- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mzee Kungubaya akiwa na gitaa la galatone enzi hizo. Picha kwa hisani ya Kijiwe cha Kitime.
Na Daniel Mbega
Wakati umewadiwa
Wa salamu za wagonjwa
Hospitalini
Leo tunawapa pole x2
Ajuaye Bwana Mungu
Kwa mzima kuwa mfu
Mgonjwa kuwa salama
Leo tunawapa pole x2
Kipindi chenu kinawapa pole
Wote tunawapa pole
Mungu awajalieni pole x2
Tunawapa pole x2.
SWADAKTA kabisa. Hapana shaka yoyote kwamba, mashairi haya si mageni masikioni mwa Watanzania walio wengi, kwani ndiyo hufungua na kufunga kipindi cha saa nzima cha Ugua Pole, kilichobeba jina la wimbo huo, kinachosikika Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kila siku ya Jumapili kuanzia saa 4.02 asubuhi hadi saa 5.00.
Lakini pamoja na kufahamika kwa mashairi hayo hata kwa vijana wa kizazi cha leo, ni dhahiri kwamba si wengi wanaomfahamu mtunzi wa wimbo huo unaoendelea kutamba redioni mpaka leo.
Huyu si mwingine bali ni Omar Kungubaya, mkongwe wa muziki aliyedumu katika fani hiyo kwa zaidi ya miaka 50.
Kwa wale vijana wa zamani, yaani wa miaka ile ya '47, enzi ambazo nyimbo kama za 'Nina Mpenzi wangu Kibamba' zilikuwa zikitamba sana katika majukwaa ya muziki, basi watakuwa na kumbukumbu tosha ya mwanamuziki huyo mkongwe, ambaye hata hivyo, kama walivyo wengi wao, hakunufaika na lolote katika muziki.
Wapenzi wengi wa muziki wa dansi walishafikiria kwamba huenda mzee huyu alikwisharejesha namba kwa Mungu kutokana na ukimya wake wa muda mrefu katika majukwaa makubwa ya muziki, tofauti na wakongwe wengine ambao wanaendelea kuimba katika bendi zinazofufuliwa na kisha kuzikwa tena kutokana na kushindwa ushindani wa kibiashara.
Sijui kwa sasa mahali aliko, lakini nakumbuka nilikutana naye mwaka 2002 katika ukumbi wa Container Bar, Maili Moja Kibaha na kufanya mazungumzo naye, wakati akiishi Kibamba. Kama yu hai, basi wakati huu atakuwa na miaka 74.
Hata hivyo, staili aliyokuwa akiitumia wakati nakutana naye ni tofauti na ile ya zamani ya kuwa na bendi, kwani kila siku za wiki endi alikuwa anazunguka kwenye kumbi mbalimbali, baa na hata vilabu vya pombe za kienyeji akiwa na 'bunduki' yake, yaani gitaa aina ya galatone akiwaburudisha wateja waliokaa kwenye meza kwa ajili ya kustarehe.
Kwa upande wao, wateja nao huamua kumtuza chochote, lakini ilimuwia vigumu kuweza kuwashawishi ili wampatie fedha kutokana na nyimbo anazoimba.
Hali hiyo ilimfanya mwanamuziki huyo mkongwe awe akizunguka mpaka kwenye vilabu vya uchochoroni, hususan huko Kibaha-Maili Moja, ambako nilikutana naye.
Kwa ujumla, staili hiyo, inayojulikana zaidi kama 'Chuna Buzi', haikuwa ikimnufaishi chochote zaidi ya kumuwezesha kupata angalau senti kidogo kwa ajili ya mkate wake wa kila siku tofauti kabisa na mchango wake alioutoa katika jamii.
ALITOKA WAPI?
Mzee Kungubaya ni matunda mengine ya hazina isiyokwisha kutoka mkoa wa Morogoro, ambao umejaa vipaji vya kila aina. Alizaliwa mwaka 1939 katika Kijiji cha Mgaza Vigolegole, Morogoro, ambapo alipata elimu yake ya msingi (darasa la nane) Msamvu Middle School mwaka 1955.
Alishindwa kuendelea na masomo ya darasa la tisa kutokana na wazazi wake kushindwa kumlipia karo.
Historia yake kimuziki inaanzia mwaka huo wa 1955 akiwa shuleni Msamvu, ambapo wakati huo alikuwa na umri wa miaka 16 tu, na aliweza kuchaguliwa kuwa kiongozi wa bendi ya shule na mara baada ya kumaliza shule akajiunga rasmi na bendi ya Cuban Marimba iliyokuwa chini ya Salim Abdallah Yazidu 'Say'.
Itakumbukwa kwamba, bendi hiyo iliyokuwa na maskani yake Nunge Welfare (sasa eneo hilo linajulikana kama Mji Mpya), Morogoro ilikuwa tishio kwa bendi nyingi za Dar es Salaam na ndiyo iliyoibua vipaji vya wanamuziki wengi. Kwa sasa bendi hiyo imetoweka katika ulimwengu wa muziki.
Katika mahojiano maalum, Mzee Kungubaya alimtaja Kibwana Katashingo, aliyekuwa dereva wa marehemu Salim Abdallah na pia mpiga drum wa bendi hiyo, kwamba ndiye aliyekuwa mwalimu wake wa kwanza katika muziki wakati alipojiunga na Cuban Marimba, ambapo yeye Kungubaya alikuwa akipiga gitaa la galatone lenye nyuzi sita.
Mwaka 1960 Kungubaya alichanja mbuga na kuelekea Nairobi, Kenya kwa kile alichosema alikwenda kujiendeleza kimuziki.
"Huko nilipokelewa na wanamuziki wakongwe wakiwemo akina John Ondolo Chacha, John Mwale na David Amunga, ambao wote walikuwa wakikung'uta magiaa ya galatone kwenye vilabu mbalimbali jijini humo.
"Hata hivyo, mwaka uliofuata nilirejea Morogoro na kujiungan na bendi ya Kilosa Jazz iliyokuwa ikiundwa na akina Yahya Abbas na marehemu Abel Baltazar. Nilidumu na bendi hiyo hadi mwaka 1963," alieleza Kungubaya.
Alisema kwamba, aliamua kurejea tena Cuban Marimba, ambapo viongozi wa bendi hiyo wakampeleka kwa Mzee Mwaipungu aliyekuwa akiongoza bendi nyingine iliyokuwa tawi la Cuban Marimba, lakini mwaka 1969 akaondoka.
Safari hii aliamua kuyaweka kando masuala ya muziki na kuwa 'cashier' katika vituo vya kuuza mafuta vya Capital Esso Services kilichopo Mtaa wa India na baadaye kituo cha Agip Centre cha Mwembesongo. Hii ilikuwa mwaka 1970.
Alieleza kwamba, mwaka 1971 akaamua kurejea tena masuala ya muziki, ambapo mara hii alikuwa akijitegemea mwenyewe. Kama ilivyo ilivyokuwa wakati nakutana naye, alikuwa akipiga gitaa moja tu la galatone, ambapo alihamia Dar es Salaam na kuanza kutumbuiza katika baa moja iliyokuwa ikimilikiwa na Mama Hamm huko Tandale, Manzese.
Penzi, anasema, halina mipaka na halichagui fukara wala tajiri. Kwanini? Anasema kwamba, bosi wake huyo 'alimzimia' na kuanguka kwenye penzi.
"Hivyo nikaamua kumuoa mama huyo, ambaye hadi anafariki mwaka 1995 hatukubahatika kupata mtoto. Lakini mwaka 1974 tulinunua shamba kijijini Kwembe, na kuanzia hapo mpaka anafariki tulikuwa kijijini na ndiko ninakoishi mpaka sasa," alibainisha.
Mzee Kungubaya alisema kwamba, kabla mkewe huyo hajafariki alimpa ruksa ya kuoa mwanamke mwingine, ameoa, na wamebahatika kupata watoto watatu, ingawa mmoja alifariki.
ANAFANYA NINI SASA?
"Kama ujuavyo, hivi sasa nimekuwa mwanakijiji. Shughuli zangu ni za kilimo ingawa kwa kweli sina mtaji wa kutosha na mara nyingi natumia jembe la mkono," alisema.
Alisema ingawa yuko kijijini, lakini muziki kwa vile uko kwenye damu yake hawezi kuuacha, ndiyo sababu kila siku ya Ijumaa hadi Jumapili jioni alikuwa akionekana katika baa mbalimbali huko Kibaha-Maili Moja, akiwatumbuiza watu kwa kutumia gitaa lake la galatone alilolinunua miaka ya 1970.
Mara nyingi ungemkuta akiimba nyimbo nyingi zilizopata kutamba miaka ya 1960 hadi 1970, hususan nyimbo kama Mtoto si Nguo na Ndugu sikilizeni navunja vunja vikombe zilizoimbwa na Heorge Mukabi wa Kenya, na Wanawake wa Tanzania na Maneno madogo madogo kwa mabibi na mabwana zilizoimbwa na marehemu Salim Abdallah kule Cuban Marimba.
Wakati wa enzi zake alitunga nyimbo nyingi sana, lakini alisema kwamba, katika miaka 47 akiwa kwenye jukwaa la muziki hakunufaika na chochote zaidi ya kuishia kutumbuiza vilabuni!
Hata hivyo, aliitaka serikali kuweka utaratibu mzuri wa kuwajali wasanii wa zamani kwa kuwaenzi na ikibidi iwekwe siku maalum ya kuwakumbuka wakongwe wa zamani na kazi zao.
Aidha, alisema kwa kuwa Sheria ya Haki Miliki imekwisha pitishwa na serikali, basi ni vyema hata wasanii wa zamani wafikiriwe kupewe chochote na Radio Tanzania kutokana na kazi zao zilizohifadhiwa huko, ambazo sasa RTD (TBC Taifa) imekuwa ikiziuza.
Nipe maoni yako: brotherdanny5@gmail.com au 0787 426161
Comments
Post a Comment