Juma, Kitwana Manara, Willy Mwaijibe/Gibson Sembuli, Isihaka Marande/Muhaji Mwabuda, Kassim Manga.
Sudan yenye ilikuwa na wachezaji mahiri wakati huo kama Zughbeir, Kaunda, Gadaura, Najru, James, Mohsin, Bushara, Bushra, Isaid, Hasab, Dehiesh, Kamar.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuifunga Sudan kati ya mechi tatu walizopata kucheza. Mara ya kwanza walikutana kwenye Kombe la Saba saba Julai 5, 1964 mjini Dar es Salaam na Tanzania ikafungwa 3-1, bao la Tanzania lilifungwa na Abdulrahman Lukongo katika dakika ya 43 wakati yale ya Sudan yalifungwa na Abo Eskandar (dakika ya 15 na 78 kwa penati) na Tigani dakika ya 22. Siku hiyo Tanzania iliwakilishwa na Maganga, Mathias Samuel Kissa (nahodha), Hamisi Fikirini Nkwabi ‘Liston’, Mbwana Abushiri, Abdulrahman Lukongo, Chaki, Mtumwa Mgeni, Hamis Kilomoni, Abdullah Aziz.
Mara ya pili ilikuwa kwenye nusu fainali ya Kombe la Gossage Februari 21, 1967 ambapo Tanzania ililala kwa bao 1-0.
Kikosi cha Taifa Stars wakati huo kilikuwa imara kwani kiliweza kutoka suluhu na Nigeria Julai 6, 1972 katika mchezo mwingine wa Kombe la Saba Saba. Nigeria ilikuwa inafundishwa na Dan Anyim na ilikuwa na wachezaji hatari kama nahodha Godwin Achebe, Otarekhua, Olayambo na Mathias Obianika.
Huko nyuma Stars ilikuwa imezifunga Lesotho na Mauritius mabao 4-1 kila moja katika michuano ya awali ya Michezo ya Afrika (All African Games).
Fedheha kama hiyo ilijirudia tena Oktoba 9, 2010 wakati wa mechi kati ya Taifa Stars na Morocco kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa Afrika. Safari hii halikuwa suala la jezi, bali Rais Jakaya Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi alishikwa na fedheha pamoja na Watanzania wote baada ya nyimbo za taifa kushindwa kupigwa kwa maelezo kwamba CD za nyimbo hizo ‘ziligoma’.
Wakati watu wote wamesimama na timu zimejipanga kusubiri nyimbo za taifa kabla ya kuanza mchezo huo ambao Morocco ilishinda 1-0, hakuna kilichosikika, ghafla mashabiki wa Yanga wakaanza kuimba: “…Mungu Ibariki Yanga…”.
Hali hiyo ilifanya Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumsimamisha kazi msemaji wake, rafiki yangu Florian Kaijage, kwamba ndiye aliyepaswa kuhakikisha kila kitu kipo sawa. Akawajibishwa kwa makosa ya wengine.
Comments
Post a Comment