Featured Post

UTAFITI: MTOTO AKIPEWA CHAKULA KIGUMU MAPEMA ANALALA VIZURI



NA MWANDISHI WETU
WATOTO wachanga wanaopewa vyakula vigumu na maziwa ya mama kuanzia umri wa miezi mitatu wanalala vizuri kuliko wale wanaopewa maziwa ya mama pekee, tafiti mpya zinaweka wazi.
Ni rasmi kuwa yapasa kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita mfululizo. Wataalam wanasema wanawake wanatakiwa kufuata ushauri huo, ingawa upo katika mapitio.
Katika utafti mpya, wataalam wa watoto (JAMA) wanasema kumpa mtoto chakula kigumu kuna faida kwa mama na mtoto.

Watoto waliokuwa na matatizo machache ya kulala na akina mama waliripotiwa kuboresha ubora wa maisha.
Na utafiti uliofanywa na vyuo vya Kings na St George huko London ulichunguza watoto wa miezi mitatu 1,303 na waligawanywa katika makundi mawili.
Kundi la kwanza walipewa maziwa ya mama pekee kwa muda wa miezi sita, na kundi la pili walipewa vyakula vigumu na maziwa ya mama kuanzia walipofikia umri wa miezi mitatu.
Wakati tafiti zikiendelea, wazazi walijaza fomu za kujibu maswali kupitia mtandao kila mwezi mpaka watoto wao walipofikisha umri wa miezi 12, na baadaye walijaza kila baada ya miezi mitatu mpaka watoto walipofikisha umri wa miaka mitatu.
Utafiti ulionyesha kwamba, watoto wachanga waliopo katika kundi ambalo wanakula vyakula vigumu na maziwa ya mama walilala zaidi, waliamka mara chache na walikuwa na matatizo machache ya usingizi kuliko wale waliopewa maziwa ya mama pekee.
Akina mama wanaojua sana:
Mashirika ya NHS na WHO hivi karibuni yaliwashauri akinamama kusubiri mpaka miezi sita kuwapa watoto wachanga vyakula vigumu, lakini maelekezo haya kwa sasa yanapitiwa upya.
Licha ya kutolewa kwa ushauri huo rasmi, asilimia 75 ya akinamama wa Uingereza wanawaanzishia watoto wachanga vyakula vigumu kabla ya kufikisha miezi mitano, huku robo yake, yaani asilimia 26, wakisema kitendo cha watoto kuamka usiku ndiyo sababu ya maamuzi yao, kwa mujibu wa utafiti wa kuwalisha watoto wachanga mwaka 2010.
Profesa Gideon Lack kutoka Chuo cha Kings, London, alisema: "Matokeo ya utafiti huu yanaunga mkono mtazamo wa wazazi kwamba kutanguliza mapema vyakula vigumu kwa watoto wachanga kunaboresha usingizi.
"Wakati mwongozo rasmi wa awali unasema kuanzisha vyakula vigumu mapema kwa watoto wachanga hakuwezi kuwafanya watoto walale usiku mzima, utafiti huu mpya unapendekeza kwamba ushauri huo unatakiwa kuchunguzwa upya kupitia uthibitisho mpya uliopatikana."
Kwa kiasi kikubwa, kundi la watoto waliopewa vyakula vigumu mapema, waliripoti nusu ya kiwango cha aina ya matatizo makubwa ya kulala, kama vile kulia na kukasirika haraka, hali ambayo inakosesha wazazi uwezekano wa kupata muda wa kulala.
Akijibu utafiti huo, Prof. Mary Fewtrell, mtaalam wa lishe katika Chuo cha Royal kinachohusiana na afya ya watoto, alidokeza kwamba muongozo wa ulishaji wa watoto wachanga kwa sasa unaangaziwa upya.
Alisema, haya ni matokeo ya kuvutia kutoka kwa kundi kubwa la watu tofauti lililo jaribiwa.
"RCPCH, tunapendekeza kwamba akina mama wanapaswa kusaidiwa kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa ajili ya afya kwa kipindi cha miezi sita, na vyakula vigumu visianzishwe kabla mtoto hajafikia miezi minne.
"Hata hivyo, ushahidi wa msingi unaotokana na ushauri unaotumika sasa juu ya unyonyeshaji ni wa zaidi ya miaka 10, na kwa sasa una hakikiwa huko nchini Uingereza na kamati ya ushauri wa kisayansi ya lishe. "Tunatarajia kuona mapendekezo yaliyosasaishwa juu ya ulishaji wa mtoto mchanga katika siku zijazo si mbali sana."

Chakula kipi unachopaswa kumpa mtoto wako?
Vyakula vya awali vinaweza kujumuisha chakula kilichopondwa au matunda laini na mboga mboga zilizopikwa - kama vile viazi, viazi vitamu, karoti au tufaha.
Matunda laini kama vile matikiti au mchele wa watoto au nafaka mchanganyiko pamoja na maziwa ya kawaida ya mtoto wako.
Watoto wengine wanapenda kuanza na vyakula vilivyo pondwa. Watoto wengine wanahitaji muda zaidi ili waweze kuzoea hivyo wanapendelea vyakula laini kabisa au vilivyo sagwa kwa mara ya kwanza.
Endelea kumpa vyakula mbali mbali. Inaweza chukua majaribio mengi kabla mtoto wako hajakubali chakula kipya.
Kufikiria chakula cha kuwapa watoto wachanga katika miezi sita ya awali inaweza kuwa utata, na akina mama wengi huwa na hofu kwamba wanashutumiwa kwa kushindwa kuwanyonyesha vizuri watoto wao, na hujiona na hatia wanapoanzishiwa watoto maziwa ya kopo au vyakula vigumu.
Mwezi uliopita chuo cha wakunga cha Royal, kilijibu juu ya shinikizo wanalopata akinamama wapya kwa kutoa hadharani mwongozo mpya kwa wakunga kuheshimu uchaguzi wa mwanamke kutonyonyesha.
Utafiti huu wa vitu vigumu sehemu ya ufadhili wake ulitoka kwa shirika la viwango vya chakula, ambalo pia lilikuwa linachunguza namna gani mzio (allergy) unatokea kwa watoto.
Msemaji wa FSA alisema: "Tunawahimiza wanawake wote kujikita kwenye ushauri uliopo wa kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza.
"Kama kutakuwa na shaka yoyote kuhusu kile kilicho bora kwa mtoto wako, tafadhali tafuta ushauri kutoka kwa daktari wako au mtaalamu wa afya."
BBC

Comments