Featured Post

NDIZI HATARINI KUTOWEKA DUNIANI


Ndizi ya Madagasca: Je ndizi hii inaweza kuokoa ndizi inayotumika duniani?

ANTANANARIVO, MADAGASCAR
NDIZI zinazomea porini ambazo huenda ndio suluhu katika kulinda ndizi za kawaida zinazotumiwa kama chakula cha binaadamu zimeorodheshwa miongoni mwa mimea inayoangamia.

Mti huo hupatikana nchini Madagascar pekee ambapo kuna miti mitano iliosalia katika pori.
Wanasayansi wanasema kuwa mmea huo unahitaji kuhifadhiwa, kwa kuwa huenda ukabeba siri za kulinda ndizi siku zijazo.
Changamoto ni kuanzisha aina mbali mbali ya ndizi ambazo ni tamu kwa matumizi ya mwanadamu na ambazo zinaweza kustahimili mashambulio yoyote kutoka kwa magonjwa ya Panama.
Ndizi ya Madagascar imekuwa pekee katika kisiwa na huenda ina vitu muhimu.
Richard Allen, muhifadhi mwandamizi katika bustani ya Royal Botanic, Kew, alisema kuwa aina yake huenda inaweza kustahimili ukame na magonjwa.
"Haina ugonjwa wa Panama hivyobasi huenda ina vitu muhimu vinavyoilinda dhidi ya magonjwa hayo," alisema.
"Hatujui hadi pale tutakapoifanyia utafiti ndizi hiyo, lakini hatuwezi kufanya utafiti huo hadi itakapookolewa."
Wanasayansi wa Kew waliutafuta mti huo wa ndizi nchini Madagascar na kugundua kwamba ulikuwa unaangamia duniani.

Hifadhi ya Maua
Wanatumai kwamba kuorodheshwa kwake miongoni mwa miti inayoangamia katika shirika la umoja wa mataifa la IUCN (International Union for Conservation of Nature utaangazia tatizo lake.
Dkt. Helene Ralimanana wa kituo cha uhifadhi nchini Madagascar anasema kuwa mmea huo ni miongoni mwa urathi mkubwa wa kisiwa hicho.
"Ni muhimu kuhifadhi ndizi hizo za porini kwa sababu zina mbegu kubwa ambazo zinaweza kutoa fursa ya kutafuta jeni ya kuimarisha ndizi inayopandwa," alisema.
Iwapo ndizi hiyo inaweza kulindwa kutakuwa na fursa za kukusanya mbegu zake na kuangalia jeni za mti huo.
Ndizi hiyo ya Madagascar inazalisha mbegu ndani ya tunda hilo, hatua inayomaanisha kwamba haipendezi kula.
Lakini kuchanganya ndizi hizo mbili kunaweza kuzalisha aina mpya ya ndizi ambayo inaweza kutumika na binadamu na vilevile kustahimili magonjwa.
Ndizi hiyo hukuwa kandokando ya pori ambapo ni rahisi kuharibiwa na hali mnbaya ya anga, ukataji wa miti, moto, mbali na kukata pori kwa lengo la upanzi.

Kwa nini ndizi zinaathiriwa rahisi na magonjwa?
Ndizi zinatoka katika eneo moja ikimaanisha kwamba zote ziko sawa. Hivyobasi iwapo ugonjwa umepatikana katika mmea mmoja unaweza kuenea kwa kasi katika mimea yote.

Tatizo ni lipi? Naweza kununua ndizi katika duka
Kwa sasa hilo linawezekana lakini sio katika siku za usoni.
Ugonjwa unaoathiri ndizi ya Cavendish umedhibitiwa barani Asia, na iwapo ungeenea nchini Marekani, ungeangamiza mmea wote wa ndizi.
Kila ndizi inayotumika kwa matumizi ya binaadamu inatoka katika mmea huo.

Je, tunaijua ndizi ya Madagascar?
Inajulikana kwa jina la kisayansi, Ensete perrieri, na imeorodheshwa kama mmea ulio katika hatari ya kuangamia.
Inapatikana katika pori la misitu ya kitropiki katika eneo la magharibi la taifa hilo ambapo inakabiliwa na hatari ya kukatwa kwa miti: Ni miti mitano pekee inayodaiwa kusalia katika pori hilo.

Comments