Featured Post

BIASHARA HARAMU YA NYAMA PORI TISHIO KWA VIUMBE HAI




NA ALOYCE NDELEIO
Alipokuwa akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii Waziri wa wizara hiyo Dkt. Hamisi Kigwangalla, alisema kuwa kanuni na taratibu  zitatumika kudhibiti biashara ya wanyamapori na mimea iliyo hatarini kutoweka.

Aidha, eneo la wanyamapori hai alisema kuwa umeandaliwa mpango madhubuti wa kusimamia kwa karibu kazi ya ukamataji wa wanyamapori hai ikiwa ni pamoja na  kufanya utafiti utakaoonesha hali halisi ya wanyamapori na kushauri kuhusu biashara ya wanyamapori hai.
Yote hayo yalikuwa sawa. Lakini licha ya biashara ya wanyamapori hai ipo biashara ya nyama ya wanyamapori ambayo kimsingi inatishia viumbe hivyo hususani vile ambavyo nyama yake hutumiwa na binadamu kama sehemu ya lishe.
Matumizi ya nyama pori kihistoria na kiutamaduni ni chakula kikuu cha jamii kulingana na shughuli zilizokuwa  zinafanywa na jamii hususani zilizokuwa na mfumo wa uzalishaji wa kuwinda wanyama na kukusanya matunda na mazao mengine ya asili kama vyakula.
Ongezeko la idadi ya watu na kushuka kwa kiwango cha maisha ni miongoni mwa sababu zinazochochea kuendelea kuwepo au kuongezeka kutegemea kile kinachopatikana katika hali ya asili  au maliasili hiyo kama chanzo kikuu cha virutubisho na hususani protini kwa wanajamii na hivyo kuifanya biashara hiyo kupanuka kutokana na wingi wa mahitaji.
Matokeo ya ongezeko kama hilo na usimamizi mbovu wa vyanzo vyake  kumeifanya sehemu kubwa ya biashara hiyo kuwa haramu licha ya kuwepo vizuizi vya kisheria.
Kwa mujibu wa Utafiti uliofanywa na taasisi ya Traffic ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kwa udhamini wa Kamisheni ya Ulaya kwa miaka miwili unabainishwa kuwa nyama pori ni chanzo kikuu cha chakula na mapato yanayotumika kuendeshea maisha kwa baadhi ya wanajamii.
Inabainishwa kuwa miongoni mwa nchi saba ulikofanyika umekuwepo utegemezi mkubwa wa kupata protini inayotokana na nyama pori kwa njia zisizo halali kuanzia wanyama wakubwa  kama tembo hadi aina mbalimbali za wadudu.
Utafiti unaarifu kuwa ongezeko la watu ndani ya jamii zinazozunguka hifadhi  huongeza mahitaji ya nyama pori na hata kutishia uwepo wa wanyamapori kwani ni mara chache fununu zinazohusu uwindaji haramu zimekuwa zinatolewa.
Utafiti huo unajulisha kuwa  tafiti nyingi za nyama pori zinaelekezwa maeneo ya Afrika Magharibi na Kati, na kuyafanya matumizi ya nyama pori kuonekana ni tabia iliyojikita kwenye  maeneo ya misitu ya tropiki.
Ilibashiriwa kuwa  kuongezeka  kwa matumizi na biashara ya nyama pori  kunaweza kuleta athari kubwa kwa mazingira na hata kwa binadamu iwapo hatua za kudhibiti hazitachukuliwa.
Unaarifu kuwa kimsingi inatakiwa matumizi ya nyama pori kwa njia halali ufanyike kwa kuboresha mawasiliano kati ya hifadhi za wanyama na sekta nyingine za mawasiliano.
Utafiti huo ulinuia kuangalia na kulinganisha biashara halali na haramu ya nyama pori, faida za kiuchumi  hususan kwa jamii za vijijini na athari za uvunaji katika maeneo ya hifadhi na aina ya wanyama wanaopendelewa kibiashara.
Nchi saba zilizohusika kwenye utafiti huo ambako matumizi ya nyama pori  ni makubwa ni Botswana, Kenya, Malawi, Msumbiji, Tanzania, Zambia na Zimbabwe
Kwa mujibu wa utafiti huo ilibainika kuwepo aina nyingi za wanyama pori wanaolengwa na kutumiwa mara kwa mara  huanzia wadudu, jamii ya panya na ndege, wanyama wenye ukubwa wa kati hususan  jamii ya swala  na wanyama wakubwa kama tembo na nyati; na wanyama kama ngiri na jamii ya swala aina ya pala  kwa ujumla hupendelewa kwani nyama yao kuwa ina ladha nzuri.
Kati ya aina zote za wanyama wanaotumiwa katika maeneo yaliyofanyiwa utafiti, nyati, swala pala na kudu wanawindwa sana na huchangia kiasi kikubwa cha nyama inayopatikana. Hata hivyo, idadi ya wanyama wakubwa inapungua kwani huwindwa kupita kiasi kwa kigezo kuwa wanaharibu mazingira.
Kupungua huko kunawafanya watumiaji wa nyama hiyo kubadilika na kuwalenga  wanyama wadogo wanaopatikana katika maeneo hayo bila kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Utafiti huo wa Traffic umebaini kasi ya ongezeko la matumizi ya nyama pori kupo  sanjari na ongezeko la haraka la idadi ya watu, kukithiri kwa umasikini na ukosefu wa ajira, hali inayofanya nyama pori ionekane kama chanzo muhimu kitakachoinua hali zao za maisha.
Inaarifiwa katika utafiti huo kuwa  uwindaji wa aina ndogo za wanyama ni alama tosha ya kupungua kwa kiwango kikubwa kwa wanyama pori na hususani aina inayopendelewa zaidi.
Kupungua kwa idadi ya wanyama hao na kwenye maeneo husika kunatokana na uwindwaji wa kupita kiasi na kuifanya bei yake kupanda hivyo wawindaji  na wafanya biashara kulenga kila aina ya mnyama anayeingia kwenye mitego yao.

Aidha, moto wa kupata faida na kuongezeka kwa thamani ya nyama pori  umewafanya wawindaji kuongeza kasi ya kupata nyama hiyo kwa namna yoyote ile hata kwa njia hatari hivyo kuwepo kwa uwindaji usio endelevu wa matumizi ya nyaya, uwindaji wa kutumia kurunzi nyakati za usiku na matumizi ya silaha kali zaidi kama bunduki za machinegun.
Utafiti huo pia umebaini kuongezeka kwa mahitaji ya nyama pori miongoni mwa jamii za Mashariki na Kusini mwa Afrika na matokeo yake ni wanyama  kukoseshwa muda wa kuzaliana na kuongezeka pindi misimu ya uwindaji unapofungwa.
Hali kadhalika mfumo wa kitamaduni wa usimamizi katika uwindaji kama vile kuchagua jinsia ya kuwindwa au kukataza kuwawinda wanyama wenye mimba umekuwa hautiliwa maanani katika maeneo yote.
Hata hivyo, miiko inayowalinda wanyama nayo imekuwa inapuuzwa na juhudi zinazofanywa na vyombo vya dola kukabiliana na uwindaji haramu unaochochewa na mahitaji ya nyama pori zimepungua kwani adhabu zinazotolewa ni faini ndogo ikilinganishwa na thamani ya nyama pori inayokuwa imewindwa.
Uvunaji halali wa nyama pori unaweza kusaidia kukabiliana na uwindaji haramu lakini kiwango kinachotakiwa hakifikiwi.
Kwa nchi zote saba zilizofanyiwa utafiti uvunaji wa nyama pori kwa kutumia njia halali za vitalu vya wanyama au uwindaji wa leseni na kupitia mikakati ya uwindaji kwa kudhibiti wanyama huwezesha kupatikana nyama ya wastani wa mita 8,500 kwa mwaka; na kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na kiwango halisi ambacho kingetakiwa kuvunwa.
Kiongozi wa chama cha kulinda viumbe duniani, Dkt. Jane Smart, amesema orodha ya viumbe vilivyo hatari barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ni kubwa na asilimia 20 inasababishwa na baishara haramu ya nyama ya pori.
Kupotea kwa wanyamapori wanaowindwa kwa ajili ya nyama huenda kukasababisha kupotea kwa mapato huku maeneo yakiachwa bila viumbe na hivyo kutowavutia tena wageni. Jambo hili huenda pia lisababishe athari za kiuchumi pamoja na hasira miongoni mwa wakazi wa maeneo hayo.
Hali kadhalika utafiti huo ulibaini kuwa mikakati ya uvunaji halali inakwamishwa na sheria  za nyama ambazo hupendelea uzalishaji wa nyama kutoka kwa wanyama wanaofugwa hivyo kuwa kikwazo kwa soko zuri la nyama pori.
Kwa vyovyote vile  lazima iwepo mikakati ya kudhibiti biashara hiyo pia kwani kuufanya uvunaji wake kwa kuzingatia kanuni na taratibu kutalifanya soko lake kuwa la uhakika na kufanywa uhai wa viumbe hivyo kuwa endelevu.
CHANZO: TANZANITE

Comments