Featured Post

NYAMLANI ATOA AHADI TISA ZA KUMMALIZA MALINZI

MGOMBEA nafasi ya U-Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athuman Jumanne Nyamlani amezindua kampeni zake za kuwania ukuu wa shirikisho hilo akipambana na Jamal Malinzi. 
Akizindua kampeni zake jana jijini Dar es Salaam, Nyamlani aliweka wazi jinsi atakavyoendeleza mipango ya sasa ya TFF kwa kuwa alishiriki katika kuiandaa na kuipanga chini ya uongozi wa sasa wa Leodegar Tenga.
Nyamlani anaenda mbali zaidi kwa kuweka pia ahadi zake tisa za kutekeleza endapo atapewa ridhaa ya kuliongoza shirikisho hilo. Miongoni mwa ahadi hizo za Nyamlani ni pamoja na;

Moja: KUIMARISHA USIMAMIZI NA MENEJIMENTI YA SOKA KATIKA NGAZI ZOTE.
Nyamlani anasema akiwa rais wa TFF, kwa kushirikiana na viongozi wa klabu na vyama vya soka vya wilaya na mikoa pamoja na serikali ataimarisha usimamiaji na menejimenti ya soka katika ngazi zote kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa viongozi pamoja na kusimamia sheria na taratibu za uendeshaji wa soka Tanzania.

Mbili: RUSHWA KATIKA SOKA NCHINI.
Nyamlani anakiri kwamba kumekuwa na malalamiko na vitendo vya rushwa ambavyo vinawahusisha viongozi wa soka. Anasema kwa kushirikiana na serikali na viongozi wa soka katika ngazi zote atahakikisha anaendeleza mapambano dhidi ya rushwa katika soka nchini.

Tatu: KUKUZA SOKA LA WATOTO, VIJANA NA WATOTO.
Endapo Nyamlani atachaguliwa kuwa rais mpya wa TFF amesema atalipa uzito wa kipekee soka la watoto wenye umri chini ya miaka 16 na soka la vijana na kukuza vipaji (miaka 9-12, miaka, miaka 13-14, miaka 15-17 na miaka 18-21) pamoja na soka la wanawake. Kazi hii Nyamlani ataitekeleza kwa kuanzisha program mbalimbali za mashindano za kukuza vipaji kwa makundi haya ya vijana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa soka.

Nne: KUIMARISHA UWEZO WA RASILIMALI FEDHA WA TFF.
Nyamlani anasema akishinda nafasi ya U-Rais wa TFF atahakikisha shirikisho hilo linapata vyanzo endelevu na vya kuaminika vya fedha ili kujenga uwezo wa TFF katika kutekeleza mipango yake na kufikia malengo kikamilifu. Vilevile ataimarisha idara ya masoko ili kuweza kupata wadhamini zaidi na kuweza kuuza nembo za shirikisho hilo.

Tano: KUONGEZA IDADI NA UBORA WA WAAMUZI, MAKOCHA NA WATAALAM WA AFYA YA MICHEZO.
Nyamlani anasema atahakikisha kunakuwa na program endelevu ya mafunzo ya makocha, waamuzi na wataalam wa afya ya michezo ili kuongeza ufanisi wao katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazoongoza mchezo wa soka nchini na pia waweze kufikia viwango vya kimataifa vilivyowekwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Pia Nyamlani anasema atahakikisha anaweka msisitizo katika kuhamasisha watu wanaopenda soka na wenye uwezo wajiunge na katika fani hizo jambo ambalo litaongeza idadi ya wataalam hao.

Sita: KUONGEZA UBORA WA LIGI KUU, LIGI DARAJA LA KWANZA, LIGI ZA WILAYA NA MIKOA.
Anasema michuano ya Ligi Daraja la Kwanza, Ligi za Wilaya, Mikoa na Ligi Kuu ni ngazi muhimu ya kukuza soka katika nchi yoyote. Ni imani yake kwamba ligi hizo zikiimarishwa kwa kushirikiana na viongozi wa soka wa wilaya, mikoa na bodi ya kusimamia uendeshwaji wa ligi kuu Tanzania itaweza itaweza kuinua ubora wa soka na kufikia viwango vya kimataifa na kuweza kuhimili ushindani wakati wote.
Nyamlani anasema atashirikiana na viongozi wa soka na vyama vya kitaalam ili kuweza kuboresha kanuni mbalimbali zitakazowawezesha wachezaji vijana kuwa wachezaji wa kulipwa. Vile vile Nyamlani anasema atasimamia ipasavyo suala la malipo kwa klabu na vituo vya kukuzia vipaji pindi wachezaji wao wanapouzwa au kupanda viwango na kuwa wachezaji wa kulipwa.

Saba: KUONGEZA IDADI YA MAWAKALA.
Nyamlani ana imani kwamba ili mpira wa Tanzania ukue kwa kasi ni lazima tuongeze idadi ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi kwa kufanya hivyo ni lazima kuwa na mawakala wanaozingatia weledi na siyo uwakala wa kupeana kiholela huku wakishindwa kuuza hata mchezaji mmoja tangu mtu alipopewa kazi hiyo.

Nane: KUIMARISHA USHIRIKIANO WA SERIKALI NA TFF.
Nyamlani anasema atahakikisha anasimamia, kukuza na kuendeleza uhusiano uliopo sasa kati ya TFF na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kwamba jambo hili ni muhimu kwa ustawi wa soka Tanzania kwa sababu ni ukweli soka kwa sasa ni ajira rasmi kwa vijana ambao ndiyo nguzo ya taifa.

Tisa: KUIMARISHA USHIRIKIANO WA TFF, CAF NA FIFA.
Nyamlani anasema atahakikisha kuwa anakuza na kuendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya TFF na CAF na FIFA ili kuongeza kasi ya ukuaji wa soka nchini kufikia viwango vya kimataifa kwa kutumia misaada mbalimbali ya kitaalam na kifedha inayotolewa na taasisi hizo kubwa Afrika na duniani.

Comments