Featured Post

MALINZI ASAMEHE WAFUNGWA WA SOKA

Jamal Emil Malinzi ndiye Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Malinzi ameshinda wadhifa huo katika uchaguzi wa Kamati ya Utendaji ya TFF uliofanyika juzi (Oktoba 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Aliibuka na ushindi wa kura 73 dhidi ya mpinzani wake pekee Athuman Jumanne Nyamlani aliyepata kura 52. Nafasi ya Makamu wa Rais imetwaliwa na Wallace Peter Karia aliyepata kura 67 na kuwashinda Ramadhan Omari Nassib kura 52 huku Imani Omari Madega akipata kura sita.
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa, Rais Malinzi ametaka ushirikiano kutoka kwa wadau wote akiwemo mpinzani wake Nyamlani katika kuhakikisha mpira wa miguu nchini unasonga mbele.
Pia ametoa msamaha kwa watu wote waliokuwa wamefungiwa kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na TFF. Msamaha huo hauwahusu wale waliofungiwa kwa makosa ya rushwa au kupanga matokeo. Vilevile msamaha huo hauhusu adhabu zilizotolewa katika ngazi ya klabu.
Rais Malinzi pia amevunja kamati zote za TFF ambapo ataziunda upya kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji.
Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda ni Kalilo Samson (Kanda namba 1- Geita na Kagera) aliyepata kura 102 za ndiyo na 17 za hapana. Kanda namba 2- Mara na Mwanza, mshindi ni Vedastus Lufano aliyepata kura 51 dhidi ya Jumbe Odessa Magati (11), Mugisha Galibona (24), na Samwel Nyalla (39).
Epaphra Swai ndiye mshindi wa Kanda namba 3- Shinyanga na Simiyu kwa kura 63 dhidi ya Mbasha Matutu aliyepata 61. Kanda namba 4- Arusha na Manyara mshindi ni  Omali Walii Ali aliyepata kura 53 dhidi Elley Mbise (51), Ally Mtumwa (19).
Kanda namba 4- Kigoma na Tabora, mshindi ni Ahmed Idd Mgoyi aliyepata kura 92 dhidi ya 28 za Hamisi Yusuf Kitumbo.
Blassy Mghube Kiondo ameshinda Kanda namba 6- Katavi na Rukwa kwa kura 73 dhidi ya Ayubu Nyaulingo aliyepata 52. Ayoub Shaibu Nyenzi ndiye mshindi wa Kanda namba 7- Iringa na Mbeya kwa kupata kura 59 na kuwapiku David Samson Lugenge (8), John Exavery Kiteve (12) na Lusekelo Elias Mwanjala (46).
Kanda namba 8- Njombe na Ruvuma inawakilishwa na James Patrick Mhagama aliyepata kura 93 dhidi ya 31 za Kapteni mstaafu Stanley William Lugenge. Athuman Kingombe Kambi ndiye mshindi wa Kanda namba 9- Lindi na Mtwara kwa kura 84 akiwazidi Francis Kumba Ndulane (30) na Zafarani Mzee Damoder (11).
Hussein Zuberi Mwamba ametetea ujumbe wa Kanda namba 10- Dodoma na Singida kwa kura 63 akiwapiku Stewart Masima (58) na Charles Komba (4). Geofrey Irick Nyange ameshinda Kanda namba 11- Morogoro na Pwani akipata kura 78 dhidi ya Juma Pinto (26), Farid Nahdi (14), Riziki Juma Majala (5) na Twahil Twaha Njoki (2).
Kanda namba 12- Kilimanjaro na Tanga, Khalid Abdallah Mohamed ndiye aliyeibuka kidedea kwa kura 69 dhidi ya 54 za mpinzani wake Davis Elisa Mosha.  Kidao Wilfred Mzigama ameshinda Kanda namba 13- Dar es Salaam kwa kupata kura 60 dhidi ya wapinzani wake Muhsin Said Balhabou (50), Omar Isack Abdulkadir (10) na Alex Crispine Kamuzelya (4).

Comments