Featured Post

YONDAN, KESSY WAIGOMEA YANGA



NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAKATI Yanga imetangaza rasmi kuwarejesha viungo wake, Deus Kaseke na Mrisho Ngassa, wachezaji Kelvin Yondan na Hassan Ramadhan Kessy  wamegoma kushinikiza kusaini mikataba mipya.
Yanga imewaongeza Ngassa na Kaseke ili kuimarisha kikosi chake kuelekea mechi zilizosalia za Kundi D kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Majina ya wachezaji hao yametumwa kwenye Shirikisho la Soka Afrika (CAF) pamoja na jina la mshambuliaji Heritier Makambo kutoka DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Jerry Tegete.
Ngassa na Kaseke wanafanya idadi ya wachezaji wapya waliosajiliwa rasmi Yanga kufika wanne, baada ya viungo wengine, Feisal Salum kutoka JKU ya Zanzibar na Jaffar Mohammed kutoka Maji Maji ya Songea iliyoshuka daraja.
Uongozi wa Yanga unakabiliwa na mtihani juu ya wachezaji waliogoma, kipa Benno Kakolanya, mabeki Juma Abdul, Andrew Vincent ‘Dante’, Hassan Kessy na Kelvin Yondan ambao wamemaliza mikataba.
Wachezaji wote hao wamesusa mazoezi wakishinikiza kupewa mikataba mipya na angalau Kakolanya, Abdul na Dante walifanya mazoezi kwa siku kadhaa kabla ya kuungana na Kessy na Yondan kususa kabisa kufuatia kuona viongozi hawatimizi ahadi.
Yanga inatarajiwa kuteremka uwanjani Jumatano Julai 18, 2018 mjini Nairobi, Kenya kumenyana na wenyeji, Gor Mahia katika mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika, kabla ya timu hizo kurudi Dar es Salaam kwa marudiano Julai 29.
Yanga haijashinda mechi hata moja kati ya mbili za awali za Kundi D baada ya kufungwa 4-0 na USM Alger nchini Algeria Mei 6 na kutoa sare ya 0-0 na Rayon Sports ya Rwanda mjini Dar es Salaam Mei 16.
Yanga itacheza tena nyumbani, Uwanja wa Taifa ikiwakaribisha USM Alger Agosti 19 kabla ya kwenda kukamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na wenyeji, Rayon Sport Agosti 28.
Timu mbili za juu katika kundi hilo zitaungana na washindi sita wa makundi mengine manne kwa mechi za nyumbani na ugenini za Robo Fainali na zitakazofuzu zitasonga mbele, Nusu Fainali na baadaye Fainali.
Bingwa wa Kombe la Shirikisho atapata zawadi ya Dola za Kimarekani, 1,250,000, mshindi wa pili dola 432,000 wakati timu zitakazoshika nafasi za pili kwenye kila kundi zitapata dola 239,000 kila moja, nafasi ya tatu dola 239,000 na za nne dola 150,000.


Comments