Featured Post

WAZIRI KIGWANGALLA AWASIMAMISHA KAZI MAOFISA NA ASKARI WOTE 27 WA TAWA KATIKA PORI LA AKIBA UWANDA

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, akimsikiliza mkazi wa kijiji cha Kilyamatundu, Shija Imeli (kulia) alipokuwa akiwasilisha malalamiko yake kuhusu tuhumu za kuwapa rushwa ya shilingi milioni 5.8 Askari watano wa Wanyamapori wa Pori la Akiaba Uwanda (pichani) ili alishe mifugo yake kwa kipindi cha miezi mitano ndani ya pori hilo.

Na Hamza Temba, Rukwa
.......................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amewasimamisha kazi Maofisa na Askari Wanyamapori wote 27 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA katika Pori la Akiba Uwanda akiwemo Kaimu Meneja, Lackson Mwamezi kwa kushindwa kusimamia vizuri pori hilo na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku tatu tangu amsimamishe kazi meneja wa Pori hilo, Mark Chuwa kwa tuhuma kama hizo pamoja na tuhuma nyingine ikiwemo kushindwa kuondoa ngo'mbe zaidi ya 12,000 ambao wamedaiwa kuwepo ndani ya pori hilo.

Pori la Akiba Uwanda lipo katika bonde la ziwa Rukwa katika wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa na linasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Dk. Kigwangalla amefanya uamuzi huo jana alipotembelea pori hilo sambamba na kufanya mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kilyamatundu ambapo alipokea taarifa ya malalamiko kuhusu askari hao kupokea rushwa kutoka kwa watu wenye uwezo na kuwaruhusu kuchunga hifadhini huku wakiwanyanyasa masikini kwa kukamata mifugo yao.

Alifafanua tuhuma hizo kuwa ni pamoja na kudaiwa kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wavuvi wanaovua samaki Ziwa Rukwa kwa kuwatozwa kila mmoja Sh. 100,000/- kwa mwezi na kuruhusu mifugo kuchungwa hifadhini kwa kipindi cha  miezi mitatu ambapo  kila mfugaji hutozwa  kati ya Shilingi milioni sita hadi saba.

Dk. Kigwangalla pia ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru kuchunguza mali  na tuhuma za rushwa walizopewa askari wote wa pori hilo wakiwemo watano waliotuhumiwa kwenye mkutano wa hadhara kwa kuomba rushwa ya shilingi milioni 6 kwa ndugu Shija Imeli ili wamruhusu kulisha mifugo yake hifadhini kwa muda wa miezi mitano.

Shija alisema mnamo tarehe 05 Januari mwaka huu akiwa nyumbani kwake na Ndugu Shemen Kuzenza, askari watano wa pori hilo walifika nyumbani kwake na kumtishia kuwa endapo atalisha mifugo hifadhini wangemkamata huku wakijua hana sehemu nyingine ya malisho hivyo wakamtaka kutoa rushwa ya shilingi milioni 6 ili aruhusiwe kulisha mifugo yake hifadhini kwa muda wa miezi mitano.

Alisema walifanikiwa kuwapa askari hao jumla ya shilingi mil. 5.8 kwa nyakati tofauti na kwamba walivyoshindwa kumalizia laki 2 zilizobakia askari hao walikamata mifugo yao nje ya eneo la hifadhi.

Kufuatia malalamiko na tuhuma hizo, Dk. Kigwangalla aliitisha gwaride la utambuzi lililohusisha askari wa Jeshi la Wananachi wa Tanzania (JWTZ), askari  wa usalama barabarani na maofisa na askari wanyamapori wa TAWA waliokuwepo katika mkutano huo wa hadhara.

Shija na mwenzake Kusenza waliweza kuwatambua askari watano wa TAWA waliowatuhumu kuwaomba rushwa na hapo hapo Waziri Kigwangalla akawaamuru kukabidhi silaha zao na kumuagiza  Mkuu wa Polisi wa  Wilaya ya Kipolisi  ya Laela, Aloyce Nyatola kuwakamata mara moja na TAKUKURU ianze uchunguzi wa tuhuma hizo ili sheria ichukue mkondo wake na iwe fundisho kwa wengine. 

Hata hivyo, baada ya mkutano wa hadhara, Dk. Kigwangalla aliamua kukagua baadhi ya maeneo ndani ya pori hilo na kubaini uharibifu mkubwa uliofanywa na mifugo huku dalili zikiwa ni kinyesi cha ng'ombe kilichokuwa kimezagaa kila mahali. 

Hapo hapo alimuagiza Mkurugenzi Mkuu TAWA, Dk. James Wakaibara ambaye aliwakilishwa na Mkurugenzi wa Biashara na Huduma za Utalii wa mamlaka hiyo, Imani Nkuwi kuwasimamisha kazi wafanyakazi wote wa pori hilo na kuleta wengine wapya wasimamie pori hilo ili kupisha uchunguzi.

"Hawa wote wasimamishwe kazi na uchunguzi ufanyike kitu gani kilikua kinaendelea hapa, kwanza ifanyike parade kuhusu suala la kumuomba rushwa yule mfugaji, wabainike moja kwa moja wafunguliwe mashtaka, na hawa wote nataka wachungunguzwe na mali walizonazo kama ambavyo imeelezwa kuwa hawa wametumia hili pori kama kitega uchumi chao binafsi, huu ni uhujumu uchumi" aliagiza Dk. Kigwangalla.

Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla ametoa siku 30 kwa wananchi wote  wenye mifugo ndani ya pori hilo kuitoa kwa hiari yao wenyewe kabla ya operesheni maalum itakayowaondoa kwa nguvu. Alisema kama walijua pori hilo ni shamba la bibi sasa wasahau na wajipange namna ya kutafuta malisho au kupunguza idadi ya mifugo yao na kuanzisha miradi mingine ya maendeleo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, akiamuru askari watano wa Pori la Akiba Uwanda wanyang'anywe silaha zao na wawekwe chini ya ulinzi kwa ajili ya uchunguzi baada ya kutambuliwa kwenye gwaride kwa tuhuma kupokea rushwa ya shilingi milioni 5.8 kutoka kwa mfugaji, Shija Imeli (Kulia) kwa makubaliano ya kulisha ng'ombe wake ndani ya pori hilo kwa muda wa miezi mitano.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na viongozi wengine wa mkoa wa Rukwa, wakikagua mazingira ya Pori la Akiba Uwanda baada kuwasimamisha kazi maafisa na askari wote 27 wa pori hilo kupisha uchunguzi wa tuhuma za rushwa zinazowakabili. Watumishi hao wananalalamikiwa kupewa rushwa ili kuruhusu wananchi wachunge mifug hifadhini na kwa wale ambao hawatoi rushwa huishia kukamtwa mifugo yao. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na viongozi wengine wa mkoa wa Rukwa, wakikagua mazingira ya Pori la Akiba Uwanda baada kuwasimamisha kazi maafisa na askari wote 27 wa pori hilo kupisha uchunguzi wa tuhuma za rushwa zinazowakabili. Watumishi hao wananalalamikiwa kupewa rushwa ili kuruhusu wananchi wachunge mifug hifadhini na kwa wale ambao hawatoi rushwa huishia kukamtwa mifugo yao.

Comments