Featured Post

JE, UNAJUA AKAUNTI YAKO YA FACEBOOK ITATUMIWAJE UKIFA?



BERLIN, UJERUMANI
MAHAKAMA ya juu nchini Ujerumani imeamuru kuwa wazazi wa binti aliyefariki wapate haki za kuingia kwenye akaunti ya Facebook ya binti yao, kwa mujibu wa sheria za mirathi nchini humo.
Mahakama hiyo imesema data za mtandaoni zipewe hadhi sawa kama vile ilivyo kwa barua binafsi au kumbukumbu nyingine binafsi na kurithishwa kwa wanafamilia.

Shauri hili lilihusisha wazazi wa binti wa miaka 15 aliyepoteza maisha kutokana na kuigonga treni mwaka 2012.
Walitaka kibali cha kuingia kwenye anuani yake ya Facebook ili waweze kufanya uchunguzi kubaini kama binti yao alidhamiria kujitoa uhai.
Facebook ilikataa kutoa kibali baada ya kifo cha binti huyo, ikijitetea kuwa hiyo ni anuani ya mtu binafsi.
Sera mpya za Facebook, Kampuni inaruhusu wanafamilia, walezi kuingia na kuitumia kwa kuruhusu kubadili ukurasa kwa ajili tu ya maombolezo mtandaoni au kuifuta kabisa (after-death controls).
Mahakama ndogo iliwaunga mkono wazazi mwaka 2015, ikieleza kuwa data za muhusika katika Facebook ziko kwenye sheria ya mirathi.
Lakini mwaka 2017, Facebook ilishinda rufaa kwa misingi kuwa mkataba kati ya binti na Kampuni ulikwisha baada ya kifo, hivyo mkataba huo hauwezi kuhamishiwa kwa wazazi.
Shauri lilifikishwa kwenye mahakama kuu na sasa wazazi wameripotiwa kuhodhi anuani hiyo.
Jaji wa mahakama hiyo, Ulrich Hermann, alisema ni kawaida kurithisha vitu kama barua na maandiko mengine ya marehemu kwa familia na haoni sababu ya anuani ya digitali itazamwe tofauti.
Zaidi ya hayo mahakama imesema wazazi wana haki ya kufahamu mtoto wao alikuwa anawasiliana na nani.

Ni kwa jinsi gani unapenda kukumbukwa utakapofariki?
Miezi micheche kabla ya kupoteza maisha, Bibi yangu alifanya uamuzi.
Bobby, kama alivyokuwa akiitwa na marafiki zake (kwao ni kizazi cha majina ya a.k.a) alikuwa mke wa mkulima ambaye si tu alinusurika katika vita ya pili ya dunia lakini pia alikuwa mahiri wa kutunza vitu, ilikuwa ni taratibu za kuishi alizojiwekea baada ya Uingereza kurejea katika uimara wake baada ya vita.
Hivyo aliendelea kutunza bahasha na makaratasi yanayotokana na maboksi ya vyakula kwa ajili ya kuandikia na kunakili orodha mbalimbali.
Alitunza pia picha za watu wa familia yake, aliendelea kutunza barua za mapenzi alizokuwa akitumiwa na babu yangu alipokuwa safarini. Nyumba yake ilikuwa na kumbukumbu nyingi sana.
Katika miezi michache kabla ya kifo chake, mwelekeo ukabadilika kumbukumbu zote zikaanza kutolewa. Kila mara nilipomtembelea hulijaza gari langu na vitu mbali mbali, katoni za juisi ya machungwa, vitabu, bilauri.
Kumbukumbu zote alianza kuzitoa nyumbani. Alituma picha zilizofifia kwa watoto wake, wajukuu na marafiki, zikiwemo barua zilizoandikwa zikiwa na aya ambazo wazi kabisa zilieleza aliyoyapitia maishani na mambo mengineyo.
Aprili 9, 2018 usiku kabla ya kifo chake alituma barua kwa marafiki wa utotoni wa marehemu mumewe.
Kwenye bahasha aliambatanisha picha za babu yangu na rafiki yake wakicheza walipokuwa watoto, aliandika ''Lazima uwe nazo,'' aliandika ilikuwa kama amri lakini pia ombi, labda akimaanisha vitu hivi si vya kuvipoteza au kuvisahau. Saa chache baadae alifariki akiwa kwenye kiti chake alichokipenda sana.
Siku hizi tunatunza kumbukumbu zetu kwenye intaneti. Kuna Facebook ambayo hurekodi matukio yetu muhimu ya maisha, Instagram ambapo tunatunza tunayoyapenda, Gmail ambayo hutunza mazungumzo yetu na YouTube ambayo hutangaza namna tunavyoendelea, tunavyozungumza na tunavyoimba. Tunakusanya kumbukumbu hizi ziweze kuishi muda mrefu.
Je inatosha? Tunatunza kile tunachoamini kuwa ni muhimu, lakini je kama tunakosa vitu vilivyo muhimu? Inakuwaje kama tunakosa kitu muhimu kwenye maneno yetu au kwenye picha zetu?
Ni kwa namna gani inaweza kuwa vyema kutunza kila kitu, si tu mawazo yetu kwa maandishi na picha zinazoonyesha maisha yetu, lakini mawazo yetu yote akilini: Kila kitu tunachokijua na vyote tunavyovikumbuka, mambo ya mapenzi na kuvunjika moyo, nyakati za ushindi na masikitiko, uongo tunaoueleza na ukweli tunaojifunza, ungeweza kuhifadhi kila kitu kichwani kama kwenye mfumo wa kompyuta?
Kuna wahandisi wanafanyia kazi teknolojia ambayo itaweza kutengeneza kopi za akili zetu na kumbukumbu zitakazoishi hata baada ya kifo.

Karatasi ya Kaboni
Ninatunza barua za Bibi kwenye kablasha lililo kwenye meza yangu. Pia nina picha zake kwenye ukuta jikoni kwangu, na vile vitabu vya zamani ambavyo vimekuwa vikuukuu vikiwa bado havijasomwa. Hizi ni njia ambazo ninamkumbuka na kumbukumbu zake nimezitunza kwenye makaratasi.
Lakini ningeweza kufanya zaidi kutunza kumbukumbu hii?
Bibi wa Aaron pia alifariki hivi karibuni. ''Kilichonishtua ni kuwa ni kwa namna ambavyo hakuna kumbukumbu za kutosha zilizobaki,'' Mjukuu wake mwenye miaka 30 ananiambia ''ameacha vitu vyake vichache. Nina shati lake la zamani ambalo huwa ninalivaa ninapokuwa nyumbani."
Kifo chake kilimhamasisha kujiunga na taasisi ya Eterni.me huduma ya mtandao ambayo huhakikisha kumbukumbu za mtu aliyefariki zinatunzwa mtandaoni.
Inafanya kazi hivi:
Wakati ukiwa hai unaipa kibali taasisi hiyo kuweza kuingia kwenye mtandao wako wa Facebook, Twitter na anuani za barua pepe, weka picha na kuonyesha maeneo mbalimbali ulipokuwa na vitu ulivyoviona, data hurekodiwa, kuchujwa na kuchambuliwa kabla ya kupelekwa kwenye teknolojia ya Avatar ambayo itakuwa ikikusoma kadiri unavyoendelea kuishi.
''Ni katika kuepuka hali ya kutokumbukwa siku za usoni," anasema Marius Ursache mmoja kati ya wabunifu wa Eterni.
''Wajukuu wa wajukuu zako watazitumia kumbukumbu zako, kwa mfano picha za familia, mawazo yako, matukio ya kukumbukwa ya familia na mawazo yako kuhusu mada mbalimbali na hata nyimbo ulizowahi kuimba lakini hazikuchapishwa."
CHANZO: BBC

Comments