Featured Post

PUTIN: MASHOGA RUKSA KUJA OLIMPIKI YA KIPUPWE 2014


RAIS wa Russia Vladimir Putin amesisitiza kwamba wachezaji mashoga na wasagaji hawapaswi kuhofia jambo lolote wakati wa Michezo ya Olimpiki ya majira ya Kipupwe itakayofanyika Sochi, Russia.
Putin alimhakikishia Thomas Bach, mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC), kwamba wachezaji mashoga - na mashabiki - watakuwa salama.
Russia imekuwa ikishutumiwa kuhusiana na sheria mpya ya kupiga marufuku "propaganda za ushoga" kwa watu walio na umri chini ya miaka 18.
Lakini kusudio la kususia Michezo hiyo limeleta matokeo hafifu.
Kulikuwa na taarifa kwamba mashoga watakaotembelea huko wangeweza kushtakiwa nchini Russia, lakini Moscow imesema hilo halitatokea.
"Tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanamichezo, mashabiki na wageni wanakuwa salama na kufurahia Michezo ya Olimpiki bila kujali wanakotoka, rangi yao au hali yao ya kijinsia. Napenda kusisitiza hilo," rais Putin alimweleza Bach.
Lakini makundi ya kutetea haki za mashoga yameituhumu IOC kwa kushindwa kuibana Russia, ambayo imewekeza sana kwenye Michezo hiyo kuliko michezo mingine iliyopita.
Wakati wa ziara yake, Bach hakuzungumzia lolote kuhusu sheria hiyo mpya, akiwa anaangalia zaidi maandalizi ya Russia kwenye Olimpiki.
"Tuna uhakika kwamba Michezo itakuwa ya kiwango cha juu," alikaririwa na Reuters akisema.
Chini ya sheria hiyo mpya ya kupinga ushoga iliyopitishwa mapema mwaka huu, watu wanaoshiriki "mapenzi ya kinyume na utamaduni" watapigwa faini ya hadi Dola za Marekani 155 wakati maofisa watalipa mara 10 zaidi. Sehemu za biashara na shule zitatozwa faini ya Dola 15,500.
Wanaharakati wa nchi za Magharibi wamekasirishwa na hatua hiyo, hivyo kuwashawishi wanamichezo wagomee Michezo hiyo.
Baa za mashoga katika miji ya New York, London na kwingineko zimegoma kuuza kinywaji cha Vodka kutoka Russia.
Lakini kwa Warussia wengi, ambako ushoga uliharamishwa mwaka 1993, sheria hiyo haina matatizo kwao.
Kura za maoni za hivi karibuni zimeonyesha kwamba karibu nusu ya Warussia wanaamini kwamba jamii za mashoga na wasagaji hazipaswi kupewa haki sawa na watu wengine.
CHANZO: BBC

Comments