Kinyogoli akimnoa Rashid Matumla.
Na Daniel Mbega
UNAPOLITAJA
jina la Habibu 'Master' Kinyogoli unakuwa kama umetaja jina la 'Chuo
Kikuu kinachotoa Shahada ya Juu ya Ndondi nchini Tanzania'. Ni sawa na
unapotaja timu ya soka ya Pamba ya Mwanza, ambayo kwa miaka mingi
imekuwa ikijulikana kama 'Chuo Kikuu cha Soka Tanzania' kutokana na
kutoa wanasoka wengi mahiri waliotamba katika klabu mbalimbali zikiwemo
Simba na Yanga pamoja na timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars.
Katika
Afrika, ukitaja jina la Zaiko Langa Langa moja kwa moja unakuwa
unazungumzia Shule ya Muziki barani humu, ambayo ndiyo iliyotoa
wanamuziki wengi wa Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), ambao
mpaka sasa ndio wanaotamba na kujulikana sana ulimwenguni. Kama
hawakujifunza muziki moja kwa moja ndani ya Zaiko, basi waliibukia
katika bendi zinazomilikiwa na watu walioanzia Zaiko!
Ndivyo ilivyo
kwa Habibu Ally Maulid Kinyogoli 'Master', ambaye yupo ulingoni kwa
zaidi ya miaka 40 sasa na hivyo kujiwekea historia ndefu na ya pekee,
pengine kuliko bondia yeyote wa enzi zake.
Kwa zaidi ya miaka 10
Kinyogoli alicheza ndondi za ridhaa, baadaye akawa mmoja wa waasisi wa
ndondi za kulipwa. Cha kujivunia zaidi ni kwamba, bondia huyo mkongwe,
kwa zaidi ya miaka 20 amekuwa akifundisha ndondi na siyo siri, wengi wa
mabondia wanaotamba sasa katika ndondi za kimataifa ni matunda yake
mwenyewe!
Ndiye aliyekuwa bondia wa pili wa Tanzania kuleta medali ya
mashindano yanayoshirikisha nchi kutoka nje ya Afrika Mashariki wakati
alipopata medali ya fedha katika Michezo ya Pili ya Afrika (2nd All
African Games) iliyofanyika mjini Lagos, Nigeria mwaka 1973.
Hadi
wakati huo mwanamasumbwi aliyekuwa ameleta medali kutoka nje ya mipaka
ya Afrika Mashariki alikuwa marehemu Titus Simba, ambaye alipata medali
ya kwanza ya fedha kwa Tanzania katika Michezo ya Jumuiya ya Madola
mwaka 1970 huko Scotland.
Kinyogoli anakiri kwamba, Simba ni mmoja wa
mabondia mahiri waliojitoa mhanga kwa kutetea heshima ya Tanzania,
lakini serikali haikuwajali kabisa hata pale alipofariki. Chama cha
Ndondi za Ridhaa (TABA) kilitoa mchango wa shilingi 4,000 tu kuchangia
mazishi ya bondia huyo mkongwe!
"Mimi binafsi serikali imenisahau
kabisa na haithamini mchango wangu katika mchezo huu, ingawa ni mimi
nilianza kuwafundisha vijana kadhaa waliolitangaza jina la nchi katika
ndondi za ridhaa na kulipwa," analalamika.
Miongoni mwa mabondia
ambao ni matunda yake ni Majuto Mchevu, aliyemfundisha mwaka sitini na
tisa katika klabu ya Magomeni Community Centre, Zakaria Yombayomba,
Habibu Mzungu, Bakari Selemani, Kweli Msigili, Abbas Pazi, Francis na
nduguye Benedict Kakokele aliowafundisha mwaka 1971.
Katika klabu ya
Urafiki mwaka 1973 aliwafundisha akina Charles Mhilu 'Spinks', Lazaro
Makali, Salum Temianga, Herbert Sempoli na Mmasi, ambao walikuwa
wakifanyia mazoezi Peninsula Hotel.
Baada ya kustaafu ndondi za
ridhaa mwaka 1978 na kuanza kufundisha watoto ndipo alipopata nafasi ya
kuwafundisha mabondia wengi zaidi. Mara tu baada ya kustaafu ndondi
mwaka huo alianzisha klabu ya ndondi ya Simba na kwa kuanzia akawachukua
watoto wa mzee Ally Matumla Namwera; akina Matumla, Haji, Rashid na
Hassan, ambao hivi sasa wamekuwa maarufu katika mchezo huo duniani kote.
Baadaye
akawachukua akina Mbwana, Karim na Mazimbo Matumla, Iraq Hudu, Joseph
Marwa, Adeli Mkajanga, Oscar Manyuka, marehemu Steven Bicco, Patrick
Kibona, Shabani Mohammed, Adam Abdulrahman, Maneno Oswald, Rajab
Mohammed, Abdallah Nyuni, Nassor Kondo, Rehema Matumla, Theresia
Kapinga, na wengineo wengi.
Anasema, pamoja na kuichezea timu ya
ndondi ya taifa kwa miaka 12, pamoja na kuendeleza vipaji vya vijana
wengi katika mchezo huo, lakini hakuna chochote alichoambulia kutoka
serikalini.
"Msaada pekee niliowahi kuupata ni mfuko wa mazoezi
(punching bag) na jozi mbili tu za gloves ambazo nilipewa na aliyekuwa
Mkurugenzi wa Michezo, Victor Mkodo," anasema kwa mamsikitiko.
Kinyogoli
alizaliwa Oktoba 20, 1948 huko Maneromango, wilayani Kisarawe, akiwa
mtoto wa tano katika familia ya mzee Ally Maulid Kinyogoli iliyokuwa na
watoto nane; wanne wanaume na wanne wanawake. Alipata elimu yake ya kati
huko Maneromango Middle School mwaka elfu mia tisa na sitini na tano.
Alianza
kucheza ngumi mwaka 1958 wakati akiwa darasa la pili. "Kulikuwa na kaka
yangu katika familia aliyeitwa Saidi Uliza 'Sheni' ambaye alikuwa
anacheza ngumi katika klabu ya Anartouglou, jijini Dar es Salaam. Kila
alipokuja likizo alikuwa akinifundisha. Pia mimi mwenyewe nilipokuwa
nikija mjini alinichukua na kunipeleka pale klabuni kwao kuangalia
mazoezi, kwa kweli nikavutiwa sana na mchezo huo," amaeleza.

Habibu
Kinyogoli kulia aliyeshika kikombe akiwa na Mfaume Kawawa Simba wa Yuda
baada ya kutoka katika mashindano ya All African Game 1973. Picha zote
kwa hisani ya www.superdboxingcoach.blogspot.com.
Baada ya
kumaliza shule aliamua kuja Dar es Salaam na kujiunga na klabu ya
ndondi ya Magomeni, ambapo walimu wao walikuwa Kassim Saidi na Joseph
Okalla. Mabondia wengine aliokuwa nao walikuwa Ayoub Zicco, Hamisi
Nassoro, marehemu Michael Nchimbi, marehemu Hemedi Selemani (kaka yake
Bakari Selemani) na wengineo.
Pambano lake la kwanza lilikuwa dhidi
ya Ally Kanduru wa JKT katika uzani wa light welter, ambalo lilikuwa la
kirafiki na lilifanyika mwaka sitini na sita. Kinyogoli alishinda
pambono hilo kwa knock out ya raundi ya pili.
Mwaka uliofuata alitwaa
ubingwa wa taifa wa uzani wa light baada ya kumchapa Jack Laimon wa
klabu ya Anartouglou. "Wakati huo uzito ulikuwa ni wa kubuni tu. Unaweza
kucheza uzito mkubwa, kesho ukacheza uzito mdogo. Mara nyingi mabondia
walikuwa wakipinishwa kwa kuangalia maumbo yao. Wakati Baraza la Michezo
la Taifa (BMT) lilipoundwa mwaka sitini na saba ndipo sheria zilipoanza
kufundishwa. Wakati huo Katibu Mkuu wa TABA alikuwa Nizar Walji,"
anafafanua.
Katika mashindano ya mikoa, anasema, mabondia wa Morogoro na Tanga walikuwa hatari na walimpa wakati mgumu sana.
Akiwa
katika timu ya Taifa, Kinyogoli aliweza kuzuru nchi nyingi kama Kenya,
Uganda, Zambia, New Zealand, Shelisheli, Nigeria, Ethiopia, Scotland,
Mexico na nyinginezo nyingi.

Kinyogoli akimwelekeza bondia Ibrahim Class
Anakumbuka kwamba, mwaka sitini na nae
alishindwa kwenda Zambia kuwania ubingwa wa Afrika kutokana na kuugua,
nafasi yake ikachukuliwa na James Jonathan.
Mapambano ambayo yapo
kwenye kumbukumbu yake ni lile la mtoano dhidi ya Adeyemi wa Nigeria
kuwania ubingwa wa Jumuiya ya Madola katika uzani wa light huko
Edinburgh, Scotland mwaka 1970, ambapo alishindwa kwa pointi. Mnigeria
huyo alinyakua medali ya dhahabu baada ya kuwatoa mabindia wengine kwa
KO. Ni katika michezo hiyo ambapo Titus Simba alitwaa medali ya fedha
baada ya kupigwa na John Conteh wa England.
Pambano jingine lililopo
kwenye kumbukumbu zake ni lile la kuwania ubingwa wa Afrika Mashariki na
Kati katika uzani wa unyoya (feather weight), ambapo alipambana na
Musoke wa Uganda mjini Nairobi, Kenya katika pambano la nusu fainali
mwaka 1971.
"Pambano hilo nilipigana kwa jihadi kama mtu mwenye
wazimu. Nilikuwa tayari kufa lakini nishinde. Hii ilitokana na ukweli
kwamba, bondia wa Tanzania nilikuwa nimebakia peke yangu katika michuano
hiyo baada ya akina Patrick Mtagalo, Said Tambwe na Frevitus Bitegeko
kutolewa. Wengi walinidharau na kujua kwamba na mimi ningebondwa kama
wenzangu. Hivyo, nilipanda ulingoni nikiwa na dhamira moja tu ya
kushinda na kuiondolea aibu Tanznaia, na kwa kweli nilishinda kwa pointi
na kuingia fainali," anasema.
Katika fainali alikumbana na John
Ndelu wa Kenya na akapigwa kwa pointi hivyo kufanikiwa kurejea na medali
ya fedha katika mashindano hayo ya kwanza kabisa katika ukanda huo.
Mwaka
huo 1971 alikwenda kushiriki katika sherehe za kuadhimisha uhuru wa
Madagascar na akasanikiwa kushinda mapambano yote mawili. Baada ya hapo
timu yote ya taifa ilikwenda Ujerumani kushiriki michezo ya
nusu-Olimpiki kujiandaa na ile ya Olimpiki ya mwaka 1972. Nchi nyingine
zilizoshiriki zilikuwa Romania, Cuba, Nigeria, Libya na wenyeji
Ujerumani Mashariki. Kinyogoli alipoteza pambano lake la kwanza tu kwa
pointi dhidi ya Peter Garth, Mjerumani, mtoto wa kocha aliyekuwa
akiwafundisha. Mjerumani huyo, hata hivyo, alidundwa na Eddy Nduku wa
Nigeria kwa KO ya raundi ya pili.
Mwaka 1972 alikwenda na timu ya
Taifa Munich, Ujerumani Magharibi katika michezo ya Olimpiki. Katika
hatua ya kwanza alimdunda bondia kutoka Cambodia, lakini akashindwa
mchezo wa pili dhidi ya Robert wa Puerto Rico, ambaye alimpiga kwa
pointi. Anasema alishindwa kwa sababu mkono wake uliteguka.
Mwaka
1973, aliweka historia nyingine kwa Tanzania baada ya kushiriki Michezo
ya Pili ya Afrika nchini Nigeria. Katika robo fainali alimpiga bondia
kutoka Madagascar na katika nusu fainali akamtwanga bondia kutoka Mali
na kusonga mbele kwenye fainali kuwania ubingwa wa uzani wa Bantam,
ambapo alikumbana na Omollo wa Uganda aliyemshinda Kinyogoli kwa pointi
na hivyo Mtanzania huyo kuambulia medali ya fedha.
"Uamuzi wa pambano
hilo ulilalamikiwa na majaji karibu wote isipokuwa wale waliokuwa
kwenye meza ya uamuzi. Matokeo yake Omollo hakuchaguliwa kwenye timu ya
ndondi ya Afrika na badala yake mimi ndiye niliyechaguliwa na kupewa
unahodha kwenye ndondi. Baada ya kufanya mazoezi nchini Senegal
nililiwakilisha Bara la Afrika mjini Mexico City, Mexico katika Michezo
ya Dunia ya Mabara," anaeleza.
Kinyogoli, akiwa nahodha wa Tanzania,
alifanikiwa kuingia fainali na kutwaa ushindi wa pili wa dunia wa uzito
wa Bantam baada ya kushindwa na Alfred Gomez wa Puerto Rico. Akarejea na
medali ya fedha.
Watanzania wengine waliokuwa wamechaguliwa kuunda
timu ya Afrika ni mwanariadha Filbert Bayi, aliyekuwa kipa wa Simba
marehemu Omar Mahadh bin Jabir na mshambuliaji wa zamani wa Young
Africans, Maulid Bakari Dilunga, ambaye alikuwa nahodha wa timu hiyo ya
Afrika.
Kinyogoli aliongozana pia na mabondia James Oduor wa Uganda
(uzito wa light), George Oduor wa Kenya (light welter), Dulla wa Kenya
(middle), na Obisia wa Nigeria (super welter). Wanamichezo wengine
walikuwa Ben Gibson wa Kenya aliyekuwa akikimbia katika mita 1,500 na
wengineo.
Mwaka 1974 alishiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola huko
Christchurch, New Zealand na kurudia robo fainali baada ya kudundwa kwa
pointi na Ally Rojo wa Uganda. Katika michezo hiyo mwanariadha wa
Tanzania Filbert Bayi alivunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500.
Mwaka
1975, Kinyogoli alishiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati mjini
Lusaka, Zambia na kutwaa medali ya shaba baada ya kupigwa na Mzambia
katika nusu fainali. Mwaka uliofuata alikuwa katika timu ya Taifa
iliyoshiriki sherehe za uhuru wa Shelisheli, ambazo zilishirikisha pia
nchi za Kenya, Uganda na wenyeji, na akashinda mechi zote mbili.
Mwaka
1977 alitwaa medali ya fedha baada ya kupigwa na bondia wa Ethiopia
katika fainali ya michuano ya Afrika Mashariki na Kati mjini Addis
Ababa, Ethiopia. Mwaka 1978 akaamua kustaafu kuichezea timu ya taifa na
kubakia kwenye klabu ya Bandari.
Mpaka anastaafu ndondi za ridhaa
alikuwa amecheza mapambano 110 na kushinda 95 na kupoteza 15. Alipata
medali saba, moja ya dhahabu, tano za fedha na moja ya shaba.

Habibu Kinyogoli akimfundisha bondia chipukizi wa kike, Lulu Kayege jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia
kuhusu makocha, Kinyogoli anasema kwamba, kocha Bajwala alikuwa
haeleweki kabisa, lakini akaongeza kwamba, alipata mchango mkubwa kwa
kocha Ogan Kodbas aliyekuwa kocha wa Afrika. Pia anamkumbuka kocha wa
timu ya Taifa, Calvin Cobb, aliyefukuzwa nchini kwa sababu za kiusalama.
Vifaa,
anasema, ndilo tatizo kubwa kwa sasa. "Mifuko ya mazoezi, gloves na
vifaa vingine ni vingi sana madukani tofauti na enzi zetu, lakini tatizo
kubwa ni fedha. Tukipata vifaa hivyo, pamoja na ulingo tutaweza kufanya
vizuri. Lakini ni vyema mabondia wa zamani wakafungua klabu nyingi za
mazoezi na wachezaji wajiunge kwenye klabu za kudumu ili kuuinua mchezo.
Lengo langu ni kuhakikisha nafungua klabu nyingi za mitaani kila
wilaya," anasema Kinyogoli ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Ngumi za
Kulipwa Mkoani Dar es Salaam (DPBU) chenye azma ya kuhamasisha klabu za
mitaani tu.
Ameitaka serikali kuhamasisha mchezo wa ndondi mikoani
kote, na ikibidi kuanzia mashuleni kama ilivyokuwa katika miaka ya
nyuma. "Uanzishaji wa klabu za mitaani kila pembe ndilo chimbuko la
mabondia wazuri," anasema.
Amewataka wafanyabiashara na Watanzania
kwa ujumla kujitokeza kuudhamini mchezo huo na akasifu jitihada
zinazofanywa na majeshi, hususan Jeshi la Ulinzi la Wananchi, kuwa hao
pekee ndio mapromota wanaoufanya mchezo huo uendelee kudumu Tanzania.
Jina
lake bado liko kwenye chati kama vile bado anacheza, na wale
aliowafundisha bado wanalitangaza. Mwaka 1998 Chama cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kilimuenzi kwa kumpa tuzo ya Bondia
Bora wa zamani.
Comments
Post a Comment