Featured Post

MREMA ASEMA: MAGUFULI USIHANGAIKE NA WAPITA NJIA, SONGA MBELE

* Asema, enzi zake wanaokejeli wangekiona cha mtema kuni
* Akumbushia dhahabu ya uwanja wa ndege, V.G. Chavda
* Bosi wa NCCR-Mageuzi naye arudi mbio CCM na watano

NA WAANDISHI WETU
WAKATI Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Dkt. Augustino Mrema, akimtaka Rais Dkt. John Magufuli kutohangaika na wanaombeza kwa kuwa ni "wapita njia", Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Tanzania Bara, Leticia Ghatti Mosore yeye ameamua kurejea CCM baada ya kukunwa na utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Mrema amesema wanasiasa wa upinzani wanaopinga jitihada za Rais Magufuli wanaendesha siasa za majitaka na akasema kitendo cha kumkejeli Rais hakivumiliki hata kidogo.
Katika mahoajino maalum, Mrema alisema Rais Magufuli hapaswikupoteza muda kusikiliza kelele za wapinzani ambao alisema wamefilisika kisiasa na kwamba yote yanayofanyika sasa Watanzania watakuja mkumbuka.
"Namuomba Rais Magufuli asipoteze muda wetu, yeye ndiye mwenye nyumba aendelee kusonga mbele, Watanzania watakuja kumkumbuka.
"Kejeli wanazozitoa wapinzani wenzangu si za kizalendo, na kama enzi zile nilipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wangethubutu kuniletea ujinga kama huu, hakika wangekiona cha mtema kuni," alisema Mrema.
Mrema alisema kwamba, mfumo wa vyama vingi ni vizuri kama vyama hivyo vitaendesha siasa za kistaarabu, kwa sababu lengo la upinzani ni kuikosoa serikali ili ijirekebishe.
"Lakini kwa sasa upinzani nchini umepoteza mwelekeo, mimi nakataa hii tabia iliyozuka ya kuzusha uongo wakati jambo unalijua ukweli wake, haiwezekani kupinga kila jambo linalofanywa na Serikali kama wanavyofanya sasa," alisema.
Ameisifu Serikali kwa kuthubutu kununua ndege ili kuimarisha sekta ya usafiri wa anga pamoja na utalii, ambayo alisema italiongezea taifa mapato badala ya kuendelea kutegemea kilimo ambacho kimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kutokana na uharibifu wa mazingira.
Aliongeza kwamba, japokuwa uchumi wa Tanzania unategemea kilimo, lakini katika hali ya sasa mvua hazinyeshi vyema na haiwezekani kuendelea kujidanganya kwamba kilimo ndio uti wa mgongo.
"Rais Magufuli ameona kipaumbele cha kukuza uchumi ni pamoja na utalii ambao utafanikiwa kwa kuwa na ndege zetu, yaani usafiri wa anga wenye uhakika.
"Nchi ya kilimo, mvua hainyeshi maana yake hatuwezi kukuza uchumi wetu. Sasa kuna maeneo ambayo hayaathiriwi sana na kunyesha kwa mvua kama ilivyo kwenye kilimo na ufugaji. Utalii ni sekta muhimu sana," alisema.
Mrema alisema kwamba, Serikali imeona umuhimu wa kulifufuana kuliimarisha Shirika la Ndege (ATCL) ambalo lilikuwa limekufa, hatua ambayo itasaidia kukuza uchumi kupitia utalii.
"ATCL haikuwepo, tunashindwa na nchi ndogo kama Rwanda ambayo ina ndege nyingi na hatua ya kununua ndege kwa fedha taslimu inaonyesha umakini wa serikali yetu," alisema.
Aliongeza kusema kwamba, Watanzania wanatakiwa kujua kwamba Tanzania ina vivutio vingi lakini inashindwa kupata watalii kwa sababu hakuna ndege.

Changamoto alizopitia
Mrema alisema kwamba, wakati akiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani alijitahidi kuwatetea wananchi na akajitoa muhanga, lakini alikosa madaraka makubwa hali iliyofanya baadhi ya watu aliowakamata kushindwa kuwajibishwa.
"Kama ingekuwa ndiyo kipindi hiki, hakika hata rasilimali zetu zisingeporwa na majambazi.
"Rasilimali zilikuwa zinatoroshwa, nakumbuka siku moja niliambiwa kuna dhahabu nyingi inatoroshwa kwenye ndege iko uwanjani, wala sikumwambia IGP nikaenda kule airport, wale watu wakakamatwa. Lilikuwa jambo kubwa, lakini sikuwa na madaraka, lile jambo lilikwisha hivi hivi," alisema.
Alizungumzia suala la mfanyabiashara Vidyadhar GirdharalChavda, maarufu kama V.G. Chavda, katika kashfa ya utoroshaji wa mabilioni ya fedha za mkopo wa kunusuru zao la mkonge.
"Chavda alikuwa amekopa benki fedha nyingi, Wazungu walitupatia ili tuweze kutoa mikopo, yeye badala ya kwenda kufanyia biashara akaenda Ulaya," alisema.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, V.G. Chavda kupitia kampuni zake za Tanfarms Ltd., Makinyumbi Estates Ltd., Centrepoint Investments Ltd., na Arusha Farms Ltd. alihusishwa katika matumizi mabaya ya Shs. 4,477,870,279.61 chini ya utaratibu wa Debt Conversion Programme.
Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Edward Oyombe Ayila, katika ripoti ya kamati hiyo alilieleza Bunge mwezi Novemba 1994 kwamba kulikuwa na uhusiano unaotia mashaka kati ya V.G. Chavda na mashamba yake na Subash Patel mwenye makampuni ya DECO ART, MM Motors, MM Garage, Hotel Sea Cliff, City Bureau De Change na Nimrod Mkono, Wakili wa kujitegemea ambaye pia ni Mkurugenzi katika makampuni ya AZANIA AGRICULTURAL ENTERPRISES, LIBERTY LEATHER SHOE LTD., AZANIA EXIMCO, n.k. (AIMS GROUP OF COMPANIES).
Mrema pia ameipongeza Serikali kwa hatua yake ya kuwakamata na kufungulia mashtaka watendaji wa Chama Kikuu cha Ushirika Kilimanjaro (KNCU) kutokana na vitendo vya ubadhirifu wa fedha za wakulima wa kahawa.
"Kuna watu tulikuwa na ujasiri wa kuwasemea watu. Nilijiuliza ni Mungu gani anayesababisha wakulima wa kahawa Kilimanjaro wasilipwe fedha zao.
"Mwaka 2013 nikamweleza Waziri wa Kilimo na Ushirika, kwamba kuna matatizo makubwa katika suala la wakulima wa kahawa Kilimanjaro, lakini hakuna kilichofanyika mpaka Rais Magufuli alipoingia madarakani na serikali yake imeweza kukifanya kile kilichoshindikana," alisema.
Mrema anakumbukwa pia kwamba, wakati akiongoza Wizara ya Mambo ya Ndani aliweza kupambana na biashara ya dawa za kulevya, ambapo mtuhumiwa wa dawa hizo, Nurdin Akasha, alikamatwa na kuswekwa ndani kabla ya kudaiwa kutoroshwa.

Makamu Mwenyekiti NCCR
Kwa upande mwingine, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa NCCR, Leticia Mosore, amesema aliondoka CCM baada ya kuona Ilani ya Uchaguzi hazingatiwi, lakini sasa amerejea kutokana na kuona kero zote zilizokuwa zikipigiwa kelele na wapinzani zinatekelezwa.
Mosore, ambaye aliambatana na wananachama wengine watano wa NCCR-Mageuzi waliorejea CCM, alisema kwamba sababu kubwa ni rushwa na ukosefu wa maadili, akidai kwamba zilikuwa hoja kuu za upinzani lakini kwa sasa zinatekelezwa ipasavyo na Serikali ya Awamu ya Tano.
"Kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais John Magufuli ameshughulikia kweli kweli rushwa na maadili. Serikali inafanya kazi kwa uwazi, ukusanyaji wa mapato ni mzuri. Pia imedhibiti matumizi yasiyo ya lazima," amesema.
Wanachama wengine wa NCCR-Mageuzi waliojiunga na CCM ni aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR, Mchata Mchata, aliyekuwa Katibu Jimbo la Segerea, Lilian Kitunga, aliyekuwa Katibu wa Wanawake Segerea, Nossy Chacha, pamoja na Vedalin Nicholaus na Eunice Zacharia.
Uamuzi huo ni kufuatia kwa kile alichodai kuwa vyama vya upinzani vinamkera kwani vimekuwa vikipinga kila kitu hadi yale mazuri.
“Kinachonikera kwenye upinzani ni kupinga kila kitu mpaka mazuri wakati hayo ndio tulikuwa tunayasema na mpaka mwisho hatueleweki tunataka nini, kwa hiyo mtu mzima kama mimi nimeona bora nirudi CCM.
''Kwa mfano wapinzani bajeti ya mwaka 2018/2019, Wapinzani walikataa kwa kupigia kura za hapana, wakati wananchi waliowachagua wanahitaji maendeleo, hivyo wapinzani hawawatendei haki wananchi wao, ambao wanateseka," alisema.
Mosore alitaja sababu zilizomshawishi kurudi CCCM kuwa, ni pamoja na kuweka nidhamu katika ofisi za Serikali, ambapo hivi sasa utendaji umekuwa wa wazi na weledi, ukusanyaji wa mapato ya Serikali umekuwa mzuri hali iliyopelekea Magufuli kununua ndege kwa kodi za Wananchi.
Aidha, alisema, Rais Magufuli kwa muda mfupi aliokaa madarakani mpaka sasa ameweza kujenga miundo mbinu ya kisasa, kama vile kujenga reli ya kisasa, kupeleka maji kutoa elimu bure  pmoja na Serikali kuweka mkazo wa kutumia electonic katika kukusanya kodi.
SOURCE: TANZANITE 

Comments