Featured Post

KLABU 7 ZATAWALA UBINGWA WA SOKA TANZANIA BARA


Na DANIEL MBEGA
LIGI Kuu Tanzania Bara inaendelea kutimua vumbi katika harakati za kutafuta bingwa katika mwaka wake wa 49 tangu harakati za kutafuta klabu bingwa zilipoanza mwaka 1965.
Mikiki mikiki yote hii isingekuwepo leo kama lisingekuwa wazo la kocha wa Taifa Stars wa wakati huo, Milan Celebic wa Yugoslavia, alilolitoa mwaka 1964 kama njia ya kusaidia kuchagua wachezaji wa timu ya taifa badala ya kutegemea michuano ya Sunlight Cup (sasa Taifa Cup).
Badala ya michuano ya Sunlight iliyohusisha klabu na timu za Majimbo, Celebic aliona kulikuwa na umuhimu wa kuwepo mashindano ya klabu pekee katika ngazi ya taifa na siyo yale ya mkoa, hasa wa Pwani (Dar es Salaam ya sasa), hivyo ‘akaliuza’ wazo lake kwa Chama cha Ligi ya Soka cha Dar es Salaam (DFLA) ambao walianzisha mashindano hayo mwaka 1965 yakijulikana kama Ligi ya Taifa.
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa TFA (TFF) uliofanyika kati ya Desemba 19-20, 1964 (Jumamosi na Jumapili) katika Ukumbi wa Arnautoglou mjini Dar es Salaam ndio uliojadili pamoja na mambo mengine, uanzishwaji wa Ligi ya Taifa.
Kumekuwepo na changamoto nyingi tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo ya Ligi ya Taifa, lakini hapa nataka kueleza tu kwamba, katika miaka yote 46 iliyopita, ni klabu saba tu ndizo zilizofanikiwa kunyakua ubingwa.
Linaweza kuwa jambo la kushangaza, lakini huo ndio ukweli wenyewe, kwamba pamoja na ligi hiyo kushirikisha zaidi ya timu 80 kwa nyakati tofauti, lakini klabu hizi saba ndizo zilizofanikiwa kutawala, huku vigogo Simba na Yanga zikiwa ‘zinauatamia’ ubingwa kwa zamu.
Hata hivyo, ni klabu nne tu kati ya hizo ambazo ziko Ligi Kuu wakati nyingine tatu hazipo kwenye ramani ya soka ama zimekufa kabisa. Makala haya yanajaribu kuzichambua, japo kwa ufupi, klabu hizi zilizowahi kutwaa ubingwa tangu mwaka 1965.

Simba na Yanga

Hakuna shaka yoyote kwamba soka ya Tanzania haiwezi kunoga bila kuwepo kwa klabu hizi za Simba na Yanga. Hii inatokana na ukweli kwamba, klabu hizi ndizo kongwe na pekee kabisa zenye mashabiki wengi kila pembe ya nchi.
Huwezi kusema kwamba ndizo za kwanza kuanzishwa Tanzania, kwa sababu kabla ya kuanzishwa kwao zilikuwepo klabu nyingine kama Goans, KAR, Prisons na kadhalika ambazo ama zilimilikiwa na wakoloni Waingereza au zilikuwa za Waasia.
Lakini kuanzishwa kwa Yanga na Simba kulileta msisimko mpya kwa Waafrika ndani ya Tanganyika kwa sababu ziliwahusisha Waafrika zaidi na zikawa kama mkombozi kwao. Kuanzishwa kwao ndiko kulikosababisha kuanzishwa kwa klabu nyingine baadaye kama Gerezani, Tambaza, Kitumbini na nyinginezo nyingi.
Ushindani baina ya Simba na Yanga, uliotokana na kugawanyika kwao mwaka 1929 kutoka klabu iliyofahamika kama Jangwani iliyoanzishwa mwaka 1926, ndio uliozidisha hamasa hiyo hadi sasa kiasi cha kufanya kila zinaposhiriki mashindano yoyote kuwe na msisimko wa aina yake.
Simba ndiyo klabu ya kwanza kutwaa ubingwa wakati Ligi ya Taifa ilipoanzishwa mwaka 1965, wakati huo ikiitwa Sunderland ikiwa chini ya meneja wake Amir Ally Bamchawi na kikosi mahiri kama kipa Mbaraka Salum Magembe, Mohammed Khamis 'Bobeya', Emmanuel Mbele ‘Dubwi’, Juma Abeid Mzee, Yussuf Omar Kimimbi, Ali Durban, Mohammed Njunde, Hamisi Kilomoni, Adam Athumani, Hamisi Kisiwa, Said Chaurembo 'Cha', Arthur Mambetta, Haji Lesso, Mustafa Choteka, Kulwa Salum, Mussa Libabu, Tayari Mussa, Maulid Kambi 'Mandemla', Salum Ally Baltash, Said Mohammed Abdallah 'Walala', Ally Wage 'Kajo' na Hamisi Fikirini Mkwabi 'Liston'.
Kabla ya mechi za jana Jumapili, Simba ilikuwa imetwaa ubingwa huo mara 18, huku Yanga ikiongoza kwenye orodha hiyo kwa kuunyakua mara 24 na kuwa klabu pekee nchini kuutwaa mara nyingi zaidi.
Miaka ambayo Simba imetwaa ubingwa ni 1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004, 2007, 2009/2010 na 2011/2012.
Yanga ilianza kuonja ladha ya ubingwa mwaka 1968 ikiwa inaundwa na wachezaji kama Kabu, Saad Mohammed Songambele, Elias Michael, Hassan Gobbos, Maulidi Dilunga, Awadh Gessani (Cosmo), Kitwana Manara, Juma Bomba, Kitenge Said 'Waziri wa Ulinzi', Mohammed Msomali, Jacob Popo, Kaisi, Edward, Mohammed (kutoka Tanga), Athumani Kilambo, Ayubu Shabani (ATC), Kassim Lengwe, Badi Salehe, Gilbert Mahinya, Twaha Masimenti 'Bryson', Hamisi Mnubi, Omar Kapera, Leonard Chitete, Salehe Zimbwe, Jamil, Abdulrahman Juma, Abdulrahman Lukongo, Sharrif, na Boi Idd ‘Wickens’.
Baada ya hapo Yanga ikatawala soka la Tanzania kwa miaka mitano mfululizo, lakini ikayumba zaidi katikati ya miaka ya 1970 kufuatia kuwafukuza wachezaji wake nyota katika mgogoro mkubwa uliokuja kuzaa ‘Raizoni na Kandambili’ mwaka 1976.
Timu hiyo imetwaa ubingwa katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2007/2008, 2008/2009, 2010/2011 na 2012/2013.

Cosmopolitans
Hii ni moja ya timu zilizoanzisha Ligi ya Taifa mwaka 1965. Wanaoifahamu vyema historia ya soka Tanzania, watakubali kwamba zamani zile usingeweza kuzungumzia soka ya Tanzania bila kuihusisha klabu hii iliyoanzishwa mwaka 1956 jijini Dar es Salaam.
Cosmo ndiyo iliyokuwa bingwa wa Dar es Salaam mwaka 1964. Haikufanya vizuri katika miaka miwili ya kwanza ya Ligi ya Taifa (1965 na 1966) kutokana na utawala wa Sunderland na Yanga, lakini ilitoa ushindani mkubwa na kushika nafasi ya tano mara mbili mfululizo kati ya timu nane zilizoshiriki.
Mwaka 1967 ndio uliokuwa wa neema kwake baada ya kuibuka bingwa katika ligi ambayo ilikuwa na utata mtupu tangu mwanzo. Ndio msimu pekee ambao ulishuhudia Yanga na Simba (Sunderland) zinashindwa kushiriki ligi hiyo.
Sunderland iliungana na Yanga kukataa kushiriki ligi ambayo ilikuwa imeandaliwa haraka mwishoni mwa mwaka. Sunderland walisema wao ndio mabingwa, wakati Yanga nao walisema hawakuwa na wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo kwani wachezaji wao wengi walikuwa katika timu ya taifa iliyosafiri kwenda Kinshasa, Zaire katika mechi ya awali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, kisha ikaenda Nairobi, Kenya kwenye michuano ya Kombe la Gossage.
FAT iliyapuuza madai ya Sunderland na kusema hayakuwa ya msingi kwa sababu mwaka wa ubingwa wa timu hiyo ulikuwa umepita hata kama hakukuwa na bingwa mpya, na ikasisitiza kwamba timu zote zilistahili kutafuta ubingwa kila mwaka. Kwa maana hiyo FAT ikaendesha ligi hiyo bila kuzishirikisha Sunderland na Yanga.
Kwa hiyo basi, FAT ikaziteua Polisi Dar es Salaam na Tambaza FC kuchukua nafasi za Sunderland na Yanga kwenye ligi hiyo ya mtoano iliyoanza Novemba 26.
Cosmo, ikiwa chini ya kocha Mansour Magram, ndiyo iliyoonekana bora kuliko timu zote zilizoshiriki. Iliundwa na wachezaji kama Pompidou, Mohammed Msuba, Kitwana Douglas, Mohamed Msomali, Emil Kondo, makipa Mfaume ‘Difu’ na Abdoulmauty Hajmy, Jamil Hizam, Shaaban Mohammed Aden (kaka wa Ismail Rage), Masiku, Hamisi Ali 'Askari', Ibrahim Maulid, Samata, Mbaraka Peter, Nizar, Mohammed Makunda na wengineo.
Kwenye fainali Cosmo ilikumbana na vijana wa Coop United ambao walikuwa wameisambaratisha African Sports kwa mabao 5-1 Desemba Mosi kwenye nusu fainali. Mechi yao ya fainali ilipangwa kuchezwa Desemba 2, 1967. Lakini Coop United ikaomba FAT kuahirisha mchezo huo saa chache kabla ya pambano kwa kuwa wachezaji wao wengi walichoka na wengine kuumia katika pambano la nusu fainali na African Sports. FAT ikashikilia kwamba mchezo huo ni lazima uwepo kwa kuwa Desemba 3 ilikuwa ni siku ya kuanza kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Waislamua wengi walitegemea kuanza kufunga, ikiwa ni pamoja na wachezaji.
Siku ya mchezo watu walijaa kwenye Uwanja wa Ilala, Cosmo wakaingiza kikosi chao kamili huku wakishangiliwa na mashabiki wao. Coop United hawakuonekana, mwamuzi alisubiri kwa muda kisha akapuliza filimbi ya kumaliza mchezo. Cosmo ikatangazwa 'bingwa' wa Tanzania wa mwaka 1967.
Cosmo ilipotea katika ramani ya soka baada ya kushuka daraja mwaka 1970 iliposhindwa kufuzu kutoka Ligi ya Mkoa, na tangu wakati huo imekuwa ikifufuka na kusinzia. Kwa sasa iko katika Ligi ya Taifa.

Mseto FC
Tangu mwaka 1965 ilipoanza Ligi ya Taifa, ubingwa ulikuwa wa timu za Dar es Salaam. Hii ilitokana na uwezo wa kimchezo wa timu hizo, hususan Simba na Yanga.
Lakini mwaka 1975 Mseto FC, ambayo ilikuwa bingwa wa Mkoa wa Morogoro, iliwashangaza mashabiki wengi ilipofanikiwa kuwa timu ya kwanza kuupeleka ubingwa huo mikoani na kuvunja utawala wa timu za Dar es Salaam.
Mashabiki wa soka wa Morogoro waliokuwa kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi Agosti 2, 1975 usiku wakati Mseto ilipotwaa ubingwa kwa kuifunga Nyota FC ya Mtwara kwa mabao 3-1 katika mchezo wa fainali ya kuwania kombe hilo lililokuwa likiitwa Karume Cup, waliingia kichaa kwa kushangilia huku wakiongozwa na Katibu wa TANU wa mkoa wao, A. Lyander.
Katika mechi hiyo Mseto ilijipatia mabao mawili kupitia kwa Shiwa Lyambiko na moja kupitia kwa Omar Hussein, wakati ambapo Said Dogoa ndiye aliyefunga bao pekee la Nyota kwa njia ya penalti. Mseto iliingia fainali kwa kuitoa Usalama (Polisi) ya Dar es Salaam kwa mikwaju ya penati 5-3.
Katika kipindi hicho Mseto, iliyokuwa inanolewa na Mohammed Hussein Hassan ‘Msomali’, ilikuwa na wachezaji wazuri kama Said Gedegela, Charles Boniface Mkwasa, Hamadan, Vincent Mkude, Ramadhan Matola, Aluu Ally, Shiwa Lyambiko, Hassan Shilingi, Omar Hussein, Spencer, Jumanne Hassan ‘Masimenti’, Miraji Salum, Abdallah Hussein, Mnyepe, Hussein Ngulungu, Hemed Musa, Roma Mapunda na Kassim Mmanga.
Kuelekea mwishoni mwa miaka ya 1980, Mseto ikaanza kudorora hasa baada ya kuwa imeshuka daraja, na baadaye kufa mwaka 1991 kutokana na viongozi na wachezaji kutawanyika, ama katika harakati za kujitafutia maisha au kuhama, hali iliyosababisha kukosekana kwa msimamo na umoja.

Tukuyu Stars
Mstari wa Nyuma: Kutoka kushoto: Kevin Haule, Hussein Zito, Karabi Mrisho, Godwin Aswile, Ally Kimwaga, Danford Ngesi, Mbwana Makata, Athuman Juma, Ramnik Patel 'Kaka'.
Mstari wa Mbele: Kutoka kushoto: Fadhili Hembe, Richard Lumumba, Yusuf Kamba, Selemani Matthew Luwongo, John Alex, Daniel Chundu, Aston Pardon.
Kati ya timu zilizoweka historia katika Klabu Bingwa Tanzania, basi ni Tukuyu Stars. Siyo tu ilikuwa timu ya kwanza kutoka ‘kijijini’, yaani nje ya makao makuu ya mkoa, kunyakua ubingwa wa Tanzania Bara, lakini pia iliweka historia ya pekee kwa kupanda daraja la tatu, kisha la pili hadi kuwa bingwa mwaka 1986.
Wachezaji waliosaidia kupeleka ubingwa wilayani Rungwe kwenye kikosi hicho kilichokuwa kinanolewa na kocha Athumani Juma ni: Nahodha Ikupilika Nkoba, kipa Mbwana Makata, Justine Mtekere, Salum Kabunda ‘Ninja’, Lumumba Richard ‘Burruchaga’, Suleiman Mathew Luwongo, Caraby Mrisho, Abdallah Shahibu, Yussuf Kamba, Aston Pardon, Ghamshard Gamdast, Vincent Buriani, Kelvin Haule, Godwin Aswile, Hussein Zitto, Haji Shomari, Taisi Mwalyoba, Augustine Mumbe, John Alex, Peter Mwakibibi, na Daniel Chundu.
Timu hii ilibomolewa baadaye na Yanga na Simba ambazo ziliwachukua wachezaji nyota kama Mbwana Makata, Justine Mtekere, Salum Kabunda, John Alex, Godwin Aswile waliokwenda Yanga baadaye, wakati Simba ilimchukua Aston Pardon.
Jitihada zake za kutwaa ubingwa ziligonga mwamba na hatimaye ikateremka daraja mwaka 2004 na mpaka leo hakuna dalili zozote za kuisimamisha tena ili irudi Ligi Kuu.

Coastal Union
Mwaka 1988 ndio uliokuwa wa neema zaidi kwa mkoa wa Tanga katika soka. Ndio ulioshuhudia klabu zake mbili za Coastal Union na African Sports zikitwaa ubingwa wa Tanzania Bara na Muungano.
Hizi zilikuwa juhudi za miaka mingi za kuhakikisha kwamba kikombe cha ubingwa kinatua mkoani humo baada ya kupigana huko nyuma bila mafanikio.
Coastal Union, iliyoanzishwa mwaka 1948, ni miongoni mwa klabu zilizoanzisha Ligi ya Taifa mwaka 1965, lakini kwa miaka mingi ufalme ulitwaliwa na klabu za Simba na Yanga.
Mwaka 1988, ulikuwa mzuri zaidi kwao, ambao ikinolewa na Zacharia Kinanda ilikuwa imesajili wachezaji mahiri kama golikipa Hamisi Hassan Makena, Mohamed Mwameja, Hussein Lugha Mwakuluzo, Ali Maumba, Kassa Mussa, Said Kolongo, Yassin Abuu Napili, Douglas Muhani, Idrissa Ngulungu, Juma Mgunda, Abdallah Tamimu, Ally Jangalu, Mohamed Kampira, Razack Yussuf, Kassa Mussa, Kassim Majeshi, Agrey Chambo, Ally Mwaliza.
Ubingwa wa mwaka huo iliutwaa kwa mbinde hasa, kwa tofauti ya mabao ya kufunga ikiwapiku waliokuwa mabingwa watetezi Yanga na mahasimu wao African Sports. Baada ya mechi 22, timu zote tatu zilikuwa na pointi 26, lakini Coastal ilifunga mabao 27, Yanga ilikuwa na mabao 24 na African Sports ilikuwa na 23.
Pamba ndiyo iliyoitia nuksi Coastal katika mechi yake ya mwisho Julai 16 baada ya kuifunga 2-1 mjini Tanga, wakati ambapo Yanga yenyewe ilishinda siku hiyo bao 2-0 dhidi ya Nyota Nyekundu, ushindi ambao haukuisaidia kutetea ubingwa kwa sababu ilitakiwa kushinda mabao matano.
Makali ya timu hiyo maarufu kama ‘Wagosi wa Kaya’ yalitoweka kitambo na imekuwa kama na homa za vipindi, ikipanda daraja na kushuka. Hii inatokana na uongozi kutokuwa makini na migogoro ya ndani nayo inachangia.
Safari hii imepanda daraja kucheza Ligi Kuu msimu ujao, na kwa vile inatarajia kufanya uchaguzi wake mwezi Mei, basi tusubiri huenda ikapata uongozi makini zaidi unaoweza kurejesha heshima ya mkoa wa Tanga iliyopotea.

Mtibwa Sugar
Kama Tukuyu Stars iliupeleka ubingwa wa Tanzania Bara kwenye makao makuu ya wilaya, basi Mtibwa Sugar iliupeleka kijijini kabisa, Turiani, takribani kilometa 100 kutoka Morogoro mjini.
Klabu hii iliyoanzishwa mwaka 1988 na wafanyakazi wa kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, ilipanda Daraja la Kwanza (kabla ya Ligi Kuu) mwaka 1996 na kuleta ushindani mkubwa kwenye soka. Miaka mitatu baadaye, yaani mwaka 1999 ikafanikiwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara na kurudia tena mwaka 2000 huku Simba na Yanga zikiukodolea macho.
Pamoja na kuyumba katika siku za karibuni, lakini timu hii bado imara na inaweza kufanya vizuri kwenye Ligi msimu ujao.
NB: Daniel Mbega ni mwandishi mkongwe na mtafiti wa michezo nchini ambaye anaandaa kitabu cha ‘UBINGWA WA SOKA TANZANIA’. Wasiliana naye kupitia: brotherdanny5@gmail.com au +255 787 426161

Comments