Featured Post

KWA UTEKELEZAJI HUU MWAKA 2020 WATAPATA TABU SANA



NA EMMANUEL J. SHILATU
NI takriban miaka miwili na nusu tangu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ale kiapo mnamo Novemba 5, 2015 cha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lakini katika kipindi hiki cha nusu muhula, tumeyaona haya yakitokea na kufanyika;-

1. Mapambano ya wazi wazi ya Serikali ya Rais Magufuli ya vita dhidi ya rushwa na ufisadi nchini. Leo hii Tanzania imepanda kwa nafasi 13 katika mwaka 2016 na 2017 na pia ikishika nafasi ya pili (2) kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
2. Serikali ya Rais Magufuli imefanikisha zoezi zima la Serikali kuhamia Dodoma.
Ni vyema tukakumbuka zoezi la kuhamia Dodoma liliasisiwa na kushindwa kufanyika toka enzi ya utawala wa awamu ya kwanza wa Rais Mwalimu Nyerere, lakini ndani ya kipindi kifupi cha miaka miwili tu Serikali ya Rais Magufuli imeweza kuuvunja mfupa huu mgumu.
3. Ujenzi wa miundombinu ya kipekee na ya kisasa. Kupitia Serikali hii ya awamu ya 5 ya Rais Magufuli tumeshuhudia ujenzi wa flyovers na ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha standard gauge inayotumia umeme na inayokwenda kwa kasi. Hii haijawahi kutokea tangu Tanzania iumbwe.
4. Serikali ya awamu ya 5 ya Rais Magufuli hutumia Shilingi bilioni 23 kila mwezi kulipia gharama za ELIMU BURE kuanzia elimu ya msingi mpaka kidato cha nne.
Mara ya mwisho Tanzania kushuhudia elimu ikitolewa bure ni katika utawala wa awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere.
5. Mafisadi Papa, wala rushwa Papa wamepandishwa mahakamani na wengine wanasota magerezani mpaka kesho. Katika miaka ya nyuma lilikuwa suala gumu sana kwa watuhumiwa “Mapapa” kuguswa tu, achilia mbali kupandishwa mahakamani.
6. Tumeshuhudia akisimamia kwa vitendo kauli yake ya Tanzania ya Viwanda.
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani, zaidi ya viwanda vikubwa na vidogo 3,000 vimezinduliwa na vinafanya kazi. Uwepo wa idadi kubwa ya viwanda unasaidia sana kupunguza tatizo la ajira nchini.
7. Uwajibikaji na uadilifu kwa watumishi wa umma umeongezeka na kuimarika vilivyo. Leo hii mtumishi wa umma hana majivuno, kiburi wala dharau kwa wale anaowahudumia.
Siku hizi watumishi wa umma wanawahi makazini, wanachapa kazi nyakati zote na wanazingatia ubora na umakini wa kazi.
8. Suala la matabaka ndani ya jamii linazidi kupungua kwa kasi tangu utawala wa awamu ya 5 uingie madarakani.
Leo hii watoto wa maskini nao pia wanakwenda shule kupitia sera ya elimu bure; hakuna tena ubabe wa dhuruma mahakamani, kwenye masuala ya ardhi; leo hii hakuna tena zile kauli kandamizi za “unanijua mimi nani” ama “Kijana kaa mbali, nitakupoteza”.
Hakika watu wanyonge maskini nao pia wanafurahia maisha vilivyo, hakuna tena ubabe wala matabaka.
9. Serikali ya Rais Magufuli imeimarisha na kuzingatia suala la amani na uhuru wa kidemokrasia ndani ya nchi. Mathalan Machi 5, 2018 tumesikia Umoja wa Mataifa (UN) ukimpongeza Rais Dkt. Magufuli kwa kudumisha amani na usalama ndani na nje ya Tanzania.
10. Kasi ya viongozi wa upinzani wakubwa kujiunga na CCM imekuwa mkubwa sana. Tumeshuhudia Madiwani, Wabunge na viongozi waandamizi wa upinzani wakijiunga na CCM ili kumuunga mkono Rais Magufuli kwa yale mambo mazuri ya kiutendaji anayoyafanya.
Kujiunga kwa upinzani na dalili tosha ya watu kuridhishwa na kiwango kikubwa cha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2015 – 2020.
11. Kufufuka kwa mashirika ya umma yaliyokuwa taabani. Tumeona Shirika la Ndege (ATCL), Reli (TRL) na la Simu (TTCL) yakipata uhai mara baada ya Dkt. Magufuli kuingia Ikulu.
Mathalan, upande wa ndege jumla ya ndege 6 mpya zimeshanunuliwa, upande wa simu Serikali ya awamu ya 5 ilinunua hisa zote za shirika za simu na hivyo kuanza kuimiliki kwa asilimia mia na kuanza kuliboresha shirika. Matokeo yake imeweza kupokea gawiwo la shilingi bilioni 1.5.
12. Tumeshuhudia Serikali ikianzisha na kufanya miradi mikubwa na ya kihistoria ya kimaendeleo.
Mathalan, tumeshuhudia ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme kwa kiwango cha Standard Gauge; Mradi wa ujenzi wa umeme wa Stiegler's Gorge utakaokuwa chanzo kingine cha umeme na hivyo kupunguza tatizo la umeme nchini; Ujenzi wa flyovers za Tazara na Ubungo ambayo itasaidia kupunguza msongamano wa magari mkoani Dar es Salaam.
13. Kufutwa kwa kodi mbalimbali za kilimo, Serikali kusimamia masoko ya bidhaa za wakulima na hivyo kufanya kilimo kuwa na tija nchini.
Wote ni mashuhuda kwa namna gani Wakulima wa Korosho nchini wanavyonufaika, ambao walikuwa wakiuza korosho kwa bei Tsh. 800 kwa kilo hapo awali lakini tangu Rais Magufuli aingie Ikulu bei ya korosho imepanda hadi kufikia bei ya Tsh. 4,000 kwa kilo. Maboresho hayo yapo hadi kwenye mazao mengine.
14. Tumeshuhudia Serikali ya awamu ya 5 ikipambana vilivyo na adui maradhi.
Mathalan, vifo vya wajawazito vimepungua kwa wastani wa kitaifa wa 556/100,000; Idadi ya Wanawake wanaojifungulia vituoni imefika wastani wa kitaifa wa asilimia; Upatikanaji wa dawa muhimu ni kwa asilimia 89 n.k. Pia tumeona kaya nyingi zikijiunga na mfuko wa afya ya jamii.
15. Tumeshuhudia Serikali ikiweka uwazi kwenye mikataba na uchunguzi wa rasilimali za Taifa na kuweka makubaliano mapya yenye tija Mathalani tumeona uwazi wa sekta ya madini ya dhahabu, almasi na Tanzanite ambapo Taifa tumeona namna ambavyo tulivyokuwa tukiibiwa na Serikali kuweka mikakati mipya ya kutokuibiwa tena.
Kama haitoshi tumeshuhudia wawekezaji wakibanwa vilivyo juu ya mikataba isiyokuwa na tija kwa Taifa. Ni Serikali ya Rais Magufuli iliweka uthubutu wa kuwabana wawekezaji wa madini wa  Acacia iliyozaa matunda kwa Serikali ya Tanzania kumiliki asilimia 16 ya hisa katika makampuni ya uchimbaji wa madini, Serikali kupata gawio la faida ya madini ya asilimia 50 kwa 50. Yote haya yamewezekana kwa sababu ya uzalendo wake Rais Dkt. Magufuli.
Kwa utekelezaji huu unaofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais Magufuli, wapinzani watapata tabu sana kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020.

Comments