Featured Post

VIGOGO WALIOKOPA SUMA JKT KUTIWA MBARONI JUMATATU



NA MWANDISHI WETU
VIGOGO mbalimbali, wakiwemo wanasiasa na wafanyabiashara, waliokopa kwenye Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) na kushindwa kulipa wataanza kusakwa na kukamatwa Jumatatu, Julai 16, 2018.
Taarifa iliyotolewa wiki hii imeeleza kwamba, zoezi la kuwasaka wadaiwa hao litaanza kutekelezwa mara moja ikiwa ni pamoja na kukamata mali zao, ambapo litasimamiwa na Suma JKT Auction Mart.

Mei 17, 2018 akiwa katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Uwekezaji cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia Suma JKT kilichopo Mgulani, jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, alimweleza Rais Magufuli kuwa, JWTZ linazidai sekta binafsi Shs. bilioni 40, huku taasisi za Serikali zikidaiwa Shs. bilioni 3.4, jambo ambalo limekuwa likiwakwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Alisema ili kuliwezesha jeshi hilo kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo, Jenerali Mabeyo alimwomba Rais Magufuli apokee orodha ya wadaiwa ili aongeze msukumo katika ulipaji wake.
Rais Magufuli alitoa mwezi mmoja kwa wadaiwa wote, kuhakikisha wamelipa madeni na kuagiza baada ya kuisha kwa kipindi hicho, mamlaka zinazohusika na ukusanyaji madeni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, kuwachukulia hatua kali wadaiwa wote.
Baadaye, Suma JKT iliwatangazia wote wanaodaiwa kupitia tangazo lao la hivi karibuni kwa kuwataka wadaiwa kulipa kabla ya Juni 15, muda ambao tayari umeshaisha.
Tangazo lingine lililotolewa na Makao Makuu ya SumaJKT la Jumanne wiki hii likiwa na kichwa cha habari 'Lipeni madeni kwa wakati' lilisema wale walioshindwa kutekeleza agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria.
Pia tangazo hilo liliwaeleza wale waliopatiwa huduma ya ulinzi na Suma JKT Guard na kushindwa kulipa kuwa huduma hizo zitasitishwa na watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwamo kukamata mali zao kufidia deni wanalodaiwa.
Inaelezwa kwamba, licha ya baadhi ya wadaiwa kuandika barua kuomba wapewe muda zaidi ili walipe madeni hayo, lakini uongozi wa Suma JKT umewagomea kwa maelezo kwamba, walikuwa na muda wa kutosha na hawakuweza kulipa.
Mwanzoni mwa wiki hii kituo kimoja cha radio kiliikariri taarifa ya uongozi wa Jeshi ikisema kwamba, uamuzi wa kuwakamata wadaiwa wote unafuatia wadaiwa hao kushindwa kulipa kwa wakati licha ya kukumbushwa mara kwa mara.
Hivi karibuni, Suma JKT ilitangaza kwenye tovuti yake kuwataka wadaiwa wake walioshindwa kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli la kulipa madeni wanayodaiwa kwa wakati, kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Aidha, tangazo hilo lilisema, kwa waliopatiwa huduma ya ulinzi na SumaJKT Guard Ltd na kushindwa kulipia, huduma hizo zitasitishwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kukamata mali zao kufidia deni wanalodaiwa.
Kwa mujibu wa orodha iliyotolewa na Suma JKT, jumla ya wadaiwa 1,561 walikopa matrekta wakati taasisi 26 zinadaiwa malipo ya huduma ya ulinzi.
Miongoni mwa wadaiwa sugu waliokopa matrekta na kushindwa kulipa wamo pia mawaziri wa sasa, mawaziri wastaafu, wabunge na wakuu wa mikoa wa sasa na wastaafu.
Baadhi ya majina ya mawaziri wa sasa yaliopo kwenye orodha hiyo ni Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Luhaga Mpina na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.
Pia kwenye orodha hiyo yumo Naibu Waziri wa Wizara ya Uvuvi na Mifugo, Abdallah Ulega, ambaye ni Mbunge wa Mkuranga.
Mawaziri wastaafu waliotajwa kwenye orodha hiyo ni Dkt. Juma Ngasongwa aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara na waziri wa wizara mbalimbali kwenye serikali zilizopita.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rodrick Mpogolo, ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato mkoani Geita pamoja na aliyekuwa Waziri wa Fedha kwenye utawala wa awamu ya nne, Mustapha Mkulo nao wamo.
Wakuu wa mikoa wa sasa waliotajwa kwenye orodha hiyo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka na Mkuu wa Mkoa wa Sindiga, Dkt. Rehema Nchimbi.
Wabunge waliotajwa kwenye orodha hiyo ni pamoja na Husna Mwilima wa Kigoma Kusini (CCM), Mbunge wa Shinyanga Mjini, Steven Maselle (CCM) na Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM).
Wabunge wengine waliotajwa ni Ignas Malocha wa Jimbo la Kwela (CCM), Mbunge wa Kilolo (CCM), Venance Mwamoto, Mbunge wa Korogwe Mjini (CCM), Mary Chatanda, Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde na aliyekuwa Mbunge wa Songea Mjini (CCM), marehemu Laurence Gama.
Kwenye orodha hiyo pia wamo wabunge waliopita akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila na aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini (CCM), Benson Mpesya (2000-2010).
Wabunge wengine waliopita waliotajwa ni aliyekuwa Mbunge wa Manyoni Magharibi (CCM), Paul Lwanji, aliyekuwa Mbunge wa Afrika Mashariki (CCM), Sylvia Kate Kamba, aliyekuwa Mbunge wa Mbarali (CCM), Modestus Kilufi na aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (CCM), Manju Msambya.
Mwingine aliyetajwa ni aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM na mwanachama wa Chadema sasa, John Guninita.
Kwenye orodha hiyo pia ametajwa aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, marehemu Said Mwambungu.
Taasisi za umma zinazodaiwa ni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jinsia, Wazee, na Watoto, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Fedha na Mipango.
Nyingine ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) Dar es Salaam, Chuo cha Madini - Nzega, Stamigold - Biharamulo na Chuo cha Serikali za Mitaa - Hombolo, na Halmashauri za Wilaya za Kasulu, Kibaha na Geita.
Wizara nne ni sehemu ya wadaiwa wa Suma JKT Guard Ltd ambapo inaelezwa kwamba, hadi mwezi Mei 2018, deni lililokuwa limelipwa ni Shs. bilioni 3.451 kati ya Shs. bilioni 4.057.
Halmashauri tatu ni miongoni mwa wadaiwa sugu waliokopa matrekta kutoka Suma JKT ambao mpaka sasa deni lao limefikia Shs. bilioni 40.
Mnamo Juni 4, 2018, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, alisema alikuwa amepokea orodha ya wabunge wanaodaiwa fedha za matrekta na Suma JKT na walitakiwa kuwa wamelipa kabla ya Juni 23.
Baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu.
Mei 17, 2018, Rais John Magufuli alitoa mwezi mmoja kwa taasisi za Serikali na watu binafsi wanaodaiwa na Suma JKT deni la Shs. 41.4 bilioni kuhakikisha wanalipa.
"Wizara ya Ulinzi na JKT imewasilisha orodha kwa Ofisi ya Spika ya wadaiwa wa fedha za matrekta na mnatakiwa kulipa madeni haya haraka iwezekanavyo kabla ya Juni 23, 2018," alisema Spika Ndugai.
"Nina orodha ndefu hapa, sijui niisome? Kuna wengine nimejaribu kuangalia basi hata wakatwe juu kwa juu kwenye fedha hizi tunazopata pata, lakini hawana hata fedha kabisa... sina pa kukata, sasa kwa kweli jitahidini tu," alisema Ndugai.
Mnamo Februari 27, 2013, Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete alilitaka Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) kulipa deni la Shs. 42 bilioni linalotokana na mkopo kutoka Serikali ya India kwa ajili ya ununuzi wa matrekta ya 'Kilimo Kwanza'.
Serikali za India na Tanzania ziliingia mkataba wa mkopo wa Shs. 40 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa mtrekta ambayo yalikabidhiwa kwa Suma JKT ili iyauze chini ya Mpango wa Kilimo Kwanza. Mkataba wa mkopo huo ulisainiwa mwaka 2010 na ulipangwa kudumu kwa miaka mitano huku Tanzania kupitia Suma JKT ikitakiwa kulipa Shs. 42 bilioni na riba.
JK alisema lengo la Serikali lilikuwa kuidhamini Suma JKT kupata mkopo huo, ili kuendeleza Mpango wa Kilimo Kwanza ambao ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
CHANZO: FAHARI YETU

Comments